Wednesday, August 07, 2013

KWAHERI RAMADHANI
Ramadhani waondoka, karibu chetu kipenzi
Nyoyo zimefadhaika, watauchia simanzi.

Machozi yabubujika, kwa huzuni na majonzi
Karibu kipenzi chetu, kwaheri ya kuonana.

Twakuomba ya Rabuka, Mola Mmiliki enzi
Tulipe yalotukuka, kuufunga huu mwezi.

Tujazie na baraka, Utuwachie na pumzi
Mwaka kesho ukifika, tufunge bila ajizi.
==================================================================== 
ANATUAGA MGENI
1:Sifa zote zilo njema,nizake Mola manani,
Mola mwingi wa neema,mwenye nguvu mwenye shani,
Mola aliye karima,Mola mwingi wa ihsani,
ANATUAGA MGENI,YA RABBI TUPE SUBIRA.

2:Hatuna budi kusema,twakushukuru Manani,
metupa afya nzima,ya kufunga ramadhani,
kikomo leo twa koma,kutimiza ramadhani,
ANATUAGA MGENI,YA RABBI TUPE SUBIRA.
3: Twauaga mwezi mwema,anaondoka mgeni,
tuloufaidi umma,pembe zote duniani,
twauaga kwa huruma,twasononeka nyoyoni,
ANATUAGA MGENI,YA RABBI TUPE SUBIRA.

4:Twasononeka nyoyoni,furaha hatuna tena,
tunalia waumini,kwa matozi mengi sana,
imetufika huzuni,waumini twalizana,
ANATUAGA MGENI,YA RABBI TUPE SUBIRA.

5: Anaondoka mgeni,mgeni mwenyemaana,
katu hatuna imani,ya mwakani kumuona,
na hatudhani mwakani,sisi naye kukutana,
ANATUAGA MGENI,YA RABBI TUPE SUBIRA.

6:Ametujenga moyoni,kwa maovu kupambana,
tulidumu ibadani,imani kuzidishana,
kujaa misikitini,kwa mema kukumbushana,
ANATUAGA MGENI,YA RABBI TUPE SUBIRA.

7:Sana tuliongozana,furaha ikatungiya,
na sote tulilingana,kwa njaa kuisikiya,
umoja tuliuona,tajiri fukara piya,
ANATUAGA MGENI,YA RABBI TUPE SUBIRA.

8:Tulitenda ya maana,kumridhisha jaliya,
kusoma qurani sana,asubuhi na ashiya,
napia tukaungana,tarawehe kutimiya,
ANATUAGA MGENI,YA RABBI TUPE SUBIRA.

9:Natukafuturishana,magharibi kuingiya,
wale ambao hawana,chakujishikiliziya,
walishukuru Rabana,kwa dua kutuombeya,
ANATUAGA MGENI,YA RABBI TUPE SUBIRA.

10:Waumini tunaliya,matozi yatudondoka,
adui anarejeya,sana anafurahika,
kufunga tumezoweya,ramadhani yaondoka,
ANATUAGA MGENI,YA RABBI TUPE SUBIRA.

11:Ya Allahu ya jaliya,kwako tunakueleka,
mikono twakwenushiya,mbele zako twageuka,
dua zetu zipokeya,nasi uweze ridhika,
ANATUAGA MGENI,YA RABBI TUPE SUBIRA.

12:Funga itakabaliya,ndani isiwe na shaka,
moto utuepushiya,pepo yako twaitaka,
ya Rabbi tujaaliya,ya mwakani kuifika,
ANATUAGA MGENI,YA RABBI TUPE SUBIRA.

***ANATUAGA MGENI***
Na: Damash Malenga Bubu.

1 comment: