Tuesday, July 30, 2013

SABABU 25 ZINAZOMFANYA MUISLAMU ASHEREHEKEE MAZAZI YA MTUME REHMA ZA M/MUNGU ZIMSHUKIE JUU YAKE NA AMANI

Kwanini Tunasherehekea Mawlid ?

1.Mawlid ni kuonesha kumfurahikia Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam), na kufurahikia mazazi ya Mtume swalallahu aleihi wa salaam kulimnufaisha kafiri, jee sisi waislamu?! na hio ni dalili aloitumia Ibnu hajar katika fathul bary v9 p145 aliposema:
وذكر السهيلي أن العباس بن عبد المطلب رضي الله عنه قال : لما مات أبو لهب رأيته في منامي بعد حول في شر حال فقال ما لقيت بعدكم راحة الا أن العذاب يخفف عني كل يوم اثنين قال وذلك أن النبي صلى الله عليه وسلم ولد يوم الإثنين وكانت ثويبة بشرت أبا لهب بمولده فاعتقها .

Ametaja imam assuhayli kua Abbaas bin Abdilmuttwalib (r.a) amesema: "Alipokufa Abu Lahab nilimuona ndotoni baada ya mwaka yupo katika hali mbaya, akanambia sijapata baada yenu mapumziko, isipokua nakhafifishiwa adhabu kila siku ya Jumatatu, akasema na jilo ni kwasababu Mtume (swalallahu aleihi wa salaam) amezaliwa siku ya Jumatatu na Thuwayba alienda kumpa bishara Abu Lahab kwa kuzaliwa Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) akamwacha huru.
Ikiwa huyu kafiri aliefurahikia mazazi ya Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) mara moja kwa kumwacha huru kijakazi chake, anakhafifishiwa adhabu kila Jumatatu, jee waislamu wanamfurahikia mara kwa mara watapata jaza gani kwa Allaah (Subhannahu wa taala)

2: Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) alikua akiitukuza siku ya kuzaliwa kwake na akiisherehekea kwa kufunga kama ilivyothubutu katika hadithi iliopokewa na Imam Muslim kutoka kwa Abu Qatada kua Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) alipoulizwa kwanini anafunga Jumatatu akasema "Ni siku nilozaliwa na kuteremshiwa wahyi"
عَنْ أَبِى قَتَادَةَ الأَنْصَارِىِّ رضى الله عنه أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ -صلى الله عليه وسلم- سُئِلَ عَنْ صَوْمِ الاِثْنَيْنِ فَقَالَ ( فِيهِ وُلِدْتُ وَفِيهِ أُنْزِلَ عَلَىَّ) .

3: Tumeambiwa na Allaah (Subhannahu wa taala) katika Qur'an tumfurahikie Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam):
. ( قُلْ بِفَضْلِ اللَّهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِمَّا يَجْمَعُونَ )) (يونس:58)
"Sema kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake, basi na wafurahi kwa hayo, haya ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya"

Katika aya hii Mwenyezi Mungu (Subhannahu wa taala) anatuamrisha kuifurahikia rahma, na Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) ndio rahma adhimu. Asema Mwenyezi Mungu (Subhannahu wa taala) katika aya nyengine: ( وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلاَّ رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ )) (الانبياء:107))
"Na hatukukutuma ispokua ni rehema kwa walimwengu"

4: Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) alikua akizingatia mafungamano kati ya zama na matokeo ya kidini yalopita, inapofika wakati ambao lilitokea ndani yake lile tokeo hua ni farsa na kulikumbuka, na kuitukuza siku hio, kwasababu ya hilo tukio. Na huu msingi ameuweka mwenyewe Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) kama ilivokuja kwa Bukhary na Muslim na Tirmidhy na wengineo kua Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) alipofika madina alikuta mayahudi wakifunga siku ya Ashuraa, akaulizia kuhusu hilo, akaambiwa kwamba wanaifunga kwasababu Mwenyezi Mungu amemuokoa Mtume wao na akamzamisha adui wao katika siku hii, kwahivo wao wanaifunga kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hio, Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) akasema: "Sisi ni bora kumkumbuka Musa kuliko nyinyi", akafunga na akaamrisha watu wafunge.

Alhafidh Ibn Hajar ndio mwanachuoni wakwanza kutolea dalili hadithi hii katika kufaa kufanya mawlid, na hakuna muislamu anaeshuku aqida ya Ibn Hajar, na maulamaa wote wamekubaliana kua yeye ndie amiri wa waumini katika hadithi.

5: Mawlid yakupelekea kumswalia Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam), na Mwenyezi Mungu (Subhannahu wa taala) ametuamrisha kumswalia aliposema:
. ( إِنَّ اللَّهَ وَمَلائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيماً )) (الأحزاب:56)
"Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Nabii. Enyi mlio amini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu"

Na chochote kinachokupelekea kufanya yaloamrishwa na sheria basi kitu hicho pia kinakubalika kisheria, kwani kumswalia Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) kunamfaidisha mja mambo mengi:

a) Anakua amefuata amri ya Mwenyezi Mungu (Subhannahu wa taala)
b) Anaswaliwa na Mwenyezi Mungu (Subhannahu wa taala) mara kumi kwa swala moja.
c) Anapandishwa daraja kumi na kuandikiwa thawabu kumi na kufutiwa madhambi kumi.
d) Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) humrudishia salamu.
e) Huondolewa hamu zake na kusamehewa madhambi yake, Na mengine mengi.

6: Mawlid yamekusanya kutaja mazazi yake na sera yake na miujiza yake, na sisi waislamu tumeamrishwa kumjua Mtume swalallahu aleihi wa salaam na kumfuata, tunapohudhuria mawlid tunapata kuyajua yote hayo.

7: Unapomsifu Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) unapata jaza kutoka kwake, kama alivyokua akiwajazi washairi walokua wakimsifu, alimpa Ka'b bin Zuhayr (r.a) kishale na akatengezea Hassaan bin Thabit (r.a) membar. Na alikua akifurahikia kusifiwa, vipi asiurahikie kwa kukusanywa sera yake na sifa zake na miujiza yake!!!
Ametaja Alhafidh ibn Sayyidin naas katika kitabu cha منح المدح zaidi ya maswahaba mia moja na sabiini walomsifu Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) kwa mashairi mazuri mazuri.

8: Maswahaba hawakuwacha kumsifu Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) hata baada ya kufa, tena ndani ya msikiti. Ametaja Imam Shafi katika musnad yake (1706), wakati wa khilafa ya Sayyidna Omar (r.a) aliingia msikitini akampata Hassan bin Thabit akitoa mashairi ya kumsifu Mtume swalallahu aleihi wa salaam, akamwambia: "Hassan watoa mashairi katika msikiti wa Mtume?!!" (Swalallahu aeihi wa salaam) Hassaan akamjibu: "Nimeyatoa mbele ya ambae ni mbora kuliko wewe ewe Omar", akamgeukia Abu Hurayra (r.a) akamwambia: "Hukumsikia Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) akisema: "Ewe Mola mjaalie Jibril amuunge?" Abu Hurayra akasema: "Ndio nimemsikia", akasema: wakamwekea membar Hassaan msikitini ili atoe mashairi ya kumsifu Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam)

Hii ni dalili tosha kuonesha maswahaba walimsifu hata baada ya kufariki, na maneno ya Sayyidna Omar (r.a) hayakua kwa ajili ya mashairi au kumsifu Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam), bali yalikua kwa ajili ya sehemu ambayo ni msikiti, lakini alipojua kua wakati wa Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) alikua akiyatoa msikitini mbele ya Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) akajua inafaa na akamwekea na membar khaswa kwa hilo.

9: Kujua miujiza yake na sera yake na tabia zake Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) kwazidisha imani kwake na kwa aliemtuma, kwani mwanadamu ameumbwa kupenda mazuri ya umbo, tabia, ilimu, amali na mengineyo, na hakuna tabia nzuri na zilokamilka na bora kama za Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) na kuongeza mahaba inatakikana katika sheria, kwahivo na lolote lenye kupelekea hilo pia latakikana.

