Saturday, August 10, 2013

FUNGA YA SITA BAADA YA RAMADHAN

Funga ya Sita ni Sunna inayopatikana katika Mwezi huu wa Shawaal baada ya Kumaliza Mwezi Mtukufu wa Ramadhani  Mtume (S.A.W) Rehma za M/Mungu zimshukie Juu yake na Amani anasema "Atakeyefunga Mwezi wa Ramadhani kisha akafuatilia (kufunga) siku sita katika mwezi wa Shawaal (anakuwa) kama aliyefunga maisha yake yote,”

Na hii ni kwa sababu mtu anapofunga mwezi mmoja wa Ramadhani, anapata thawabu ya kufunga miezi kumi, kwa sababu mtu anapotenda Jema moja hulipwa kumi badala yake. Na anapofunga siku sita katika Shawwal, anakuwa mfano wa aliyefunga siku sitini. Ukijumlisha funga ya Ramadhani na funga ya sita, unapata miezi kumi na miwili, na kwa ajili hiyo anakuwa mfano wa aliyefunga mwaka mzima. Na mtu anapoendelea hivyo maisha yake yote anakuwa mfano wa anayefunga maisha yake yote”.
 
NAMNA YA KUFUNGA.

Imam Annawawi ambae ni katika Maulamaa wakubwa wa madhehebu ya Imam Shafi anasema;

"Ni vizuri kufunga siku sita mfululizo mara tu baada ya kumalizika sikukuu ya mwanzo, na atakayefunga siku sita mbali mbali katika mwezi wa Shawaal , pia inakubaliwa”.

Amma Imam Ahmed bin Hanbal anasema;
“Ukifunga mfululizo au ukizifunga siku sita tofauti katika mwezi wa Shawaal yote ni sawa tu.”

UZINDUZI.

Maulamaa wanasema kuwa;
‘Lazima mtu atimize Ramadhani yake kwanza, ndiyo aweze kufunga sita. Yaani ikiwa mtu anadaiwa katika Ramadhani, basi lazima alipe kwanza deni lake lote kisha ndio afunge sita.’

Na hii ni tafsiri ya kauli ya Mtume  (S.A.W) Rehma za M/Mungu zimshukie Juu yake na Amani aliposema;
ATAKAYEFUNGA Mwezi wa Ramadhani KISHA akafuatilia (kufunga) siku sita…”

Wakasema kuwa kutokana na kauli hii, Mtume  (S.A.W) Rehma za M/Mungu zimshukie Juu yake na Amani hapa anasisitiza kuwa mtu lazima kwanza afunge Mwezi wa Ramadhani, KISHA afunge sita. Na ikiwa mtu ana deni la kufunga, basi huyo anakuwa hakufunga mwezi wa Ramadhani, na kwa ajili hiyo ikiwa anazitaka thawabu zilizotajwa katika hadithi hiyo, basi inampasa kulipa deni lake kwanza, kisha ndiyo afunge sita.
 
M/Mungu ndiye Mjuzi .
 

No comments:

Post a Comment