Wasifu wa AL-HABIB SAYYID AHMAD BIN HUSSAIN BIN SHAYKH ABI-BAKAR BIN SALIM, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie.
Ho, tusijiache na fahamu ya kawaida ya tamko hilo, kwani Sharif Junaid, umashuhuri wake, alikuwa akipiga mbali. Tamko Raihana, katika tangamano kama hili alilitumia kwa mara ya mwanzo Shekhe Mkubwa wa Tariqa na Haqiqa, naye ni Al-Junaid wa Baghdad. Alilitumia kwa Bwana Ahmad Bin Abi Hawari – Radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie . Na maana yake ni yule Walii mkubwa ambaye wengine, kwa kusikia uturi wa harufu yake, hupata jazba na hamasa ya kushamiri kuwania Maqamati za juu na juu tena. Na hapa tunazungumza malimwengu ya mbali zaidi kuliko Arshi.
Na mwahala pengine al-Habib Umar Bin Sumeit akimtaja Bin Hussain kuwa: “Ni al-Habib ambaye yeye mzima, wote ni nuru.”
Unguja, na sasa tunasikia Daresalaam pia, kunafanywa Hadhara ya Bau-Saudan, yaani Hadhara ya Ajabu ya Zama, Sheikh Abdallah Bin Ahmad Bin Abdallah Bin Muhammad Bin Abdur-Rahman Bin Muhammad Ba-Saudan – Mwenyezi Mungu atunufaishe naye na elimu zake. Katika kitabu chake kinachoitwa Hadaaiqi-l-Arwaa, yaani Bustani ama Vitale vya Roho, anazungumza kile tutachokiita ‘Ngazi za dhikri’. Anataja ngazi moja, na hiyo anaita ‘Sultani wa dhikri’. Yaani dhikri ya mwili, mwili wote, nje na ndani, kiungo kwa kiungo, kia kwa kia, mshipa kwa mshipa, damu na nyama na nywele. Ni dhikri adhimu kweli hii, na ndiyo inayoashiriwa kwenye dua ya Bwana Mtume SallaLLahu ‘Alayhi Wasallam anaposema: “Ewe Allahumma, Jaalia kwenye moyo wangu nuru, na kwenye usikivu wangu nuru, kwenye macho yangu nuru...”, mpaka mwisho wa dua. “Hakika”, anasema Sheikh Abdallah Ba-Saudan: “Mwili
wote, nje yake na ndani yake, na pande zake sita, zinataka nuru hii
adhimu. Na Mashekhe wengi hawataji dhikri nyingine iliyo juu ya hapo.
Ukweli wa mambo, hali haiko hivyo. Ukweli ni kwamba, Sultani ya dhikri
ina mwanzo na mwisho.”
Sheikh Ahmed Islamu, mojawapo kati ya watu waliokuwa wakishikamana sana na Bin Hussain, anasema kwamba Bin Hussain alikuwa wote makini tupu alipokuwa akiisoma ile dua ya Al-Murshidul Kamil, al-Habib Ali Bin Muhammad Bin Hussain Al-Habshi inayoanza kwa maneno haya: “Allahumma Salli wa Sallim Billisaani-l- Jamia, Fi-l-Hadharati-l-Wasia, ‘Alaa Abdika-l-Jamia, Li-l-Kamaalaati-l-Insaniyyah...na humo, al-
Habib Ali Al-Habshi anaomba nuru hii hii aliyoomba Bwana Mtume SallaLLahu ‘Alayhi Wasallam, ambayo Sheikh Abdallah Ba-Saudan anaiita: Sultani wa dhikri zote.
Wasifu huu wa al-Habib, as-Sayyid Ahamd bin Hussain ni kutoka katika sherhe ya Ratib al-Attas, uradi ambao bwana wetu Bin Hussain aliupa umuhimu mkubwa . Sherhe hiyo iitwayo Lulu na Almasi ipo mbioni kuchapwa.