Monday, September 02, 2013

JWTZ: HIVI NDIVYO ASKARI MWENZETU ALIVYOULIWA NA BOMU NA WAASI WA M23 HUKU TUKISHUHUDIA. HASIRA ZA JWZT SASA ZAWATIA HOFU WAASI HAO!


JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limeleezea namna mwanajeshi wake, Meja Khatibu Shaaban Mshindo, alivyouawa baada ya kuangukiwa na bomu, wakati akiwa katika jukumu la ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

  Pamoja na hayo, Watanzania wametakiwa kuimarisha mshikamano na kuachana na makundi yenye nia ya kuleta mgawanyiko, hasa katika kipindi hiki kigumu ambacho Tanzania imepoteza askari wake waliopewa dhamana ya kitaifa ya ulinzi wa amani katika nchi zenye migogoro Afrika.

  Akitoa salamu za rambirambi wakati askari huyo wa kikosi cha Mizinga namba 83 KJ kilichopo Kibaha akiagwa rasmi kijeshi Dar es Salaam jana, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamnyange, alisema askari huyo pamoja na askari watano wa Tanzania, waliangukiwa na bomu hilo na kujeruhiwa vibaya.

  “Waliangukiwa na bomu Agosti 28, mwaka huu huko Goma DRC eneo walilokuwa wakifanyia kazi… Meja Mshindo aliumia vibaya na kukutwa na mauti njiani akipelekwa hospitalini,” alisema Jenerali Mwamunyange.

  Alisema katika tukio hilo, askari wengine watano wa Tanzania walijeruhiwa vibaya na wanaendelea vizuri na matibabu nchini humo na hali zao zinaendelea vizuri.

  Akimzungumzia Meja Mshindo, Jenerali Mwamunyange alisema katika uhai wake alikuwa mchapakazi, muaminifu, hodari na mtiifu na kifo chake kimetokea wakati jeshi linamhitaji.

  “Kifo chake kimeacha pengo ndani ya JWTZ na itachukua muda mrefu kuziba pengo hili.” Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema kifo cha askari huyo ni msiba wa kitaifa na kumtaja Meja Mshindo kuwa shujaa aliyekutwa na mauti wakati akitekeleza kazi aliyotumwa na nchi yake.

  Alisema kifo hicho pamoja na vifo vya askari wengine saba wa JWTZ vilivyotokea Darfur mwaka huu, ni chachu kwa Tanzania kuendeleza jitihada za kusaidia nchi zenye migogoro na kuhamasisha amani Afrika.

  “Serikali inapata matumaini namna Watanzania walivyosimama pamoja na kuunga mkono jeshi letu katika kipindi hiki kigumu. Ingekuwa nchi nyingine, haya yaliyotokea yangeleta mgawanyiko mkubwa miongoni mwa raia, lakini kwa hapa kwetu hali imekuwa tofauti,” alisema Membe.

  Aliwataka wachache wenye mawazo ya kutumia matukio hayo kuwagawa Watanzania, waache mara moja nia yao hiyo, kwa kuwa moja ya kazi ambayo Tanzania inayo, ni pamoja na nia yake ya kuhamasisha na kutangaza amani Afrika na dunia kwa ujumla.

  “Jamani wajibu wetu ni kuhakikisha haya maeneo yenye migogoro yanakuwa na amani, kule DRC hali ni mbaya, watu wanakufa kila kukicha na akinamama na watoto wanabakwa na kudhalilishwa, sasa sisi kama taifa ni vyema kujitokeza na kusaidia wenzetu,” alisisitiza.

  Meja mshindo, alizikwa jana nyumbani kwao Fujoni Zanzibar na ameacha mke mmoja, Hawa Mnimbo na watoto watatu ambao ni Shaaban, Abuu na Samir Mshindo.
------------------------------------------------------------------

Balozi Seif Ajumuika na Wananchi katika Mazishi ya Meja Khatib Mshindo Fujoni.

Wapiganaji wa Jeshi la Wananachi wa Tanzania { JWTZ } wakitoa salamu zao za mwisho wakati wa mazishi ya kamanda wao Meja Khatibu Shaaban Mshindo yaliyofanyika kijijini kwake Mangapwani.

Meja Khatib Shaaban ambae alikuwa Mkuu wa Kambi ya Kibaha alifariki dunia Mjini Goma Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo akiwa katika ulizi wa amani katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa.
Mamia ya wananachi, ndugu na Jamaa walioshiriki kuusitiri mwili ma marehemu Meja Khatibu Shaaban katika mahali pake Huko Mwangapwani Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiongoza mamia ya wanajeshi, wananchi na Ndugu  na jamaa katika Mazishi ya Meja wa Kikosi cha JWTZ  Kibaha Khatib Shaaban aliyeuawa Nchini DRC akiwa katika shughuli za ulinzi wa vikosivya Umoja wa Mtaifa.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mohammed Aboud Mohammed akitia udongo kwenye kaburi wakati wa mazinshi ya Meja Khatibu Shaaban Mshindo yaliyofanyika kijijini kwake Mangapwani.
Mwakilishi wa Vikosi vya Umoja wa Mataifa vilivyopo Mjini Goma Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Meja E.B. Samuel akitia udongo kuashiria ushiriki wa Umoja wa Mataifa katika mazishi ya  Marehemu Meja Khatibu Shaaban Mshindo yaliyofanyika kijijini kwake Mangapwani.

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimfariji Kiongozi wa Familia ya Marehemu Meja Khatibu Shaaban Mshindo bwana Alhaji Machano Mtumweni mara baada ya kukamilika kwa mazishi ya Kamanda huyo yaliyofanyika kijiji kwake Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment