HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, ALIYOITOA BUNGENI KUHUSU JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI, 7 NOVEMBA, 2013, DODOMA
Mheshimiwa
Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa
Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa
Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa
Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni;
Waheshimiwa
Wabunge;
Mabibi
na Mabwana;
Nakushukuru
sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga muda wenu ili niweze
kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu masuala muhimu kwa uhai,
ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika;
Nimeambiwa
kuwa taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge,
kumekuwepo na dhana mbalimbali. Wapo
waliodhani kuwa nakuja kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa
matukio ya wiki chache zilizopita. Wapo waliodhani nakuja kuzungumzia “Operesheni
Tokomeza”. Tena wapo waliokwenda mbali
na kufikiria kuwa nakuja kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge waliotoa maoni yao
kuelezea kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni hii muhimu. Na
wapo pia waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa majeshi yetu ya Tanzania
katika Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Hayo
si makusudio yangu. Kinachonileta mbele
ya Bunge lako Tukufu ni kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa
Tanzania katika Jumuiya hiyo. Lakini, kwa
sababu ya umuhimu wa masuala hayo niliyoyataja na rai niliyopewa kuwa niyasemee
japo kidogo. Nimeona ni vyema nifanye
hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, napenda
kusema kuwa tumefikia hatua nzuri katika utekelezaji wake. Kama mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imekamilisha, kwa mafanikio, hatua ya mwanzo ya kusikiliza maoni ya wananchi
kuhusu Katiba wanayoitaka. Pia
walishatoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba na kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya Katiba. Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi wote, ni
Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 15
Desemba 2013 au kabla ya hapo.
Mheshimiwa Spika;
Kwa
upande wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka kwenu
yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua zinazofuata. Jambo la kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya
Kura ya Maoni na pili kufanyika kwa marekebisho ya nyongeza ya Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha utekelezaji wake. Baada ya Bunge kukamilisha kazi yake hiyo itafuatia
uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba
ifanyike na kutupatia Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na wananchi
katika Kura ya Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani, tutakuwa tumepata
Katiba Mpya. Hivi sasa katika Serikali
tunaendelea kufanya tafakuri na tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na
Kura ya Maoni kufanyika kwa mafanikio.
Operesheni
Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
Napenda
kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa sikukasirishwa na
maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni kuokoa maliasili za misitu na wanyamapori
dhidi ya uvunaji haramu ambao umefikia kiwango kinachotishia kutoweka kwa
raslimali hizo. Kwa kweli hali inatisha. Miti inakwisha na ndovu na faru
wanaangamia.
Mheshimiwa Spika;
Wakati,
tunapata Uhuru Tanzania ilikuwa na ndovu waliokadiriwa kuwa takribani 350,000. Lakini, kwa sababu ya ujangili uliokithiri katika
miaka ya 1970 na 1980 ilipofika mwaka 1989 kulikuwa na ndovu wapatao 55,000
tu. Ilipofikia hali hiyo Serikali
ikaanzisha Operesheni Uhai iliyohusisha Jeshi la Ulinzi na kuongozwa na Meja
Jenerali John Walden (ambaye sasa ni
marehemu) kuendesha mapambano dhidi ya majangili. Kutokana na hatua hiyo na uamuzi
wa Shirika linalosimamia biashara ya wanyama walioko kwenye hatari ya kutoweka (CITES)
kupiga marufuku biashara ya pembe za ndovu duniani, idadi ya ndovu nchini
iliongezeka na kufikia 110,000 mwaka
2009.
