Aliyekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak anatarajiwa kutolewa gerezani leo
baada ya mahakama kuamuru achiliwe huru, lakini mara tu baada ya
kuachiwa atawekwa chini ya kifungo cha nyumbani.
Haijabainika wazi ni saa ngapi Mubarak atatoka gereza la Tora lililoko
mjini Cairo au ni wapi atakakopelekwa huku vyanzo vikidokeza huenda
aidha akapelekwa katika mojawapo ya hospitali mbili za kijeshi ambako
amekuwa akipatiwa matibabu katika siku za nyuma au nyumbani kwake.
Mahakama ya rufaa hapo jana iliagiza kuachiliwa kwa kiongozi huyo
aliyeoingoza Misri kwa miaka 30 kabla ya kung'olewa madarakani mwaka
2011 baada ya vuguvugu la umma la kutaka mageuzi ya uongozi na
demokrasia.
Waziri mkuu ndiye wakuamua hatma ya Mubarak
Punde tu baada ya agizo hilo la mahakama, serikali ya muda ya Misri jana
ilitangaza kuwa Mubarak atawekwa chini ya kifungo cha nyumbani iwapo
ataachiliwa. Waziri mkuu wa muda Hazem el Beblawi ameagiza kuzuiwa kwa
Mubarak.
Waziri mkuu wa muda wa Misri Hazem el-Beblawi |
Taarifa kutoka serikalini imesema kuambatana na kanuni za sheria ya hali
ya hatari iliyoko nchini humo hivi sasa, naibu mkuu wa jeshi ambaye ni
el Beblawi ameagiza Mubarak kuzuiliwa.
Mubarak bado anakabiliwa na mashitaka ya ufisadi na kushindwa kuchukua
hatua muafaka za kuzuia vifo vya waandamanaji 850 waliomng'oa
madarakani.
Kikao kingine cha mahakama kusikiza kesi hizo zinazomkabili ni Jumapili
hii. Shirika la habari la serikali MENA limesema jalada la Mubarak
litapelekwa kwa mwendesha mashitaka mkuu leo asubuhi ili kuthibitisha
kuwa hakuna msingi wowote wa kuendelea kuzuiliwa kwake.
Iwapo hilo litakubalika, basi atasafirishwa kwa helikopta ya kijeshi
kuanza kutumikia kifungo cha nyumbani. MENA limeripoti kuwa waziri mkuu
el Beblawi ndiye aliye na maamuzi ya mwisho ya ni wapi atakakozuiliwa
Mubarak.
Kuachiliwa kwa Mubarak kutaligawanya taifa zaidi
Hatua hiyo ya serikali ya kumuweka Mubarak chini ya kifungo cha nyumbani
inaonekana ni ya kuwatuliza Wamisri ambao huenda wakaghadhabishwa na
kuachiliwa kwake na kuhisi utawala wa zamani unarejea pole pole
madarakani huku taifa hilo likiwa limegawanyika vibaya tangu jeshi
kumpindua Mohammed Mursi mwezi uliopita.
Wafuasi wa Rais aliyeng'olewa madarakani Mohammed Mursi |
Zaidi ya watu 900 wameuawa katika makabiliano kati ya maafisa wa usalama
na wafuasi wa Mursi na polisi imewakamata wanachama kadhaa wa udugu wa
kiislamu akiwemo kiongozi wao mkuu Mohammed Badie huku Mursi akiwa bado
anazuiliwa katika eneo lisilojulikana.
Umoja wa Ulaya hapo jana ulitangaza kusitisha biashara ya silaha na
Misri ili kushinikiza Misri kurejea katika mchakato wa kisiasa wa
kurejesha demokrasia lakini wataendelea kutoa misaada ya kuboresha
uchumi wa nchi hiyo.
Marekani pia ilisitisha zoezi la pamoja la mafunzo ya kijeshi na kusema
inatafakari upya uhusiano wao na Misri. Hata hivyo nchi kadhaa za
Kiarabu zimeahidi kuiunga mkono serikali ya muda ya Misri.
CHANZO.DWSWAHILI.
No comments:
Post a Comment