Friday, September 20, 2013

Mama Mwanamwema Shein, Ahimiza Jamii Kuwekeza katika Madrasa.

Na Mwantanga Ame

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein, ameitaka jamii kuona umuhimu wa kuwekeza katika shughuli za madrasa ili kuweza kupata kizazi kilichobora.

Mama Shein, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na walimu na wanafunzi wa Madrasa Hidayatu ya Kidoti Nungwi, Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, baada ya kukabidhi vifaa mbali mbali kwa ajili ya matayarisho ya ufunguzi wa Madrasa hiyo, iliyojengwa kwa mchango wa ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

Akitoa nasaha zake kwa niaba ya Mama Shein, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Suleiman Iddi, alisema ni vyema jamii ikaona umuhimu huo kwa vile utaweza kujenga kizazi kilicho bora kutokana na maeneo hayo huchangia imani njema ya dini ya kiislamu.

Alisema nyingi ya Madrasa hivi sasa zimekuwa zikionekana kama vile si maeneo ya msingi yanayohitaji kuwekezwa katika hali ya ubora, jambo ambalo jamii inapaswa kuona inabadili tabia hiyo.

Alisema maeneo ya madrasa hivi sasa yanahitaji kuonekana kuwa bora, ili yaweze kwenda sambamba na mafunzo yaliomo katika dini ya kiislamu, ambayo kwa kiasi kikubwa yanasaidia kuandaa kizazi kilicho bora.

Alisema sehemu kubwa ya jamii ya kiislamu inasahau umuhimu wa kuwekeza katika madrasa na kuwa tayari kusaidia maeneo mengine ambayo hayana msaada katika kujenga jamii iliyo na umani za kidini.

Alisema mfano halisi hivi sasa baadhi ya watu wamekuwa wakitoka nje ya misingi ya kidini kuitana majina ambayo yanapingana na uislamu, jambo ambalo kama wangelikuwa na elimu ya kutosha wangeliepuka.

Kutokana na hali hiyo, Mama Shein, alisema ni lazima jamii kuanza kuziona kasoro hizo na kuachana na mambo yalio nje ya misingi ya kiislamu.

Mama Asha, aliwakabidhi madrasa hiyo, vifaa mbali mbali, vikiwemo sare kwa wanafunzi na walimu wa madrasa hiyo, misahafu 210, Vijuzuu 200, pamoja na meza, kabati na viti ambapo vyote vinathamani ya shilingi milioni 12.

Baadhi ya viongozi wa Mkoa huo akiwemo Mkuu wa Wilaya Riziki Juma Simai, alipongeza hatua ya Mama Shein, kuona madrasa hiyo inakamilika kwa wakati, kwani itachangia utoaji wa elimu bora kwa watoto wa kijiji hicho.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, anatarajiwa kuifungua madrasa hiyo kesho, ambayo ina wanafunzi wapatao 358.

No comments:

Post a Comment