Saturday, August 31, 2013

KONGAMANO NA MSIMAMO WA MANSOUR KUHUSU KUFUKUZWA CCM AMBAPO AMEPINGA KWENDA MAHAKAMANI NA KUKAA PEMBENI

04
Aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki Mansour  Yusuf Himid akielezea msimamo wake baada ya kufukuzwa Uanachama CCM ambapo amesema haendi Mahakamani kupinga uamuzi wa Chama, katika ukumbi wa Salama hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar. (Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar)
……………………………………………………………………………………….
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar  
Aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilisihi Jimbo la Kiembe Samaki (CCM) Mansour Yussuf Himid amesema licha ya kufukuzwa Uanachama katika chama hicho hatoenda Mahakamani kutetea nafasi hiyo kwani kufanya hivyo ni kukaribisha Malumbano ambayo hayana tija.
Amesema kwenda kupinga uamuzi huo Mahakamani ni kuhalalisha yeye kuwa Mwakilishi wa Mahakama badala ya Wananchi jambo ambalo hapendelei kutokea katika maisha yake.
Mansour ameyasema hayo leo katika Kongamano la Kamati ya Maridhiano lililofanyika Ukumbi wa Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.
Amesema amekuwa akiulizwa Maswali mengi na Watu tofauti kuhusu mustakabali wake kisiasa baada ya kufukuzwa uanachama na kuongeza kuwa hana Pesa za kuchezea kwenda kupinga uamuzi wa Chama cha Mapinduzi Mahakamani.
“Wenzangu wamenipima na wameniona sifai ni haki yao, siendi Mahakamani, sina pesa za kuchezea wala sitaki kuwa Mwakilishi wa Mahakama” Alisema Mansour
Mansour aliyejiunga CCM mwaka 1987 alienguliwa Uanachama siku za karibuni kutokana na Kamati kuu ya Chama CC kuridhika na madai ya kwenda kinyume na misimamo ya Chama pamoja na kushindwa kuitetea Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mansour ameongeza kuwa kwenda Mahakamani ni kukaribisha malumbano na kusisitiza kuwa Waungwana hawalumbani hivyo ameamua kukaa pembeni.
Amedai kwamba baada ya kufukuzwa uanachama CCM vyama tofauti nchini vimejitokeza kuzungumza naye ili ajiunge navyo na kudokeza kuwa bado hajaamua ni Chama gani ataenda hadi pale muda utakapofika kufanya hivyo
Mansour amesisitiza kuwa hata kama Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC itaitisha uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kiembesamaki yeye hatogombea na kwamba anaweza kufanya hivyo ifikapo mwaka 2015.
Ametumia fursa hiyo pia kuwaomba Radhi wana Jimbo la Kiembe Samaki alilokuwa akiliongoza toka 2005 na kuwashukuru Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliomsaidia katika kupindi chake chote cha Uongozi.
Akigusia suala la Muungano Mansour amesema ataendelea na harakati zake kusimamia maslahi ya Zanzibar  ili kuona mchakato wa Katiba Mpya unakuja na Katiba yenye Muundo wa Muungano wa Haki na Usawa baina ya Tanganyika na Zanzibar.
Awali katika Kongamano hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar Mzee Hassan Nassor Moyo alimshukuru Rais Kikwete kwa ujasiri wa kuleta mchakato wa Katiba Mpya na kusisitiza kuwa Kamati yake itaendelea kudai Muungano wa usawa na haki.
Mzee Moyo amedai kuwa Kamati yake haihitaji kutambuliwa na Watu wengine na kwamba inatosha kujulikana na Wananchi ambao wanafahamu wajibu wa Kamati hiyo.
Itakumbukwa kwamba kabla ya Kongamano hilo Chama cha Mapinduzi kilitoa taarifa kwa Vyombo vya habari kuhusu kutoitambua Kamati hiyo inayoongozwa na Mzee Moyo akisaidiwa na Makamo wake Aboubakar Khamis Bakar.
Katika hatua nyingine Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye alikuwa pia Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi Eddy Riyami alitangaza kujiengua na Chama hicho na kusema kwa sasa yupo huru bila Chama chochote.
Kabla ya Kongamano hilo Kamati hiyo pia iliwasilisha maoni yake kwa Tume ya Katiba mpya ambapo maoni yake yalijikita katika kuifanya Zanzibar kuwa na Mamlaka yake kamili ndani ya Mfumo wa Muungano.

No comments:

Post a Comment