Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Serikali ya Oman
ukiongozwa na Waziri wa Habari wa Nchi Hiyo Dr. Abdulmumin Mansour Bin
Said Al- Hasani hapo Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Waziri wa Habari wa Nchi Hiyo Dr.
Abdulmumin Mansour Bin Said Al- Hasani akiagana na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya ujumbe wake
kuzungumza nae hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Ujumbe wa Serikali ya Oman ambao
pia upo Zanzibar kushiriki Kongamano la Kimataifa la Ustaarabu wa
Kiislamu.
Kulia
ya Balozi Seif ni Waziri wa Habari wa Nchi Hiyo Dr. Abdulmumin Mansour
Bin Said Al- Hasani na kushoto yake ni Waziri wa Habari, Utamaduni,
Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Uhusiano wa
kubadilishana nyaraka za Kihistoria kati ya Oman na Zanzibar unaweza
kuwasaidia wananchi wa pande mbili pamoja na watafiti wa masuala ya
Kihistoria kuelewa kwa kina maingiliano ya muda mrefu yaliyopo kati ya
Wazanzibar na Waoman ambayo yanafanana Kisilka na Kiutamaduni.
Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa
mazungumzo yake na Ujumbe wa Viongozi sita wa Serikali ya Oman
ulioongozwa na Waziri wa Habari wa Nchi hiyo Dr. Abdulmumin Mansour Bin
Said Al- Hasani aliokutana nao hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif
alisema Zanzibar na Oman zimekuwa na uhusiano wa Kihistoria wa muda
mrefu tokea karne ya 18 ambao umethibitishwa na wataalamu pamoja na
watafiti wa mambo ya Kihistoria kutoka vyuo vikuu tofauti Duniani.
Alielezea haja
kwa Viongozi na Wananchi wa Oman na Zanzibar kuendelea kushikamana na
kushirikiana katika masuala mbali mbali ya maendeleo yatakayosaidia
ustawi wa vizazi vya sehemu zote mbili rafiki.
Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Serikali ya Oman kupitia ushirikiano
wa mamlaka ya kumbu kumbu na nyaraka ya Oman na Chuo Kikuu cha Taifa
cha Zanzibar { SUZA } kwa kuandaa Kongamano la Kimataifa la Ustaarabu wa
Kiiislamu kwa Nchi za Mashariki mwa Bara la Afrika.
Balozi Seif
alisema uamuzi huo wa kufanywa kwa kongamano hilo hapa Zanzibar
umekuja wakati muwafaka kwa wataalamu wa mambo ya Kale kubainisha
kwamba Historia ya Uislamu imeanzia hapa Zanzibar.
“ Nimefurahi
kusikia kwamba Historia ya Uislamu imeanza Zanzibar. Inaonyesha watafiti
wameliona hili kutokana na asilimia kubwa ya wakaazi wa Visiwa vya
zanzibar kuwa waumini wa Dini ya Kiislamu sambamba na Utamaduni wake
“. Alieleza Balozi Seif.
Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar alishauri tafiti za Wataalamu wa masuala ya
Historia ambazo zitaibuka katika Kongamano hilo zielekezwe zaidi
kunufaisha wananchi na waislamu wa ukanda wote wa Afrika Mashariki.
“ Tafiti hizi
za Wataalamu wetu wa Kihistoria itapendeza kama zitaendelea kubakishwa
katika maktaba zetu ili zisaidie wananchi, waislamu na hata wasomi wetu
wa vyuo vikuu vya ukanda wetu wa Afrika Mashariki “. Alisisitiza Balozi
Seif Ali Iddi.
Naye Kiongozi
wa Ujumbe huo wa Serikali ya Oman Waziri wa Habari wa Nchi hiyo Dr.
Abdulmumin Mansour Bin Said Al- Hasani alisema ipo haja ya kuendelea
kuhifadhiwa kwa Historia iliyopo ya Zanzibar na Oman kwa faida ya vizazi
vijavyo.
Dr. Abdulmumin
alieleza kwamba upeo wa tabia za watu wa oman na Zanzibar unaolingana
ndio unaochangia na kushawishi wageni na watalii wa mataifa mbali mbali
duniani kupendelea kuzitembelea nchi hizi zinazofanana kiutamaduni.
Waziri huyo wa
Habari wa Oman alifahamisha kwamba Kongamano hilo la ustarabu wa
Kiislamu linalofanyika hapa Zanzibar mbali ya utafiti uliopatikana
lakini pia litafungua uhusiano katika Nyanja nyengine za maendeleo kwa
nchi shiriki.
Dr. Abdulmumin
alielezea faraja yake kutokana na umuhimu wa udugu uliopo kati ya watu
wa Oman na Zanzibar ambao umepelekea waoman wengi kujitokeza kushiriki
kwenye kongamano hilo.
Alifahamisha kwamba ipo ishara ya kuendelea kwa ziara za mara kwa mara kati ya watu wa pande hizo mbili.
Kongamano hilo
la siku tatu linalofanyika katika Hoteli ya Kimataifa ya La Gemma Della
East Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja na kushirikisha Mataifa yapatayo
17 lina lengo la kuitangaza Zanzibar katika Nyanja za utafiti na Taaluma
Kimataifa.
Hilo ni
kongamano la Pili la Kimataifa la Ustarabu wa Kiislamu kufanyika
likitanguliuwa na lile la mwaka 2012 lililofanyika Nchini Uganda na
kutolewa uamuzi wa kongomano linalofuata kufanyika hapa Zanzibar
kutokana na Historia yake iliyopo sambamba na uhusiano wa karibu
iliyonayo na Mataifa ya Kiarabu.
No comments:
Post a Comment