10: Kumtukuza Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) ni jambo liloamrishwa katika sheria,
. ( : لتؤمنوا بالله ورسوله وتعزروه وتوقروه وتسبحوه بكرة وأصيلا ) (سورة الفتح)
Na kufurahikia siku ya kuzawa kwake kwa kudhihirisha furaha na kukusanyika kuleta dhikri, na kuweka chakula, na kuwakirimu maskini ni katika alama za kumtukuza na kumfurahikia na kumshuru Mwenyezi Mungu (Subhannahu wa taala) kwa kutuongoza kwa dini ya kiislamu na kutuletea zawadi kubwa ambayo ni Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam)

11: Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) alipokua anataja ubora wa siku ya Ijumaa alitaja kua ni siku aloumbwa nabii Adam (a.s) ikiwa Ijumaa imekua bora kwa kuumbwa nabii Adam siku hiyo, je siku alozaliwa mbora wa Mitume na manabii itakosaje kua ni siku bora.

12: Qur'an imetaja mazazi ya baadhi ya mitume, na hii ni dalili tosha kuonesha siku ya mazazi ya Mtume swalallahu aleihi wa salaam ni siku tukufu na ni siku ya kukumbukwa.

13: Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) alipokua anaenda israa alipofika Bayt Lahm aliambiwa na Jibryl ashuke aswali rakaa mbili, alipomuuliza hapa ni wapi, akamwambia hapa ni sehemu alipozaliwa nabii Isa (a.s). Ikiwa sehemu alozaliwa nabii Isa (a.s) imestahiki kukumbukwa, vipi mazazi ya Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) yasikumbukwe?

14: Mwenyezi Mungu (Subhannahu wa taala) katika Qur'an anasema: 
. ( وَكُلاًّ نَقُصُّ عَلَيْكَ مِنْ أَنْبَاءِ الرُّسُلِ مَا نُثَبِّتُ بِهِ فُؤَادَكَ )) (هود: من الآية120)(
"Na yote tunayo kusimulia katika khabari za Mitume ni ya kukupa nguvu moyo wako"

Ikiwa moyo wa Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) wapewa nguvu kwa kusimuliwa khabari za Mitume, je sisi hatustahiki kuzipa nyoyo zetu nguvu na thabati kwa kusimuliana khabari za Mtume  (Swalallahu aeihi wa salaam)?

15: Kuhuisha ukumbusho wa mazazi ya Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) ni kitu kinacho takikana kisheria, kwani hatuoni amali za hajj nyingi ni kuhuisha ukumbusho ulotangulia, kama kupiga mawe jamaraat na sa3y kati ya swafa na marwa na kuchinja katika mina.

16: Amepokea Imam Bayhaqi kutoka kwa Anas (r.a) kua Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam)alijichinjia aqiqa baada ya kutumilizwa. Na imepokewa kua babu yake alimchinjia siku ya saba baada ya kuzaliwa. Imam Suyuti asema: na aqiqa hua ni mara moja tu, itakua maana ya kitendo hicho ni kua alichokifanya Mtume (Swalallahu aeihi wa salaam) ni kudhihirisha shukurani kwa kuletwa na Mwenyezi Mungu kama rahma kwa walimwengu, kwahivo inapendekezwa kudhihirisha shukurani kwa kuzawa kwake na kulisha chakula na mengineo katika sampuli za ibada na furaha.

17: Mwenyezi Mungu (Subhannahu wa taala) katika Qur'an asema:
. ( اللَّهُمَّ رَبَّنَا أَنْزِلْ عَلَيْنَا مَائِدَةً مِنَ السَّمَاءِ تَكُونُ لَنَا عِيداً لِأَوَّلِنَا وَآخِرِنَا وَآيَةً مِنْكَ وَارْزُقْنَا وَأَنْتَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ) المائدة / 114 )
"Ewe Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu! Tuteremshia chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni Ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanao ruzuku"

Ikiwa kuteremshwa meza ya chakula waliifanya ni sikukuu ya kuikumbuka hio neema, je siku ya kuzaliwa neema kubwa (Mtume swalallahu aleihi wa salaam) si inastahiki zaidi kukumbukwa?