Tumewaomba Fankfurt
Zoological Society ambao ni wabia wetu katika uhifadhi wa wanyama pori kwa
miaka mingi wafanye sensa maalum ya ndovu katika Hifadhi ya Selous na kote
nchini ili tujue hali halisi ikoje. Kazi
hiyo inaendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya mwaka 2009 kumezuka wimbi jipya, tena la nguvu kubwa, la kuua ndovu na
faru nchini na kwingineko katika Bara la Afrika ambako wanyama hao wapo. Idadi kubwa ya meno ya ndovu yaliyokamatwa na
yanaoendelea kukamatwa nchini na kwingineko duniani inathibitisha ukweli
huo. Kwa mfano, kati ya mwaka 2010 na Septemba,
2013, hapa nchini, kwa jitihada zetu vipande 3,899 vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo 11,212 na vipande 22 vya
pembe za ndovu zilizochakatwa zenye uzito wa kilo 3,978 vilikamatwa. Aidha,
katika kipindi hicho vipande 4,692
vya pembe za ndovu vilivyotokea Tanzania vyenye uzito wa kilo 17,797 vilikamatwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika;
Kama
nilivyokwisha sema hapo awali matatizo ya kuuawa kwa wingi kwa ndovu na faru
lipo pia katika nchi nyingine Afrika zenye wanyama hao. Nchi
za Gabon, Kenya, Afrika ya Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Zimbabwe,
Zambia na nyinginezo nazo zinakabiliwa na matatizo kama yetu. Tatizo limekuwa kubwa kiasi cha kuifanya
Jumuiya ya Kimataifa kushtuka na kuamua kuingilia kati kwa namna mbili. Kwanza kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa
ndovu na faru katika nchi zenye wanyama hao.
Na, pili, kuchukua hatua thabiti kudhibiti biashara ya meno ya ndovu
duniani. Ni ukweli ulio wazi kuwa kama
hakutakuwepo na wanunuzi wa meno ya ndovu na faru hakuna ndovu au faru atakayeuawa.
Mheshimiwa
Spika;
Kutokana na ukweli ulivyo uamuzi wetu wa
kuendesha Operesheni Tokomeza ni sahihi kabisa.
Manufaa yaliyopatikana baada ya Operesheni Uhai ya mwaka 1989
yanatupa imani kuwa na safari hii pia
tutafanikiwa. Tusipochukua hatua kama
hii sasa ni sawa na kuwapa kibali majangili waendelee kumaliza ndovu na
faru nchini. Hakika wanyama hao watakwisha. Itakuwa ni aibu kubwa
kwetu na historia
itatuhukumu vibaya.
Mheshimiwa Spika;
Tumeyasikia
maelezo ya Wabunge kuhusu kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji
wa Operesheni Tokomeza. Nawaahidi kuwa
tutayafanyia kazi. Serikali imeahirisha
kwa muda Operesheni hii ili kujipa muda wa kurekebisha kasoro hizo na kujipanga
upya. Watendaji wasiokuwa waadilifu na
wale wasiokuwa waaminifu wataondolewa. Halikadhalika,
kasoro za kimfumo nazo zitasahihishwa ili tutakapoanza upya Operesheni itekelezwe
kwa mafanikio yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika;
Miongoni
mwa mambo yaliyozungumzwa kwa uchungu ni ukamataji wa mifugo iliyokutwa kwenye
mapori ya hifadhi za wanyama na vitendo vibaya walivyofanyiwa wenye mifugo na
mifugo yenyewe. Narudia kusisitiza kuwa taarifa
zote hizo zitafanyiwa kazi na waliohusika watachukuliwa hatua zipasazo. Pamoja na hayo, napenda kuwakumbusha ninyi watunga
sheria wetu kuwa sheria ya hifadhi za wanyamapori hairuhusu mifugo kuchungwa
katika maeneo ya hifadhi.
Naomba
tuwakumbushe
wananchi tunaowaongoza wajiepushe na kufanya hivyo. Ni uvunjifu wa
Sheria za nchi. Naomba pia, wananchi waelimishwe ili wajue kuwa
wakifanya hivyo na kukutwa katika maeneo hayo na mifugo yao kuna adhabu
iliyotamkwa kwenye sheria. Hivyo tusiwalaumu
wala kuwaona maafisa wanyamapori kuwa ni watu wabaya. Wanatekeleza
Sheria iliyotungwa na Bunge
hili. Pale wanapotenda visivyo tuseme,
watawajibishwa ipasavyo.
Jeshi
la Umoja wa Mataifa Kongo
Mheshimiwa Spika;
Mapema
mwaka huu (2013) Umoja wa Mataifa uliomba nchi yetu ichangie kikosi kimoja cha
wanajeshi katika Brigedi Maalum iliyoundwa na Umoja huo kuongeza nguvu ya kudhibiti
waasi Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Lengo la msingi ni kuiwezesha nchi hiyo kupata
amani ya kudumu ambayo imekosekana kwa muda mrefu kutokana na kuibuka kwa uasi mara
kwa mara.
Mheshimiwa Spika;
Tulikubali,
kwani hata kabla ya kuombwa na Umoja wa Mataifa tulishakubali maombi kama hayo yaliyotolewa
kwenye Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu.
Ni miezi saba (tangu Aprili) sasa tangu wanajeshi wetu waende Kongo na
wamekuwa wanatekeleza majukumu yao vizuri tena kwa weledi na nidhamu ya hali ya
juu. Sifa hiyo kwa wanajeshi wetu
imekuwa inatolewa na viongozi wa juu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa juu wa
Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo (MONUSCO) na viongozi wa juu wa Serikali ya
Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Majeshi
ya Umoja wa Mataifa hupewa majukumu na mamlaka ya namna mbili. Yapo
yanayopewa jukumu la kulinda amani tu. Wanajeshi wake huwa hawapewi
majukumu ya
kimapigano na hata pale wanaposhambuliwa wanatakiwa kujihami tu. Kwa
kawaida majeshi yenye jukumu hili hupelekwa
mahali ambapo kumekuwepo na makubaliano ya kuacha mapigano. Wanapelekwa
kusaidia kuona Mkataba
unatekelezwa ipasavyo.
Aina ya pili ni ile
ya majeshi yanayopelekwa mahali ambapo hakuna amani hivyo wanapewa jukumu la
kuchukua hatua za kufanya amani ipatikane.
Majeshi haya hupewa mamlaka ya kutumia nguvu ya kijeshi dhidi ya
wanaosababisha amani ikosekane kama ni lazima kufanya hivyo. Maana yake ni kwamba wanayo ruhusa kuingia
katika mapigano dhidi ya watu au vikundi vinavyovuruga amani. Tofauti na wenzao wa kundi la kwanza, wanajeshi
wa kundi la pili wako kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha au kujeruhiwa
kuliko wenzao ingawaje wapo wengi nao wameuawa na kujeruhiwa.
Mheshimiwa Spika;
Wanajeshi wetu wamekwenda
Kongo chini ya utaratibu huu wa pili ambao unahusu kuingia kwenye mapigano dhidi
ya waasi kama hapana budi kufanya hivyo.
Wametekeleza majukumu yao vyema na kwa ujasiri mkubwa na weledi wa hali
ya juu. Bahati mbaya tumepoteza vijana wetu watatu shupavu. Daima tutawakumbuka na tutawaenzi ipasavyo mashujaa
wetu hawa. Tuzidi kuwaombea kwa Mola
awape mapumziko mema. Ameen.
Wakati huo huo,
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Rais Joseph Kabila wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mafanikio ya kihistoria waliyoyapata hivi
majuzi dhidi ya waasi wa M23. Tunamtakia
yeye na wananchi wa Kongo kila la heri katika kazi ngumu iliyo mbele yao ya
kujenga upya eneo hilo na kujenga mahusiano mapya miongoni mwa watu wa Kongo. Pia nawapongeza sana wanajeshi wa Brigedi
Maalum ya Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri waliyoifanya iliyowezesha mafanikio
kupatikana. Wanajeshi hao ni kutoka Afrika Kusini,
Tanzania na Malawi wanaoongozwa na Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa
JWTZ.
Jumuiya
ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika;
Kama
nilivyosema awali, haya mambo matatu siyo hasa makusudio yangu nilipoomba kuja kuzungumza
na Waheshimiwa Wabunge wetu.
Nimeyachomekea tu kwa sababu ya umuhimu wake katika jamii kwa wakati
tulio nao. Jambo lililonileta hapa leo ni
kuzungumzia hali ilivyo sasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na nafasi ya Tanzania
katika Jumuiya hiyo. Nimeona nifanye
hivyo kutokana na maswali mengi ambayo Watanzania wanajiuliza kufuatia matukio
ya hivi karibuni ya viongozi wa nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki yaani Uganda, Rwanda na Kenya kukutana bila ya ushiriki wa viongozi
wa Tanzania na Burundi. Viongozi wenzangu
hao wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe 24-25 Juni, 2013 mjini Entebbe,
Uganda; tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa, Kenya; na tarehe 28 Oktoba, 2013 mjini
Kigali, Rwanda.
Mheshimiwa Spika;
Naomba
kwanza niweke wazi jambo moja, kwamba nchi mbili wanachama au zaidi hazikatazwi
kuwa na makubaliano ya ushirikiano katika kufanya mambo mbalimbali. Hata sisi Tanzania tunao ushirikiano wa namna
hiyo na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini, nchi wanachama zinatakiwa kufanya
hivyo kwa yale mambo ambayo hayako kwenye shughuli za Jumuiya kwa maana kwamba
hayamo katika Mkataba au Itifaki au hakuna uamuzi wa msingi uliofanywa na vikao
au taasisi za Jumuiya kuyashughulikia. Pia,
tunaweza kufanya hivyo kwa mambo ambayo yalishaamuliwa na Jumuiya yatekelezwe
na ruhusa imetolewa kwa nchi yo yote iliyokuwa tayari kutekeleza ama peke yake
au kwa kushirikiana na nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika;
Kwa
mujibu wa matamko ya pamoja (Communique) yaliyotolewa baada ya mikutano hiyo, kuna
mambo yapatayo manane ya msingi
yaliyoamuliwa kufanywa na nchi hizo kwa lengo la kuendeleza utengamano wa nchi
hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mambo hayo ni haya yafuatayo:
(1)
Kujenga reli ya
kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala,
Kigali na Bujumbura.
(2)
Ujenzi wa Bomba la
Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
(3)
Kujenga Kiwanda cha
kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4)
Kuanzisha Himaya Moja
ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote;
(5)
Kuharakisha
Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya
Katiba ya Shirikisho.
(6)
Kuharakisha
uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single
East African Community Tourist Visa);
(7)
Kuandaa utaratibu wa kutumia
vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao; na
(8)
Kuongeza uzalishaji
na usambazaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika;
Ni
dhahiri kwamba orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na yale
yasiyo ya Jumuiya. Kwa mfano, mambo manne kati ya hayo manane hayamo kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha
au kupata ridhaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jambo la kwanza ni uzalishaji na usambazaji
wa umeme. Ni kweli kwamba tunao mkakati
wa kuwa na akiba ya pamoja ya nguvu ya umeme (East African Power Pool). Hata hivyo, bado jukumu la kuzalisha na
kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama zenyewe kuamua. Lakini, hivi ndugu zetu hawa wanao muhali
kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya
Afrika Mashariki ambayo sote ni wanachama?
Jambo la pili, ni
ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda. Hili si suala la Jumuiya bali la nchi ya
Uganda kuamua yenyewe peke yake au kwa kushirikiana na wadau wengine. Rais Yoweri Museveni alituarifu mpango huo na
sote tuliupokea kwa furaha kwamba sasa tutapata mafuta karibu na nyumbani. Alitualika kushiriki katika ujenzi wake
sijui sasa amebadili mawazo kwamba Tanzania siyo muhimu.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la tatu ni
ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Sudani ya Kusini na Uganda. Hili si jambo linalobanwa na masharti ya
Jumuiya. Ni juu ya nchi hizi tatu kuamua kufanya ili kuwezesha mafuta yao
kufika kwenye masoko. Hata hivyo,
nimeambiwa kuwa Jumuiya imeshazungumzia bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi
Uganda, Rwanda na Burundi kuwa nalo lifike Tanzania kupitia upande wa Kaskazini
Magharibi mwa Tanzania. Inaelekea mpango
huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika ujenzi wa bomba hilo.
