Friday, September 06, 2013

SOMA KISA HIKI ILI UJIFUNZE TABIA ZA MATAPELI WA MJINI

Ndugu zangu,

Naomba nichukue nafasi hii niweze ku share na nyinyi tukio lililonitokea Jumatatu ya tarehe 12 Agosti, 2013 saa 8 mchana. Nilikuwa nimekwenda  NIDA kwenye ofisi zao zilizopo Victoria Hse katika jengo  lililoandikwa  BMTL.
Nilikwenda hapo kuchukua national ID yangu, nilipotoka  nikaingia katika ATM ya NBC ambayo iko kwenye jengo hilo. Nilipo maliza  nikaelekea kwenye gari niliyokuwa nimeiegesha nje ya jengo. Hapo nikamkuta mama mmoja anaweza akawa na umri kama miaka 45hivi. Mweupe kwa rangi na ni mnene  kiasi, ana tumbo kubwa na si mrefu lakini sio mfupi sana.
Alikuwa amevaa gauni la kitenge. Alikuwa amebeba handbag kubwa ya brown, kaikumbatia kifuani.
Akanisalimia kwa upole na kuniuliza kama ndani ya hilo jengo ninalotoka kuna ofisi za Barrick Gold. Nikamwambia sikuona kama kuna  ofisi za Barrick akaniambia kuwa anatokea Tanga, yeye ni mchimbaji mdogo na alikuwa na dhahabu ambayo alikuwa anataka kuipeleka huko kwa  vile watu  wanaokwenda kununua huko Handeni wanawalalia bei na ameongea na dereva  wa Barrick akamwambia akija Dar aende ofisini kwao atampatia bei nzuri. Alikuwa anaongea na lafudhi ya kitanga.
Wakati ananiambia hayo, walikuwepo watu wengine, walinzi nk lakini mtu mmoja mwanamme amevaa suruali ya rangi ya blu na shati la  blu light alikuwa karibu, akaingilia mazungumzo akamwambia, mama usiongee mambo ya namna hiyo kwa sauti, hapa mjini watu sio wazuri, umemkuta  huyu dada (mimi) mstaarabu lakini wengine watakufanyia unyama.
Huyo kaka akaendelea kujieleza kuwa yeye anavyojua ofisi za Barrick ziko Oysterbay, lakini yeye anafanyakazi NBC na bosi wake ndio branch manager pale Victoria, na huwa ananunua dhahabu. Akaendelea  kutueleza kuwa  anaweza akampeleka huyo dada kwa bosi wake lakini bei haitakuwa nzuri sana maana bosi wake huwa ananunua hiyo dhahabu na kumuuzia padri mmoja wa kanisa la Monrovia lililoko sinza.
Yule dada akasema kama padri atampa bei nzuri yeye hana tabu atamuuzia tu. yule jamaa akapiga simu kwa "padri. " ili ajue kama yupo na bado anataka kununua hiyo dhahabu. Basi akapiga hiyo simu na akanipa mimi niongee,  nikawa kama nimepigwa na bumbuwazi maana sikujua hata hiyo dhahabu inauzwa kwa vipimo gani, yule dada akawa ananielekeza jinsi ya kusema, sijui tola moja atainunuaje, padri akanijibu kuwa ananunua kwa 170,000 yule dada akaniambia hiyo nzuri maana hao jamaa waliokuwa wakienda huko Handeni, walikuwa wanawalipa 100,000 tu.
Basi yule dada kwa upooole sana akaniomba "dada naomba tafadhali ndugu yangu unisindikize maana mmeshanitia uoga, nitakupa na wewe asante yako". Nikamwambia mimi sijali hilo la asante, ila namuonea huruma anaweza  akadhulumiwa. Yule dereva akaanza kunielekeza huko kwa padri, nikamwambia sielewi, akasema basi ngoja nikimbie niwapeleke, lakini namimi lazima nipate. Nilikuwa nikitoka hapo NIDA narudi  nyumbani,  nikaona kwa vile Sinza ni karibu na Kijitonyama, basi ngoja nimsaidie.