18: Mwenyezi Mungu (Subhannahu wa taala) katika Qur'an anaamrisha kukubusha masiku yake yeye:
. ( وَذَكِّرْهُمْ بِأَيَّامِ اللَّهِ ...) (إبراهيم:5)
"Na uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu"

Je, kuzaliwa kiumbe bora na rehema ya walimwengu na Mtume wa mwisho sio siku katika masiku ya Mwenyezi Mungu? Siku ambayo imepelekea kupatikana Mtume alikuja kuziongoza nyoyo na kuwatoa watu katika kiza cha ushirikina na ukafiri.

19: Mawlid ni moja katika njia ya kufanya da'wa, na sote tunakubali kuwa mawlid imesilimisha mamilioni ya watu afrika mashariki, hii ni dalili tosha kuonesha ni jambo la kheri.

20: Amenukuu Sheikh Ibn Taymiya katika Iqtidhwaa swiratwal Mustaqim katika ukurasa wa 304 na 305 kuwa maansari (watu wa Madinah) kabla ya kuja Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) Madina walisema: Tuangalieni siku tukusanyike tukumbuke hii neema alotuneemesha Mwenyezi Mungu wakasema: "Siku ya Jumamosi", kisha wakasema: 'hatutangamani na mayahudi katika siku yao', wakasema "Jumapili", wakasema: 'hatutangamani na manaswara katika siku yao', wakasema "Ijumaa", wakajumuika katika nyumba ya Abu Umamah Saad bin Zurarah, wakachinjiwa mbuzi akawatosha wote.

21: Mawlid imefanywa kwa muda ma maqarne bila ya kupingwa na wanazuoni, na wametaja sherehe ya mawlid wana tarekhe katika vitabu vyao, kama Ibnu Kathyr na Ibnul Jawzy na Ibnu Dihya al'Andalusy, na Ibnu Hajar na Assuyutwy na wengineo na wote hao ni vigogo katika elimu za Hadith, Fiqhi, Aqidah na hawakuogopea kwa kuwatisha waisilamu na neno la Shirk au Bidaa na mengineyo tuyasikiyao zama hizi zenye kutokuwa na Maulamaa sampuli za maulamaa hao tuliowataja.
Ha hadithi ya Ibn Mas'ud yasema:
. "مَا رَآهُ المُسلِمونَ حَسَناً فَهوَ عِندَ اللهِ حسنٌ، وَمَا رَآهُ المُسلمونَ قَبيحاً فَهوَ عندَ اللهِ قَبيحٌ"
"Wanaloliona waislamu ni jema basi na mwa Mwenyezi Mungu pia ni jema, na wanachokiona waislamu ni kiovu basi na kwa mwenyezi Mungu pia ni kiovu"

22: Mwenyezi Mungu (Subhannahu wa taala) asema:
{وَمَنْ يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّهِ فَإِنَّهَا مِنْ تَقْوَى الْقُلُوبِ} [الحج:32]
"Na mwenye kutukuza sha'air za Mwenyezi Mungu, basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo"

Ikiwa kuadhimisha na kutukuza tambiko la Mwenyezi Mungu (Subhannahu wa taala) ni katika unyenyekevu wa nyoyo, basi na Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) ni tambiko la Mwenyezi Mungu (Subhannahu wa taala), na kutukuza mazazi yake ni kumtukuza yeye.

