Na Salvator Rweyemamu, Mwanza
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo (jana), Ijumaa, Septemba 6, 2013, amefungua shule ya kisasa ya
msingi ya Ntulya katika kata ya Mondo, Wilaya ya Misungwi, iliyotolewa
kama zawadi kwa wanakijiji cha Ntulya na taasisi moja ya Marekani.
Aidha,
Rais Kikwete amezindua huduma za x-ray kwenye Hospitali ya Wilaya ya
Misungwi mjini Misungwi ikiwa ni hatua zake za mwanzo kwenye siku ya
kwanza ya ziara ya kikazi ya Rais Kikwete katika mkoa wa Mwanza ambako
atakaa siku tano akikagua na kuzindua miradi na shughuli za maendeleo.
Shule
ya Ntulya iliyoko kilomita 47 kutoka mjini Misungwi ina wanafunzi 466
na walimu 11 na ni zawadi ya Taasisi ya Africa School House ya Marekani
kwa wanakijiji cha Ntulya ambako Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi
hiyo, Dkt. Aimee Bessire ambaye amehudhuria sherehe za uzinduzi wa shule
hiyo na mume wake, Mark Bessire walipata kuishi wakifanya utafiti
kuhusu utamaduni wa Kabila la Wasukuma.
Shule
hiyo ya kisasa imejengwa kwa matofali ya kuchomwa na ilijengwa kati ya
2008 na 2010. Ina madarasa 11, nyumba 10 za walimu na kisima cha maji
safi. Kwa jumla shule hiyo ina uwezo wa kuwa na wanafunzi 600 kwa wakati
mmoja.
Akizungumza
kwenye sherehe za leo, Dkt. Bessire ambaye amezungumza kwa ufasaha
lugha za Kiingereza, Kiswahili na Kisukuma, amesema kuwa shule hiyo
imejengwa kwa jumla ya sh bilioni 1.038, na kati ya hizo sh milioni 980
zilitolewa na Africa School House, Halmashauri ya Misungwi ilichangia sh
milioni 28 na nguvu za wananchi zilichangia sh milioni 30.
Taasisi
hiyo ya Marekani pia imewajengea wanakijiji hao wa Ntulya Kituo cha
Afya kwenye eneo hilo la shule na Dkt. Bessire amesema kuwa Taasisi hiyo
ina mipango ya kujenga shule ya mfano ya sekondari ya bweni ya
wasichana.
Dkt. Bessire pia amesema kuwa yataanzishwa madarasa kwenye shule hiyo kwa ajili ya watu wazima wasiojua kusoma na kuandika.
No comments:
Post a Comment