Maafisa 24 wa polisi wauawa Misri
Takriban maafisa 24 wa polisi kutoka Misri wameuawa
kwenye shambulizi la kuvizia katika eneo la Rasi la Sinai. Duru
zinaarifu polisi hao walikuwa kwenye msafara wa mabasi mawili
yaliyoshambuliwa na kundi la watu waliokua na silaha karibu na mji wa
Rafa mpaka na Ukanda na Gaza.
Polisi watatu walijeruhiwa kwenye shambulio
hilo. Katika siku za karibuni jeshi la Misri limeimarisha operesheni
dhidi ya wanamgambo eneo la Sinai hususan baada ya mashambulizi
kuongezeka tangu kuanguka kwa uliokua utawala wa Hosni Mubarak mwaka
2011.
Misri
imekua ikishika doria eneo la Sinai chini ya mkataba wa mwaka 1979 kati
ya Israel na Misri.Mashirika ya habari yanaripoti kwamba wanaume wanne
waliojihami kwa silaha walisimamisha mabasi hayo na kuwaamrisha abiria
wote kuondoka kisha wakaanza kuwapiga risasi.
Baadhi ya duru zinasema washambuliaji hao
walitumia maroketi kulenga mabasi hayo. Utawala wa mpito umetangaza hali
ya hatari kufuatia maandamano ya umma yaliofuatia kuondolewa mamlakani
kwa Muhammed Morsi kama Rais wa nchi hiyo. Amri ya kutotoka nje usiku
imewekwa mji mkuu Cairo.
Zaidi ya watu 800 wakiwemo polisi 70 wameuawa
tangu Jumatano ya wiki jana wakati jeshi lilipovunja kambi za wafuasi wa
vuguvugu la Muslim Brotherhood anakotokea Morsi. Na hapo Jumapili
mahabusu 36 walikufa wakati wakisafirishwa katika jela moja nje ya mji
wa Cairo.Serikali na jeshi wamesema mahabusu hao walikosa hewa kwenye
gari walimokua. Hata hivyo Muslim Brotherhood wametaja kitendo hicho
kama mauaji ya kinyama.
Huku haya yakiarifiwa Muungano wa Ulaya
umeitisha kikao cha dharura kujadili uhusiano wake na Misri. Muungano
huo umetoa taarifa ya pamoja na kusisitiza haja ya kumaliza ghasia mara
moja.Wafuasi wa Morsi wametaja kuondolewa kwake kama mapinduzi, lakini
jeshi na serikali zinasema vuguvugu la Muslim Brotherhood liliendesha
kampeini ya ugaidi tangu kuondolewa kwa kiongozi wake kama Rais.
source : bbc swahili .
No comments:
Post a Comment