23: Kuhudhuria mawlid kunakuza mahaba ya mu'min kwa Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam), na Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) anasema katika hadithi iliopokewa na Imam Bukhary:
. "لاَ يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى أَكونَ أحبَّ إليه مِن والده وَوَلدِه وَالنَّاسِ أَجمعين"
"Haikamiliki imani ya mmoja wenu mpaka anipende mimi zaidi ya mzazi wake na watoto wake na watu wote"

24: Maulamaa wakubwa walofika daraja ya kua mahuffaadh wametunga vitabu kuhusu mawlid:

A: Alhaafidh Ibnu Kathyr anayetegemewa na wenye kujiita Salafiyah. Ametaja hilo Ibn Hajar katika Addurarul Kaaminah.

B: Alhafidh al'Iraqy, ametunga : المورد الهني في المولد السني .

C: Alhaafidh Ibn Naaswiruddyn Addimashqy, huyu ana vitabu vitatu:
i) جامع الآثار في مولد النبي المختار
ii) اللفظ الرائق في مولد خير الخلائق
iii) مورد الصادي في مولد الهادي .

D: Alhaafidh Assakhaawy, ametunga: الفخر العلوي في المولد النبوي .

E: Alhaafidh Mullaa Ali Alqaary, ametunga: المورد الروي في المولد النبوي .

F: Alhaafidh Ash'shaybany Azzabidy, anaejulikana kwa Ibnud dayba’a, ametunga maulidi yake mashuhuri mawlid addayba’a.

G: Alhaafidh Assuyutwi, ametunga حسن المقصد في عمل المولد .

H: Alhaafidh ibnu Dihya, ametunga: التنوير في مولد البشير النذير .

J: Alhaafidh Ibnul jazary, ametunga: عرف التعريف بالمولد الشريف .
Mbali na hufaadh kuna muhadditheen walotunga mawlid na fuqahaa na mufassireen na wengineo wengi, hatutowataja wote kwa kutorefusha nukta hii.

25: Sababu wanazotoa wanaokataza kusherehekea mawlid:

Sababu ya 1: Wanasema lingekua ni kheri basi Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) angelifanya.

Tunawauliza; je, kutia nukta na shakli katika msahafu ni kheri ama si kheri? na Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) hakulifanya, je, tuzitoe kwa kuwa (Swalallahu aleihi wa salaam) hakulifanya?

Sababu ya 2: Wanasema Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) hakufanya mawlid.

Tunasema; Sio kila ambalo hakuliamrisha Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) wala hakulikataza halifai, mashindano ya Qur'an Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) hakufanya, tahajjud kwa jamaa msikitini Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) hakuifanya, kukhitimisha msahafu katika tarawehe Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) hakulifanya hilo, na wengi wanaopinga mawlid wanayafanya yote hayo na hayakufanywa na Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) Nani kawapa rukhsa ya kuyafanya hayo na kutukataza sisi tusifanye kwa kuwa tu wao hawafanyi na hawapendi?

Sababu ya 3: Wanasema Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) amesema mwenye kuzusha katika dini kisokua katika dini basi haikubaliwi!

Tunawaambia; hamkuifahamu hadithi kama walovyoifahamu maulamaa wakubwa wa karne na karne tena Mahufaadh. Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) amesema kisochokua katika dini, ama kilichoko katika dini basi kinakubaliwa, na yote yanayopatikana katika mawlid kama kusoma Qur'an na kumswalia Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) na kulisha chakula yote yapo katika dini.

Sababu ya 4: Wanatumia lugha ya kutisha na wanasema kufanya mawlid ni kumtuhumu Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) kuwa amefanya khiyana na haitufikishia kila jambo katika dini!

Tunawaambia; Na hayo mambo tulowatajia hapo juu ambayo hata wao wanayafanya na hayakutajwa na Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) sio kumtuhumu kwa khiyana? Kisha maulamaa waloweka mambo haya tayari mushawatuhumu.

Sababu ya 5: Wanasema katika baadhi ya mawlidi kunapatikana munkarati, kwahivo ni haramu.

Kwanza twawauliza; Je, Mawlid isiyokua na munkaraati mwaikubali? pili kama kuweko munkaraati kwa baadhi ya mambo itapelekea kuharamisha yote basi itabidi tuharamishe harusi pia, maana kuna zengine hujaa munkarati.

Sababu ya 6: Wanasema mawlidi haifai kwasababu kwasifiwa Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam), na Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) amekataza aliposema:
. "لا تُطْروني كما أطْرَتِ النَّصارى الْمَسيحَ ابنَ مَرْيَمَ"

Tunawaambia; Neno ‘’itraa’’ katika lugha maana yake ni kuvuka mpaka katika kusifu, na kuvuka mpaka kwenyewe tayari Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) amekupigia mfano katika hadithi hiyohiyo aliposema kama walivyo vuka mpaka manaswara kwa Isa. Ni mpaka upi huo waliovuka manaswara? Walifika kumuita Mungu na Mtoto wa Mungu. Je, kuna muislamu ambae anaitakidi Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) ni Mungu ama ni mtoto wa Mungu? Kwahivo namna tutakavyo msifu madamu hatujafika katika huo mpaka basi hakuna uharamu wala makosa. Na qaaida ya ki-usuli yasema, linapokatazwa jambo maana yake ni kulifanya jambo hilo kinyume cha makatazo yake, kwahivyo Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) katika hadithi hii hajatukataza kumsifu sana, bali ametuamrisha kumsifu sana, madamu hatutavuka mipaka.

Sababu ya 7: Wanasema kufanya mawlid ni kuyafunga mahaba ya Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) katika siku moja tu!

Tunawauliza; Pale Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) aliposema sisi ni awla kumsherehekea Musa kuliko wao, kisha akafunga na akaamrisha watu wafunge je, aliyafunga mahaba ya nabii Musa katika siku moja?

Sababu ya 8: Wanasema maswahaba walikua ni wabora na wanampenda Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) kuliko sisi na hawakunya mawlid

Tunawaambia; je, alotia nukta katika msahafu wakati wa Hajjaaj bin Yusuf alikua aipenda Qur'an kuliko maswahaba? je, Sayyidna Omar (r.a) alipowakusanya watu msikitini kuswali tarawehe alikua ni mbora kuliko Sayyiduna Abu Bakr ambae hakulifanya hilo? je, Sayyiduna Uthmaan (r.a)alipoweka adhana yapili alikua ni mbora kuliko sayyidna Abu Bakr na Sayyidna Omar? wanazuoni wamesema: الْمَزِيَّةُ لا تَقْتَضي التَّفْضيلَ .

Sababu ya 9: Wanasema mawlid imekua ni hoja ya wanaoenda kufanya uchafu wao!

Tunawaambia; Tatizo lipo katika niya ya huyo mtu, wala sio kwa mawlid, na kama anavotumia mawlid kama hoja na pia atatumia mengine pia kama kuenda tarawehe. Kuna watu wanaenda hajj kwa ajili ya kuiba, na wengine huenda kutongoza na wengine huenda kufanya makubwa kushinda hayo, jee tuondoe ibada ya hajj? Usiseme huswali kwa kua nguo ina najasa, safisha najasa uswali.

Sababu ya 10: Wanasema mawlid ni katika mambo yenye shaka, na Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam) ametuambia tuwache yenye shaka.

Tunawaambia; Shaka ipo katika wahm zao, ama kwetu hamna shaka hata kidogo kuwa mawlid yafaa na hayapingani na mafundisho ya dini tukufu ya Kiisilamu wala Mafundisho ya Mtume (Swalallahu aleihi wa salaam)

Mwisho tunatoa nasiha kwa wanaotumia juhudi kubwa kupinga mawlid:

Lau mngelitumia juhudi hizo katika kukataza mambo ya haramu ambayo hayana shaka tungekua hatuna uchafu tunaouona katika jamii, kuenea madawa ya kulevya na zinaa na vijana kupuuza swala na mengineo.

Wabillahi Tawfiq.

Imetayarishwa na Vijana wa Kitwariqa Afrika Mashariki  , Followers of Tariqah Alawiyah East Africa.

kwa makala zaidi tembeea : www.twariqah.blogspot.co.uk

No comments:

Post a Comment