Wasifu wa SHAYKH SULAYMAN BIN MUHAMMAD AL-ALAWIY, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie.
Alipofariki
Shaykh Suleimani, Sharif Junayd alimlilia hivi, “akili yangu amkani
nahisi zimenipotea. Kwa mazito malemevu nimo kwenye ulimwengu mwengine.
Si bida’a ikiwa nimezisahau hisi zangu, nikawa wote nimekufa ganzi.
Kwani masiku yamenielemea kwa mambo mazito, kwa msiba ulionivunjavunja
nisibaki kitu. Kwa kuondoka Ustadh wetu Suleimani, taa ya ilmu na hazina
ya ‘irfaani. Bahari ya ilmu, mwenye kuiendea huchota johari atakazo na
dhahabu pia. Jamali ya zama, mwema wa utajo. Hatajwi kwa baya tangu
ujana wake. Mwingi wa kurejea kwa Mola wake, mcha Mungu mwingi wa
kurukuu mwingi wa kusujudu, mwenye kuhuisha ashari kwa Qurani. Zagao za
amali zake njema ziwazi na zenye kuonekana. Ni shani kubwa ilioje, yiyo
ikiwa ya nuru. Sifa ngapi zenye kuhimidiwa na magapi matukufu ya
kumtenga alikuwa nazo, na ambazo maneno yangu hayafiki. Wara’a fika na
khuluka zenye kuridhisha na uthabiti ambao kamwe wa pili hana, na haiba
na murua na vumilia ya maudhi na khashya ya rahmani. Kalelewa Unguja
kwenye mabustani ya ilmu anachuma matunda yenye wingi wa utamu, kapokea
kwa wakuu ma-Bwana niwasifu vipi wanazuoni hao rabbani. Mtaje shihabu
wetu khasaa mwana wa Sumeyti, mwana kwea wa juu kweye mbingu za ilmu.
Wakammiminia siri zao na kwazo akawazidi kimo wote wa rika yake, ai moyo
wangu na huzuni zangu leo kaniondokea. Hayuko tena kwenye duru wala
kwenye majengo, ai moyo wangu na simanzi zangu. Kwani ye' ni mwezi wa
mwisho kuduru kwenye midani, sasa kumekuwa kiza tangu kuuka kwake na
totoro imetawala. Ewe ni kuu huzuni zangu na mkubwa mno msiba wangu,
furifuri machozi yangu furifuri yanamiminika. Nikiuambia moyo subiri,
huniambia subira si uwezo wangu.... Ewe baba wa Zamil ghafula umeondoka
na kughibu, ewe pweke wa zamani umeghibu hali ya kuwa sisi kubwa haja
yetu kwako, katika kila shani.... Na vikulilie vitivo vya ilmu. Na vilie
vururu visiwe na kizuizi. Ikulilie Unguja kwani buruji ya ilmu nguzoze
zimedamirika. Naapa machozi na kilio changu yatadumu urefu wa zama.
Kaburilo likiwa ardhini ewe mkuu wa matukufu basi lilo liko kwenye pepo
ya Jinani.... furahika basi kwani milele utabaki utajo wako mwema na huo
ni umri wa pili. Lala usingizi macho tele kwenye bustani ya kaburi,
hali umefurahika kwa Raufu na Rayhani.... Ewe Rabbi huyu mja Wako, mgeni
Wako, hela mpokee kwenye dari ya ridhaa na nyumba ya amani. Na
mwonjeshe kwa fadhila Zako maji ya ridhaa na afua Yako, na mkuruba na
maghfira Yako. Na tupe ujira Ewe Rabbi na tupe badili miongoni mwetu, na
tupe kheri na ihnsani. Na juu ya kaburi lake yaanguke mawingu ya radhi,
na yawe ya kudumu urefu wa zamani."
Wasifu
huu wa Shaykh Sulayman al-Alawiy umetoka katika kitabu juu ya maisha ya
al-Habib al-Imam Ahmad bin Hassan al-Attas, radhi za Mwenyezi Mungu
ziwaalie wote wawili, kitabu kilicho njiani kuchapwa.