MADRASATUL Nnajjary Islamiya ipo nyumbani kwa mlezi wa madrasa hiyo
Mzee Abbasi Hamza Masoud, Mwananyamala kwa Kopa Jijini Dar es Salaam.
Madrasa hii ni maarufu kwa wakazi wa maeneo hayo kutokana na kazi nzuri
inayofanywa na walimu ya kuwafundisha wanafunzi wa Kiislamu dini yao.
Madrasa hii ilianzishwa na mlezi huyo wa madrasa Abbasi Hamza Masoud
mnamo mwaka 1963 ikiwa na wanafunzi wasiopungua 15, wasichana kwa wavulana.
Kwa kipindi hicho Ustaadh Abbas alifanya kazi kubwa sana ambapo wanafunzi
walikuwa wakiongezeka siku hadi siku.
Mpaka hivi sasa wapo wanafunzi 125 wasichana kwa wavulana, masomo yanayotolewa
madrasani hapo ni Fiqh, Tawheed, Sira, Hadithi, Tafsiri ya Qur’an, Hifadhi
ya Qur’an na Qur’an kwa njia ya Tajwidi.
Kwa sasa madrasa hii ipo chini ya usimamizi wa Ustaadh Ahmad Issa, Zuberi
Issa, Khalid Abbas na Zuberi Ramadhani.
Upo utaratibu ambao umewekwa na walimu kwa kila mzazi kulipa Pesa Maalum kwa kila baada ya mwezi ili kuweza kuwasaidia walimu pesa za matumizi
yao binafsi.
Hata hivyo walimu hao wamesema wazazi wa wanafunzi wamekuwa wagumu kutoa
pesa hizo bila ya kujali kwamba nao wanahitaji kuishi na kujikimu katika
mambo mbalimbali.
Madrasa Nnajjary inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa vifaa vya
kufundishia pamoja na vikalio kama vile mikeka, majamvi na hata magunia
na pia hulazimika walimu pamoja na wanafunzi kukaa sehemu ambayo haina
mikeka.
Madrasa hii ina sehemu yake ya kujitegemea na ipo katika mikakati ya
kukifanyia chuo ukarabati wa kutosha kwa sababu hakipo katika hali ya kimadrasa.
Hivyo, wito umetolewa kwa Waislamu wote wajitokeze kwa wingi kutoa sadaka
zao za hali na mali ili kufanikisha mikakati hiyo.
No comments:
Post a Comment