AINA ZA NYOYO:
Aina za nyoyo ni tatu:
1 Moyo uliosalimika:
Moyo uliosalimika ni ule moyo ulioepukana na shirki, unafiki, riyaa, chuki, hasad, dhanna n.k. Na ndio moyo ambao utamfaa mja mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) siku ambayo haitamsaidia mali yake wala watoto wake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
{{يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ * إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ}} الشعراء: 88-89
{{Siku ambayo hayatafaa mali wala watoto * isipokuwa atakayekuja kwa Allaah na moyo msafi}} Ash-Shu'araa6:88-89
2 Moyo wenye maradhi:
Moyo wenye maradhi ni ule moyo ambao haujaonja ladha ya imani, umezungukwa na maradhi ya hatari ambayo tiba yake haipatikani popote isipokuwa kwenye Qur-aan. Maradhi ya nyoyo ni maradhi hatari kuliko hata saratani, na yanapomsibu mja basi huwa hakuna dawa mpaka arejee kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Na wagonjwa wengi wa moyo huwa katika kundi baya kabisa la wanafiki. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
{{فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ فَزَادَهُمُ اللّهُ مَرَضاً}} البقرة: 10
{{Nyoyoni mwao mna maradhi na Allaah Amewazishia maradhi}} Al-Baqarah 2:10
Maradhi ya nyoyo ni maradhi ambayo yanapelekea katika unafiki, moja miongoni mwa sifa mbaya kabisa ambayo haitakikani kwa Muislamu kusifika nayo,kwani mnafiki ana daraja mbaya kabisa zaidi hata ya kafiri, na ni kiumbe muovu zaidi kuliko viumbe wote.
3 MOYO ULIOKUFA:
Moyo unapozidiwa na maradhi hufikia daraja ya kifo, na kifo cha moyo sio kupoteza uhai bali ni kususuwaa na kuwa mgumu, kuwa ni moyo usioathirika, usiowaidhika, na usioogopa. Moyo wa aina hii ndio ule uliosifiwa na Allaah katika Qur-aan pale Aliposema:
ثم قست قلوبكم من بعد ذلك فهي كالحجارة أو أشد قسوة..) البقرة 74 )
(Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo; hata zikawa kama mawe au ngumu zaidi..) 2:74
Moyo uliokufa umeelezwa kwa majina tofauti katika Qur-aan, majina yote yakiwa yanaashiria kususuwaa na kufungika kwa nyoyo kutokana na kuishi katika maradhi kwa muda mrefu bila kupata tiba, mfano tu wa aya zinazoashiria hali hiyo ya nyoyo ni kama zifuatazo:
1. Kufungika kwa nyoyo na kutoruhusu mawaidha au nasaha kupenya, Anasema Allaah:
(Je hawazingatii hii Qur-aan? Au katika nyoyo zao kuna kufuli?) 47:24
2. Nyoyo kupatwa na kutu na kutoathirika kirahisi kwa kutofikiwa na mionzi ya imani, Anasema Allaah:
(كلا بل ران على قلوببهم ما كانوا يكسبون)
(Sivyo hivyo, Bali yametia kutu ndani ya nyoyo zao maovu waliyokuwa wakiyachuma) 83:14
3. Nyoyo zenye vifuniko au vizibo,nyoyo ambazo hazina tundu wala njia ya kupenyeza mawaidha, Anasema Allaah:
(Na walisema nyoyo zetu zimefunikwa (hatufahamu unayoyasema) 2:88
4. Ujinga wa nyoyo na kutokuwa na mazingatio, Anasema Allaah:
(لهم قلوب لا يفقهون بها)
(Nyoyo wanazo, lakini hawataki kufahamu kwazo) 7:179
5. Upofu wa nyoyo, kutotaka kuona haki na ukweli, Anasema Allaah:
(فإنها لا تعمى الأبصار ولكن تعمى القلوب التي في الصدور) الحج 46
(Kwa hakika macho hayapofoki, lakini nyoyo ambazo zimo vifuani ndizo zinazopofoka) 22:46
Baada ya kuangalia aina tatu za nyoyo, ni vema tukaangalia kwa undani zaidi baadhi ya maradhi ya nyoyo ambayo kama hayatashugukiliwa mapema, husababisha kifo cha nyoyo ambayo ndio daraja mbaya zaidi kwa mwanadamu, kwani mtu ambae moyo wake umekufa, si rahisi kurudi kwa Allaah kwa kufanya Toba. Aidha matendo yake mara nyingine humfanya aonekane kama mnyama au zaidi hata ya mnyama.
Na : Mussa Al-shiraziy·
Stone Town, Zanzibar Urban, Tanzania
No comments:
Post a Comment