Dk Shein atoa wito kwa Wahitimu wa afya kubakia nyumbani kuitumikia jamii
Na Salum Vuai, Maelezo
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema wahitimu wa fani
mbalimbali za afya wanaosomeshwa na serikali hawana budi kubaki nchini
na kuitumikia jamii yao.
Dk. Shein ametoa wito huo jana baada ya
kuzindua majego mapya ya dahaklia ya wnafubzi wa kike na jengo la
madarasa, katika Chuo cha Taaluma ya Sayansi za Afya, Mbweni nje kidogo
ya mji wa Zanzibar.
Akizungumza na wanafunzi na wananchi
mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo, Dk. Shein alisema, serikali
inatumia gharama kubwa kuwasomesha wanafunzi wake, hivyo nao wanapaswa
kutimiza ihsani na utu kwa kufanya kazi nchini badala ya kukimbilia nje.
Amesema kwa bahati mbaya, wapo baadhi ya
wananchi na watumishi wa umma wakiwemo wafanyakazi wa sekta ya afya
ambao husomeshwa kwa fedha nyingi za serikali lakini baada ya kumaliza
masomo yao huondoka nchini na kukwepa wajibu wao wa kuwatumikia wananchi
wanyonge waliogharamia fedha hizo.
"Hili siyo jambo zuri kwani siku zote ni vyema binadamu azingatie ihsani anayofanyiwa na wenzake", alisisitiza.
Akitoa mfano kwa kunukuu hadithi ya
Mtume Muhammad (S.A.W), Rais Shein aliwanasihi vijana wote wanaopata
fursa ya kusomeshwa na serikali, kuwa na uzalendo na mapenzi kwa jamii
yao inayowategemea kuihudumia.
Alisema kwa hadithi hiyo, alisema Mtume
Muhammad (S.A.W) anautanabahisha umma juu ya ubaya wa kuwaacha watu
wanaoutegemea kwa kusema:
"Yatosha kwa mtu kupata dhambi kwa kumtupa yule anayemtegemea"
Hata hivyo, alisema kama mtu anataka
kuondoka kwenda kutafuta kazi nje ya nchi, serikali haimzuii, lakini
kwanza ni lazima alipe fedha zote zilizotumika kumsomesha, kwa mujibu
wa agizo la serikali kwa wizara zake zote.
Alifahamisha kuwa, iwapo mtu atashindwa kulipa gharama hizo, wazee au familia yake italazimika kufanya hivyo.
Akizungumzia kukamilika kwa ujenzi wa
majengo hayo pamoja na kupatikana vifaa vya kisasa, alisema hiyo ni njia
moja ya kuimarisha mazingira ya utoaji mafunzo kwa vijana wanaojiunga
na chuo hicho kwa masomo mbalimbali yanayotolewa hapo.
Pamoja na kuwapongeza vijana
waliobahatika kujiunga na chuo hicho katika huduma tafauti za afya, Dk.
Shein alisema ni imani yake kuwa wanachuo wanaojiunga hapo,
huchaguliwa kwa kutimiza sifa, na kwamba nao huamua kujiunga kwa
kuelewa ugumu wa kazi yenyewe baada ya kumaliza masomo yao.
Alisema utoaji bora wa huduma za afya,
lazima utanguliwe na huruma na ubinadamu, na kwamba kazi hizo humtaka
mhudumu kuzingatia wito wa kuwahudumia wagonjwa kwa upendo pamoja na
maadili ya taaluma yenyewe.
"Kwa bahati mbaya, wapo baadhi ya
wafanyakazi wa sekta ya afya ambao huweka pembeni vigezo hivyo na
matokeo yake hutokea manung’uniko kwa wagonjwa wanaohudumiwa", alieleza
Dk. Shein
Alisema, mlahaka mzuri na lugha nzuri kwa mgonjwa ni miongoni mwa mambo muhimu katika kumuhudumia mgonjwa.
Pamoja na changamoto mbalimbali
zinazoikabili sekta hiyo na chuo hicho, Dk. Shein aliwapongezz viongozi
na wafanyakazi wa hospitali za Unguja na Pemba na taasisi za afya kwa
kujitahidi kuondoa udhaifu huo kwa lengo la kuwahudumia vizuri wagonjwa.
Alieleza kuwa, siku zote mgonjwa
anahitaji huruma na imani kutoka kwa anaemuhudumia wakiwemo wanafunzi
wanaohitumu kwenye chuo hicho.
Aliwahakikishia wanafunzi na watendaji
wa sekta hiyo, kuwa daima serikali inatambua na kuthamini mchango wao
kwa jamii, na hivyo inajitahidi kuimarisha maslahi yao kila uwezo
unapopatikana.
Aidha, alisema serikali inaendelea na
sera yake ya kutoa matibabu bure kwa wananchi, ingawa katika baadhi ya
maeneo, inapokwazwa na ufinyu wa bajeti huwataka kuchangia, lakini si
nia ya serikali kuona wananchi wanapata shida.
Pia alifahamisha kuwa, katika kutanua
wigo wa taaluma chuoni hapo, serikali imeamua kukiweka chini ya Chuo cha
Taifa Zanzibar (SUZA), pamoja na kuanza kutoa digriii ya uuguzi
kuanzia mwaka huu.
Aliishukuru serikali ya Oman chini ya
uongozi wa Sultan Qaboos Bin Said, kwa uamuzi wake wa kujenga na
kukiendeleza chuo hicho, akisema hiyo ni dalili ya mahaba makubwa kwa
wananchi wa Zanzibar, ambao wana uhusiano wa miaka mingi na wenzao wa
Oman.
Mapema, akitoa taarifa za ujenzi huo,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Saleh Mohammed Jidawi, alisema hadi
kukamilika kwake, ujenzi huo umegharimu dola za Kimarekani milioni 2.36,
na samani zake dola 277,000.
Naye Waziri wa Afya Juma Duni Haji,
alisema kujengwa chuo hicho na kuongezwa kwa dakhalia hizo,
kutawaondoshea wanafunzi na walimu usumbufu kwani saa watapata nafasi
ya kusoma na kufanya kazi kwa utulivu.
Mkuu wa chuo hicho Dk. Haji Mwita,
aliishukuru serikali kwa kushirikiana na uongozi na bodi ya chuo katika
jitihada za kukiendeleza huku akiainisha changamoto kadhaa zinazohitaji
kupatiwa ufumbuzi zikiwemo uhaba wa walimu, usafiri, vitendea kazi na
uvamizi wa eneo la chuo unaofanywa na watu mbalimbali.
Kwa upande wake, Mshauri wa masuala ya
afya wa serikali ya Oman, Dk. Sultan Al Busaidy, akitoa salamu sake kwa
niaba ya nchi yake, alisema nchi yake inaona fahari kubwa kuiona
Zanzibar ikipiga hatua katika kustawisha hali za watu wake, hasa katika
sekta ya afya na elimu.
Alisema serikali ya nchi yake,
inajivunia uhusiano wa dhati na udugu wa damu uliopo kati ya wananchi
wa nchi mbili hizo, na akawaombea Wazanzibari mafanikio zaidi katika
kuleta maendeleo.
Ujenzi wa majengo hayo uliofanywa na
kampuni ya Mazrui Building Contractors, uliwekwa mwezi Januari 2011,
baada ya kuwekwa jiwe la msingi na Rais Dk. Shein tarehe 6 ya mwezi huo.
No comments:
Post a Comment