Friday, August 30, 2013

MATUKIO YANAYO ENDELEA KUHUSU SYRIA.

Matukio ya Kisiasa

Marekani inapanga kuingilia kijeshi Syria

►Marekani inaendelea kusaka"Muungano wa kimataifa" katika maandalizi yake ya kuishambulia Syria.Hata hivyo,haijaondowa uwezekano wa kuhujumu peke yake baada ya mshirika wake muhimu,Uingereza, kukataa kuingilia kati.
►Marekani inaendelea kusaka"Muungano wa kimataifa" katika maandalizi yake ya kuishambulia Syria ikibidi, kutokana na tuhuma za serikali ya nchi hiyo kutumia gesi ya sumu dhidi ya raia. Hata hivyo, Marekani haijaondowa uwezekano wa kuhujumu peke yake baada ya mshirika wake muhimu, Uingereza, kukataa kuingilia kati.
Tuanzie lakini nchini Syria kwenyewe ambako wataalamu wa Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa wanatarajiwa kuyatembelea kwa mara ya mwisho hii leo yale maeneo ya karibu na mji mkuu Damascus yanayosemekana gesi za sumu zilitumika na kuangamiza maisha ya mamia ya watu Agosti 21 iliyopita, kabla ya kuondoka Syria kesho Jumamosi.
Kutokana na kitisho cha Urusi na pengine hata China kutumia kura zao za turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na baada ya bunge la Uingereza kulipinga pendekezo la serikali kuingilia kijeshi nchini Syria, ikulu ya Marekani imedokeza Rais Barak Obama huenda akaamua kuchukua hatua ya upande mmoja dhidi ya utawala wa Syria.
"Marekani itaendelea kushauriana na serikali ya Uingereza, mmojawapo wa washirika wetu na rafiki wa karibu zaidi,lakini uamuzi wa rais Obama utatuwama zaidi katika suala la masilahi ya Marekani," amesema msemaji wa baraza la usalama wa taifa la Marekani Caitlin Hayden.
Rais Obama anahisi masilahi ya Marekani yako hatarini na kwamba nchi zinazovunja sheria za kimataifa kuhusu silaha za kemikali zinalazimika kujieleza .
Marekani isaka ushirika wa kimataifa dhidi ya Syria
Kwa upande wake waziri wa ulinzi wa Marekani, Chuck Hagel akizungumza na waandishi habari mjini Manilla Philippines amesema:
"Msimamo wao unahusu kuendelea kusaka muungano wa kimataifa utakaochukua hatua za pamoja.Anahisi kuna idadi kubwa ya nchi zilizoelezea wazi wazi msimamo wao dhidi ya ya kutumiwa gesi za sumu.Kwa hivyo wataendelea kushauriana na washirika wao,na marafiki zao."
Waziri wa ulinzi wa Marekani amesema Washington itaheshimu uamuzi wa bunge la Uingereza ambako wabunge 285 dhidi ya 272 wamepinga jana usiku mswaada uliopendekezwa na waziri mkuu David Cameron kuhusu misingi wa kuingilia kati kijeshi nchini Syria.
Urusi inasema itapinga uamuzi wowote wa kijeshi dhidi ya Syria
Jana usiku pia mkutano wa wanachama 5 wenye kura ya turufu katika baraza la Umoja wa mataifa ulimalizika dakika 45 tu baada ya kuanza.Wajumbe walishindwa kuafikiana.
Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi mshirika wa jadi wa Syria amesema Urusi itapinga azimio lolote la baraza la Usalama litakalozungumzia uwezekano wa kutumiwa nguvu dhidi ya Syria."
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ameondowa uwezekano kwa Ujerumani kushiriki kijeshi nchini Syria.
Wachunguzi wa Umoja wa mataifa wakamilisha shughuli zao leo
Akijivunia uungaji mkono huo wa Urusi,rais Bashar al Assad ameahidi kuihami nchi yake "dhidi ya uvamizi wa aina yoyote" wa nchi za magharibi,na kusisitiza nchi yake "imepania kuuteketeza ugaidi" akiwafungamanisha kwa mara nyengine tena waasi na magaidi."
Jana wataalam wa Umoja wa mataifa walitumia saa nne kuvichunguza vituo vya kitongoji cha mashariki cha mji mkuu. Hii leo wamekwenda katika hospitali ya kijeshi ya Mazze wanakotibiwa wahanga wa mashambulio ya gesui za sumu kabla ya kuondoka Damascus kesho jumamosi.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef

CHANZO :DW.DE

No comments:

Post a Comment