Brotherhood yalaani kukamatwa kwa Badie
![]() |
Kiongozi wa Muslim Brotherhood yuko kizuizini huku akikabiliwa na tuhuma za kuchochea ghasia na mauaji |
Vugu vugu la Muslim Brotherhood
limelaani kukamatwa kwa kiongozi wake Mkuu Mohammed Badie, kwa tuhuma za
kuchochea ghasia na mauaji.
Msemaji wa kundi hilo amesema kukamatwa kwa
kiongozi huyo ni njama ya kulipiza kisasi mapinduzi ya umma
yaliyomuondoa madarakani Rais wa zamani Hosni Mubarak mwaka wa 2011.
Badie alikamatwa na maafisa wa polisi kutoka makaazi yake karibu na
kitovu cha maandamano ya wafuasi wa Brotherhood Mjini Cairo.
Jeshi la Misri lilivunja kambi hizo
wiki jana ambapo kulitokea maafa ya raia wengi. Wakati huo huo Aliyekua
Makamu wa Rais Mohamed ElBaradei anakabiliwa na mashtaka ya kusaliti
imani ya taifa.
Bw ElBaradei aliondoka nchini Misri baada ya
kujiuzulu kufuatia hatua ya jeshi kuvunja kambi za wapinzani na
kusababisha maafa ya mamia ya watu.Utawala wa mpito umetangaza hali ya
hatari nchini Misri na kumekua na operesheni kali dhidi ya wafuasi wa
Rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Morsi.
Hapo Jumanne Vugu vugu la Muslim Brotherhood
limewaomba wafuasi wao kuendelea na maandamano kushinikiza jeshi
imrejeshe madarakani Bw. Morsi. Kwenye mkutano na waandishi wa habari
mmoja wa viongozi wa chama cha Justice And Freedom Party, mrengo wa
kisiasa wa Brotherhood alisema kukamatwa kwa kiongozi wake
hakutadidimiza harakati zao.
Naibu kiongozi wa vugu vugu hilo Mahmoud Ezzat
ametangazwa kama kaimu kiongozi. Mohammed Badie amekua akiongoza
maandamano ya wafuasi wa Bw Morsi. Hata hivyo aliingia mafichoni baada
ya serikali kutangaza onyo la kuvunja kambi za waandamanaji.
Kiongozi huyo anakabiliwa na mashtaka ya
kuchochea ghasia na mauaji ya raia wanane waliopinga Muslim Brotherhood.
Mzozo wa kisiasa nchini Misri umepelekea mauaji ya watu 900 na maelfu
kujeruhiwa.
Mauaji hayo yamepelekea laana za kimataifa,
baadhi ya wafadhili wakitarajiwa kukutana Jumatano kuamua ikiwa
watasitisha msaada kwa utawala wa Misri.
Wakati huo huo Misri imetangaza siku tatu za
maombolezi ya kitaifa kufuatia mauaji ya maafisa 24 wa polisi katika
Rasi ya Sinai. Wanamgambo wa kiisilamu wamelaumiwa kwa kutekeleza mauaji
hayo.Chanzo BBC SWAHILI.
No comments:
Post a Comment