Mheshimiwa Spika;
Jambo
la nne ni ujenzi
wa reli ya kisasa kutoka Mombasa – Kampala – Kigali – Bujumbura. Hili
nalo hatuna tatizo nalo. Si mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni
jambo
lililo chini ya mamlaka ya nchi wanachama husika. Hata hivyo, ni vyema
kutambua ujenzi wa
miundombinu ya reli, barabara na usafiri wa anga na majini kuunganisha
nchi za
Afrika Mashariki ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha juu
yanayoshughulikiwa
na Jumuiya yetu. Jumuiya hutengeneza
mikakati ya pamoja na ndiyo maana tuna East African Railway Masterplan,
tuna
East African Road Network, na tuna Lake Victoria Development Programme
kwa ziwa
Victoria.
Kwa ajili hiyo, nilitegemea
kuwa reli ya kutoka Mombasa hadi Kigali na Juba ingekuwa na tawi
linalounganisha reli hiyo na reli ya Tanzania kama ilivyo reli ya Moshi – Voi –
Taveta aliyotuachia mkoloni. Tulitegemea hivyo kwa minajili ya kuunganisha soko
la Afrika Mashariki ambapo naamini Tanzania ni mdau muhimu. Lakini inaelekea kwa maoni ya wenzetu hivyo
sivyo.
Mheshimiwa Spika;
Lazima nikiri kuwa inashangaza
na tunayo kila sababu ya kuuliza kwa nini wenzetu wameamua kufanya hivi. Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha
Aprili 28, 2013 na Juni 24, 2013 walipokutana kuamua kufanya mambo ya kujenga
na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kubaguana, Haijawahi kuwa hivi kabla.
Mheshimiwa Spika;
Katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa
na kuwekewa utaratibu wake wa utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili
hatuna maneno nayo. Mambo hayo ni
matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria na Visa ya Pamoja ya
Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa tayari
waanze. Lakini, kwa upande wa kuanzishwa
kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory) na Shirikisho
la Afrika Mashariki tunadhani wenzetu wamekiuka uamuzi wetu wa pamoja.
Mheshimiwa Spika;
Katika
Mkutano Maalum wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 28 Aprili,
2012 Jijini Arusha, tulipokea na kuridhia mapendekezo ya kuanzisha Himaya Moja
ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory). Kwa mujibu wa mapendekezo hayo kila nchi
mwanachama itasimamia shughuli zake za kiforodha na kukusanya mapato yake kama
ilivyo sasa. Hata hivyo, kwa bidhaa
zinazopitia nchi moja kwenda nchi nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji wa
mapato utafanyika katika kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia. Mapato hayo yatawasilishwa kwa nchi husika
baada ya kuthibitisha kuwa bidhaa zilivuka mpaka.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana
na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza la Mawaziri kuunda Kikosi Kazi
cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji wa mfumo huo. Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa kutolewa
katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 30 Novemba,
2013. Iweje leo nchi tatu wanachama ziamue
peke yao kuanza kutekeleza? Wanatekeleza
nini na kwa nini wafanye hivyo?
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu Shirikisho la Kisiasa la Afrika
Mashariki hadithi yake inafanana na hii ya Himaya ya Forodha. Katika
Mkutano wa 14 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe
30 Novemba, 2012, Nairobi, tulipokea taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusu
mchakato wa kutaka kuanzishwa kwa Shirikisho.
Mkutano huo uliagiza nchi
wanachama kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi wa kufikia Shirikisho la
Kisiasa
na mpango wa kutekeleza mapendekezo mengine yaliyotolewa na Timu ya
Wataalamu. Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri
litawasilisha mapendekezo ya majadiliano hayo katika Mkutano wa 15 wa
Wakuu wa
Nchi mwezi Novemba, 2013. Iweje leo
wenzetu hawa waamue kuanzisha mchakato wao wa kuharakisha Shirikisho la
Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Kwa
kweli huwa najiuliza maswali mengi na kukosa majibu kuhusu nini kinachoendelea kufanywa
na viongozi wenzangu watatu na kwa nini! Nakosa majibu ya uhakika. Je wenzetu wamekosa imani na Jumuiya ya
Afrika Mashariki na je wanataka kuunda yao?
