Na Salva Rweyemamu, Misungwi
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa kazi kuu na kipimo halisi cha kiongozi bora na hodari ni
jinsi kiongozi anavyohangaikia maendeleo ya wananchi, ubunifu wake wa
kuwaongezea wananchi mapato na kujali kumaliza kero zao.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa kazi ya madiwani nchini haiwezi kuwa ni
kupokea posho za vikao ama kupima na kujigawia viwanja bali iwe ni
kupambana na umasikini wa wananchi ambayo ndiyo kazi waliyoomba wakati
wanatafuta kura za kuwa madiwani.
Vile
vile, Rais amewataka madiwani wote nchini kutumia haraka na ipasavyo
fedha zinazotolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ndani ya halmashauri
zao na siyo kuziweka hadi mwisho wa mwaka wa fedha na kulazimika
kuzirudisha kwenye Mfuko wa Barabara.
Rais
Kikwete ameyasema hayo leo, Ijumaa, Septemba 6, 2013, wakati alipopokea
Taarifa ya Maendeleo ya Wilaya ya Misungwi wakati alipoanza ziara ya
siku tano katika Mkoa wa Mwanza kukagua na kufungua shughuli na miradi
ya maendeleo.
Akiuliza maswali na kutoa maelekezo wakati Ripoti hiyo inawakilishwa na
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Bibi Mariam Lugaija kwenye Shule ya
Sekondari ya Misungwi, Rais Kikwete amewaambia viongozi wa Wilaya hiyo
na wa Mkoa wa Mwanza:
“Kazi
muhimu na uhodari wa kiongozi unathibitishwa na jinsi kiongozi huyo
anavyopambana kupunguza umasikini wa wananchi na anavyobuni mbinu za
kuongeza mapato ya wale anaowaongoza.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Kila kiongozi lazima awe na uchungu wa maendeleo na
tamaa ya kuleta mabadiliko kwa wananchi wao. Kazi ya kiongozi ni
kuhangaika na maendeleo ya wananchi.”
Akionyeshwa
kutoridhishwa na kiwango cha uongozi cha baadhi ya madiwani mkoani
humo, Rais Kikwete amewaambia viongozi hao: “Kazi ya madiwani haiwezi
kuwa kupima na kugawa viwanja. Mliomba kazi ya udiwani ili kuwatumia
wananchi na kuwaletea maendeleo. Nyie madiwani hamuwezi kuendelea
kuwasibiri TASAF kuwaletea wananchi wenu maendeleo. Hii ni kazi yenu.”
Ameongeza
kuelekeza Rais Kikwete: “Kazi yenu haiwezi kuwa ni kusubiri posho ya
vikao na kupokea mishahara bure. Lazima muwe na tamaa ya maendeleo ya
wananchi wenu.”
Aidha,
aliwakumbusha kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa halmashauri kwa
ajili ya ujenzi wa barabara kwenye halmashauri hizo, lakini madiwani
wanashindwa ama kuchelewa kuzitumia fedha hizo kujenga barabara hadi
mwaka wa fedha unamalizika.
“Hili
nalo halikubaliki. Kwa sababu Serikali inawapa fedha nyingi, lakini
nyie hamzitumii kwa wakati na fedha hizo zinarudishwa kwenye Mfuko wa
Barabara.”
No comments:
Post a Comment