Waziri
Mkuu, Mizengo pinda akizungumza baada ya kutembelea kampuni ya
Aluminium Corporation of China , Beijing akiwa katika ziara ya kikazi
nchini China Oktoba 18, 2013. (picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………..
*Ataka viongozi wabadili mitazamo yao kuhusu sekta binafsi
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema kuna haja ya taasisi za mafunzo ya uongozi
za China na Tanzania kuandaa kozi zenye kuwafaa makundi fulani ya
viongozi ambazo zitasaidia kubadili mwelekeo wao na utendaji wao wa kazi
hasa katika masuala yanayohusu sekta binafsi.
Amesema
taasisi hizo zinapaswa kuwa na uelewa mkubwa kuhusu ushirikiano wa
pamoja baina ya sekta binafsi na za umma (PPP), zinapaswa kujua faida za
ushirikiano huo na zinapaswa kubainisha ni sekta zipi zinapaswa
kutekeleza mpango huo wa ushirikiano.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Oktoba 18, 2013) wakati akifungua mafunzo
ya siku 14 kwa maafisa 20 kutoka idara na taasisi za serikali ya
Tanzania yanayoendeshwa kwa pamoja baina ya Chuo cha Uongozi cha China
na Taasisi ya Uongozi ya Tanzania.
Mafunzo
hayo ni sehemu ya mpango wa Serikali kuboresha utendaji wa Maeneo ya
Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZ) yameanza leo kwenye Chuo cha Uongozi
cha China (China Governance Academy), jijini Beijing, China.
Alisema
Tanzania imefanya maamuzi ya kutumia ushirikiano wa pamoja baina ya
sekta binafsi na za umma (PPP) kama njia ya kukuza na kuendeleza
miundombinu, kuhamisha ujuzi na teknolojia pamoja na ujenzi wa viwanda.
“Ni
muhimu taasisi zetu hizi mbili zikatambua jambo hili na kuchangia kwa
juhudi zote ili kuhakikisha kuwa linafanikiwa,” alisema.
Alisema
kozi kama hizo zinapaswa kuwalenga watumishi kutoka taasisi za serikali
pamoja na sekta binafsi na akazitaka taasisi hizo kuhakikisha
zinaisaidia kuwepo kwa ufanisi wa hali ya juu kwenye ushirikiano wa
pamoja baina ya sekta binafsi na za umma. “Muwasaidie watu hawa waweze
kutambua ni wakati gani ushirikiano wa aina hii unakuwa wa manufaa zaidi
kwa wahusika, ni wakati gani wahusika wanafaidika na PPP, je
wanakabiliwa na changamoto zipi, na wanafanyaje ili kukabiliana na
changamoto zinazojitokeza,” aliongeza.
Alisema jambo lililo wazi kuwa ushirkiano baina ya wajasiriamali wa Kichina na wa Kitanzania utasaidia kuongeza fursa za kuhamisha
ujuzi na teknolojia pamoja na kuendeleza miundombinu. “Natambua kwamba
kuna wafanyabiashara zaidi ya 500 wa kutoka China ambao wako nchini
Tanzania, hawa wanachangia maendeleo ya kiuchumi Tanzania kwa kuingiza
teknolojia mpya na kutoa fursa za ajira,” aliongeza.
Waziri
Mkuu ambaye yuko katika siku ya tatu ya ziara ya kikazi yake ya siku
tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo, alitembelea kiwanda cha
aluminium cha China CHINALCO) na kiwanda cha kutengeneza zana za kijeshi
ambako alionyeshwa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na viwanda hivyo.Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, (OWM) Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk.
Mary Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda; Waziri
wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uvuvi na Mifugo wa
Zanzibar, Bw. Abdallah Jihad Hassan; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Juma Maalim na Naibu Waziri wa
Fedha, Bibi Saada Salum Mkuya.
Pia
amefuatana na Balozi wa China, Luteni Jenerali (Mst.) Abdulrahaman
Shimbo, Wakuu wa mikoa ya Mtwara, Shinyanga na Simiyu; wabunge wawili,
Bw. Godfrey Zambi (Mbozi) na Dk. Titus Kamani (Busega) na viongozi
wakuu wa Tanzania Private Sector Foundation, Bw. Reginald Mengi, Bw. Salum Shamte na Bw. Godfery Simbeye.
No comments:
Post a Comment