Je wanaichukia nchi yetu na hivyo wameamua kutufanyia vitimbi
tutoke! Au sijui wanachuki na mimi! Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge
kuwa hatuna mpango wa kutoka (kama vijana
wasemavyo hatoki mtu hapa). Tupo na
tutaendelea kuwepo!
Mheshimiwa Spika;
Tanzania haijafanya jambo lo lote baya
dhidi ya Jumuiya au nchi yo yote mwanachama.
Na ukweli ni kwamba ni mwanachama mvumilivu, mtiifu na mwaminifu kwa
Jumuiya. Tunatimiza ipasavyo wajibu wetu
kwa Jumuiya na kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wake na utengamano ndani
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sabahu
ya wenzetu watatu kuamua kufanya mambo yahusuyo Jumuiya yetu peke yao kwa kweli
haieleweki.
Mheshimiwa Spika;
Tunasikia
eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini wengine hatupo wakasema kuwa wao
wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari tutajiunga. Yaani wana Umoja wa Waliokuwa Tayari
(Coalition of the Willing). Hivi ni nani
hayuko tayari (who is not willing?)
Haiwezekani watu waitane wenyewe bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao
ndiyo wako tayari na kujenga dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao hatuko
tayari. Madai hayo hayana ukweli. Ni vyema waseme ukweli. Kama walitualika tukakataa ndiyo wanaweza
kusema hayo.
Mheshimiwa Spika;
Kumekuwepo
na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu, eti kwamba Tanzania haina moyo wala
dhamira ya dhati ya kuendeleza utengamano
wa Afrika Mashariki. Kwa sababu hiyo inasemekana
eti nchi yetu imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba
Tanzania tunawachelewesha wengine kupiga hatua za haraka. Wanadai kama siyo hivyo Jumuiya ya Afrika
Mashariki ingekuwa mbali kwa maendeleo. Maneno hayo yamekuwa yanarudiwa au
kujirudia mara nyingi kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu wa Afrika Mashariki na
hata kwingineko duniani waamini hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Napenda
kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba madai hayo hayana ukweli wo wote. Isitoshe hata sababu zinazotolewa kuthibitisha
ukweli wake hazina mashiko. Hazifanani
na ukweli kuhusu Tanzania na Watanzania walivyo. Tanzania ni muumini wa dhati wa umoja na utengamano
wa nchi za Afrika Mashariki na Afrika.
Tumethibitisha hivyo kwa vitendo kwa kuunganisha nchi zetu mbili huru yaani
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika na kuwa taifa moja liitwalo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano
wa nchi zetu mbili ndio pekee uliodumu kwa muda mrefu kuliko yote Afrika.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki kwa maana ya kutekeleza Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa Itifaki
zake na maamuzi halali ya vikao na taasisi za Jumuiya. Kama lipo jambo ambalo hatujalifanya ilivyotakiwa
itakuwa ni kwa sababu za msingi na siyo kwa sababu ya kupuuza Jumuiya. Tunaithamini
sana Jumuiya na tumeipa kipaumbele cha juu.
Hatuwezi kuhangaika kwa gharama kubwa ya muda wetu, fedha zetu na kutoa
mchango wa hali na mali kuianzisha, kujenga na kuifikisha Jumuiya hapa ilipo
halafu tuwe ni watu tunaoongoza kutokuipenda na kudhoofisha maendeleo na ustawi
wake. Ni maneno ya kushangaza na wala hayaingii akilini. Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi.