Hata sikupata nafasi ya kutafakari, yule dada akaingia kwenye gari yangu, na yule dereva, akaingia kwenye gari yake Mark X reg inaanzia na C tukaanza kuongozana, ndani ya gari yule dada akawa ananieleza jinsi Yesu alivyotuunganisha, aliponiuliza jina langu, nikamwambia, akagundua kuwa mimi muislam akabadili maongezi na kunieleza hata yeye muislam anaitwa Rehema, na kwamba anazo dhahabu zingine lakini hataki yule dereva ajue ila atanipa mimi share kubwa zaidi..akaniambia yeye kaja kamili (ana madawa ya kumkinga) kwa hiyo nisihofu.
Tulipofika usawa na Usalama wa Taifa, nikaanza kupata fikira zaidi, nikasema moyoni kwangu, hivi Barrick tangu lini wananunua vidhahabu vidogo vidogo vya mkobani? Ghafla nikaona roho yangu imekuwa nzito sana, nikamwambia, unajua ni vema nimpigie kaka yangu ambaye ni Polisi, yuko pale polisi mabatini (huo ni uongo sina kaka yeyote polisi) nimueleze tunakokwenda ili atupe msaada atufuatilie nyuma. Akanijibu, hapana dada usimpigie kabisaa si unakumbuka kina Zombe waliwafanya nini wale jamaa wa mahenge? Nikamwambia lakini huyu ni kaka yangu, akasema hapana dada usimpigie acha tu mimi niko kamili kabisaa usihofu, na hapo sasa roho yangu ikakataa kabisa! Nikatoka nje ya foleni nikapita kushoto halafu nikaingia mbele ya ile gari ya dereva nikasimamisha gari nikamwambia yule dada, naona wewe nenda tu na yule dereva mimi roho yangu nzito, akasema khaa dada wee unanitelekeza, nikamwambia wewe nenda tu na mungu atakusaidia mambo yako yataenda salama.
Basi akashuka kwa upole, akaenda kwenye ile gari, nikawaacha wapite mbele nikawa nawafuata nyuma, lakini nikampigia rafiki yangu Monica, nikawa namueleza huo mkasa.
Yule dereva alikuwa anaangalia kwenye kioo, nadhani yule dada alimueleza kuhusu nilivyomwambia nimpigie kaka yangu polisi, na akaniona naongea na simu, ghafla, nikashtuka nawaona wanapiga u-turn, kuna mtu alikuwa ankuja na pikipiki wakamzoa, wakaondoka speed kali wakatokomea zao! Wakaelekea tulikotoka!
Hapo nilistuka nikajua kuwa wale walikuwa wanajuana na ule ulikuwa ni mtego niliokuwa nimeuingia na kuponyoka kupitia kwenye tundu ya sindano.
Nilitetemeka sana hata nikawa siwezi kuendesha gari, na kujiona jinsi nilivyofanya ujinga ambao ungeweza kunigharimu hata maisha yangu.
Nilijiuliza kwanini nilikubali tu yule dada aingie kwenye gari yangu na huku simjui?
Nilijaribu kutafakari kama nilipata tamaa kuwa nitafaidika? Lakini ndugu zangu, naomba muamini kuwa hilo halikuwa motisha kwangu, bali niliona kama nitakuwa nimemsaidia mwanamke wenzangu, aliyekuwa anajifanya mpoole sana na kwamba anahangaika aweze kulea watoto wake, ambaye vinginevyo angeweza kudhulumiwa, nisijue kuwa yeye ndiye jambazi mwenyewe!
Nimeona nichukue wasaa huu niwapeni tahadhari, kwani leo mimi lakini kesho inaweza ikawa niwewe. Wema hivi sasa ni hatari tupu, tafadhali jihadharini..
Naomba nanyinyi pia muwatahadharishe ndugu jamaa na marafiki zetu wengine wasije na wao wakadhurika.
Namshukuru Mungu, Subhana wa Taalah kwa kunipa uwezo wa kuamka na kuchukua hatua mapema kabla madhara makubwa hayajanikuta.

Alhamdullilah!
Ndugu yenu,
Mwanamvua

No comments:

Post a Comment