Msako wa kuwakamata wahamiaji haramu unaoendelea nchini kote, umezua balaa, baada ya vibaka na vijana wengine wa kihuni, jijini Dar es Salaam, kuutumia kujeruhi watu na kupora mali zao kwa kutumia silaha mbalimbali, yakiwamo mapanga na visu, wakijifanya ni maofisa uhamiaji.
Matukio hayo, ambayo yana takriban wiki sasa, yanadaiwa kukithiri katika maeneo ya Mwananyamala na kuwafanya wakazi wake kuishi kwa hofu.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ernest Kimora, alithibitisha kuibuka kwa vijana hao wa kihuni wanaotumia dawa za kulevya na bangi na kusema operesheni ya kuwakamata inaendelea.
Habari zilizopatikana jana zinaeleza kuwa maeneo, ambayo vijana hao wamekuwa wakiyatumia kuendesha vitendo hivyo vya uhalifu, ni pamoja na Mwananyamala Kwa Kopa, Kwa Mama Zakaria na Ujiji.
Wanadaiwa kuvamia majumbani na mitaani katika nyakati za usiku na mchana na kuwajeruhi watu kwa kutumia silaha hizo na kisha kupora mali zao.
Baadhi ya mali ambazo zimeripotiwa kuporwa na vijana hao ni pamoja na simu za mikononi na fedha taslimu. Huku wakijifanya kuwa ni maofisa uhamiaji, vijana hao wa kihuni wamekuwa wakiwavizia mitaani hata raia wema wa Tanzania na kuwajeruhi na kuwapora mali.
Askari polisi wa kituo kidogo cha Minazini, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, aliliambia NIPASHE jana kuwa awali vijana hao walikuwa wakiendesha vitendo hivyo kwa wahamiaji haramu wanaoishi katika maeneo hayo.
Kwa mujibu wa askari huyo, wengi wa wahamiaji haramu wanaoishi katika maeneo hayo, ni wa kabila la Wanyasa kutoka Malawi na kwamba, wamekuwa wakiingia gharama kubwa za kodi ya nyumba ili waishi nchini.
Alisema vijana hao wa kihuni walikuwa wakivamia nyumba wanazoishi wahamiaji haramu na kupora mali zao muda mfupi tu baada ya wahamiaji hao kukamatwa na maofisa uhamiaji halali kutoka Idara ya Uhamiaji.
Lakini alisema baada ya kuonja ladha ya ‘utamu’ wa kupora mali za wahamiaji haramu majumbani, vijana hao wakaanza tabia ya kuwavizia mitaani na njiani watu wengine bila kujali kwamba, ni raia wema wa Tanzania.
Alisema wanapokutana na mtu njiani au mtaani wanamsimamisha na kujitambulisha kuwa wao ni maofisa uhamiaji.
Alisema baada ya kujitambulisha hivyo, humtaka mtu huyo awathibitishie uraia wake kwa kuonyesha kitambulisho au kibali kinachomruhusu kuishi nchini.
“Mtu huyo akijaribu kusita au kubishana nao, wanamvamia na kuanza kumshambulia kwa visu na mapanga na kumpora kila alichonacho,” alisema askari huyo.
Baadhi ya wakazi wa maeneo hayo waliozungumza na NIPASHE jana, pia walithibitisha vijana hao wa kihuni kuendesha vitendo hivyo na kwamba, wamekuwa wakiishi kwa hofu.
NIPASHE ilifika katika kituo hicho kidogo cha polisi na kushuhudia mmoja wa watu aliyejeruhiwa na vijana hao wa kihuni kwa mapanga kichwani na katika sikio la upande wa kushoto.
Mtu huyo, Shukuru Mfaume, mkazi wa Mwananyamala ‘B’, Mtaa wa Mpunga, alidai mbali na kujeruhiwa kwa mapanga, pia aliporwa fedha taslimu.
Alisema kati ya fedha alizoporwa, ni pamoja na Rand 500 za Afrika Kusini, Sh. 20,000 za Tanzania, simu ya mkononi yenye thamani ya Sh. 200,000 na saa ya mkononi, ambayo alisema thamani yake haikumbuki.
Shukuru alisema baada ya kushambuliwa na vijana hao usiku wa kuamkia jana, alitoa taarifa katika kituo hicho cha polisi na kufungua jalada namba MNZ/RB/1156/2013.
Alisema pia alipewa hati maalum ya polisi ya matibabu na kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
“(Vijana hao wa kihuni) Walinikuta eneo la Msikiti Kwa Bozi njiani. Walikuwa kundi la watu watano wakiwa kwenye Bajaj na mapanga. Wakashuka. Baada ya kuniuliza uraia wangu na mimi kuwajibu, wakaanza kunishambulia na kunipora,” alisema.
NIPASHE ilishuhudia vijana wengine wawili; mmoja akiwa amejeruhiwa na vijana hao usiku wa kuamkia jana mdomoni na mwingine kwenye paji la uso wakisubiri kuandikisha maelezo katika kituo hicho.
Pia ilishuhudia watu saba wanaosadikiwa kuwa ni Wanyasa, ambao walikwenda katika kituo hicho cha polisi kulalamika kuvamiwa na vijana hao wa kihuni na kujeruhiwa na kuporwa mali zao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alipoulizwa, alisema yuko safarini. Hata hivyo, alisema taarifa za matukio ya uhalifu wa vijana hao wa kihuni amezisikia.
“Niko safarini, Lakini nimekuwa nikikisikia habari hizo tangu jana na wamefuatilia,” alisema na kumtaka mwandishi awasiliane na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Kimora.
Kimora alipoulizwa na NIPASHE jana, alisema taarifa za vijana hao wa kihuni anazo na kwamba, operesheni ya kuwakamata inaendelea na kwamba, inafanywa na polisi kwa kushirikiana na viongozi wa mtaa.
Hata hivyo, alipotakiwa kutaja idadi ya vijana wa kihuni wanaoendesha uhalifu huo waliokwisha kukamatwa kufikia jana, alisema taarifa za suala hilo zitatolewa leo na Kamanda wa Poilisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Msako wa kuwakamata wahamiaji haramu unafuatia agizo la Rais Kikwete alilolitoa alipokuwa katika ziara mkoani Kagera Julai 29, mwaka huu.
Hata hivyo, agizo hilo halikutoa ruhusa kwa wahalifu wakiwamo vibaka kuwadhuru wengine kama inavyofanyika Mwananyamala kwa sasa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment