Thursday, September 19, 2013

KONTENA ZA SAMAKI WABOVU ZAKAMATWA

MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) imekamata kontena mbili zenye urefu wa futi 46 kila moja zenye samaki wanaodaiwa kuwa wameoza, zikiwa zimefichwa eneo la Tabata jijini Dar es Salaam zikisubiri kupelekwa sokoni Feri.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, msemaji wa TFDA, Gaudencia Simwanza alisema samaki hao waliingizwa nchini kutoka China kupitia Kampuni ya Sais Boutik, na kwamba taarifa zake zilizagaa tangu wiki iliyopita.

Alisema samaki hao wenye thamani ya dola za Marekani 6,700, walikamatwa baada ya Kampuni ya Sais Boutik kukwepa kuwasilisha nyaraka za mzigo huo kwenye mamlaka zinazohusika ili kuthibitisha ubora wake kisha uweze kulipiwa ushuru.

“Hawa samaki waliombewa kibali cha kuingizwa nchini, lakini kampuni hiyo baada ya kuwaingiza walitakiwa wapeleke nyaraka zao TFDA ili iweze kuthibitisha kwa kugonga mhuri kuashiria kuwa mzigo huo ulikuwa salama kuingizwa sokoni,” alisema.

Gaudencia alisema kati ya kontena hizo mbili, moja ilikuwa na samaki aina ya kibua, ambao ndio waliogundulika kuwa wameoza baada ya walaji kuwanunua.

“Makontena hayo ya samaki tuliyakuta yakiwa yamefichwa nyumbani kwa Saidi Makoro wakiwa katika mazingira machafu na ya kutisha,” alisema.

Aliongeza kuwa baada ya kuwakamata samaki hao, waliwapeleka kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini kama walikuwa na madhara au la.

Hata hivyo, hadi wanawakamata samaki hao kulikuwa hakuna mwananchi aliyedhurika kwa kuwa wengi waliwabaini mapema kuwa wameoza, hivyo waliweza kuwarudisha haraka.

Gaudensia alisema kuoza kwa samaki hao huenda kumechangiwa na wamiliki wake kushindwa kufuata njia bora zinazotakiwa.

No comments:

Post a Comment