Mheshimiwa Spika;
Nionavyo mimi msimamo wetu kuhusu
kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira, uhamiaji, pengine ndiyo yanayotuletea
hisia zisizokuwa sahihi juu yetu. Mimi
siamini kama kuna mengine. Hata hivyo,
napata taabu kuamini kwamba kutofautiana kwa mawazo katika mambo hayo
kutapelekea baadhi ya wenzetu wasipende hata kushirikiana nasi kwa mambo ambayo
hayana matatizo na tumekuwa tunashirikiana vizuri.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania
imekuwa inawasihi wanachama wenzetu kuwa tujenge Jumuiya yetu hatua moja baada
ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Hatuna tatizo la kuongeza
kasi ya ujenzi wa Jumuiya lakini tusivuke hatua yo yote. Tusiende kasi ya kupindukia. Mkataba
unaelekeza tunaanza na Umoja wa Forodha, inafuatia Soko la Pamoja kisha Umoja
wa Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Mheshimiwa Spika;
Ni
kweli kabisa hatukuunga mkono kuharakisha Shirikisho la Kisasa kabla ya
kukamilisha baadhi ya hatua. Na,
tulifanya hivyo kwa nia njema ya kutaka Shirikisho lijengwe juu ya msingi
imara. Na, msingi huo si mwingine bali
utengamano wa kiuchumi kwa maana ya Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja
wa Kifedha zilizojengeka vizuri na kufanya kazi ipasavyo na kunufaisha
wanachama wote sawia.
Mheshimiwa Spika;
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni kati ya zile nchi zinazotaka
ngazi zote za mchakato wa utengamano zitekelezwe moja baada ya nyingine bila
kuruka hata moja. Kwa msimamo na mtazamo
wetu, Shirikisho iwe ndiyo hatua ya
mwisho. Na huo siyo msimamo wangu au wa
Serikali peke yake, ndiyo msimamo wa Watanzania walio wengi.
Bila ya shaka sote tutakumbuka kuwa
mwaka 2006 Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya waliunda Kamati Maalum katika
kila nchi kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuharakisha Shirikisho la Afrika
Mashariki. Kwa hapa nchini Kamati hiyo
iliongozwa na Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa yake, Kamati ilieleza kuwa asilimia 74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho
lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo waliunga mkono
kuharakishwa kwake.
Mheshimiwa Spika;
Takwimu hizi zinaelezea ukweli kuhusu
hisia za Watanzania, kuhusu kuwepo kwa Shirikisho na kasi ya utekelezaji
wake. Watanzania wengi sana wanaunga
mkono kuwepo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki lakini wanataka jambo hilo lisifanywe
haraka haraka. Wanataka lifanywe kwa
umakini mkubwa na tuende hatua kwa hatua kama ilivyoainishwa katika Mkataba
uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Sera na msimamo wa Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inakwenda sambamba na ile ya wananchi wa Tanzania. Ndiyo maana tumeafiki mapendekezo ya Kamati ile
ya mwaka 2004 iliyoongozwa na
Mheshimiwa Amos Wako wakati ule akiwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya. Kamati hiyo iliundwa kupendekeza namna ya
kuharakisha utekelezaji wa mchakato wa utengamano wa Afrika Mashariki.
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
umetamka muda wa kutekeleza ngazi ya Umoja wa Forodha lakini uko kimya kuhusu
ngazi zilizofuata. Ili kuondoa kasoro
hiyo na kwa nia ya kuharakisha Shirikisho Kamati ilipewa jukumu la kutoa maoni
na mapendekezo juu ya namna ya kufanya hivyo.
Kamati ilifanya kazi nzuri ya kupata maoni na hisia za watu wa makundi
mbalimbali katika nchi wanachama kuhusu ujenzi wa Jumuiya na utengamano.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Tanzania kwa mfano,
Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako ilitambua hisia za Watanzania kuhusu ardhi na
ajira na kupendekezwa kuwa masuala hayo yabaki kwenye mamlaka ya nchi wanachama
kuamua. Kuhusu mchakato wa utengamano Kamati
ilipendekeza kwanza kwamba mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Forodha uachwe mpaka
ufike ukomo wake wa miaka mitano. Baada
ya hapo muda wa kutekelezwa ngazi zinazofuata unaweza kupunguzwa. Kwa mfano walipendekeza kuwa matayarisho ya
kuunda Soko la Pamoja yaanze hata kabla ya mchakato wa Umoja wa Forodha kufika
mwisho ili mara wakati huo ukifikiwa Soko la Pamoja linaanze. Hivyo hivyo mara baada ya ngazi hiyo kuanza
matayarisho ya kuanza ngazi ya Umoja wa Kifedha yanaanza. Ngazi hiyo nayo ikianza matayarisho ya kuunda
Shirikisho yanaanza. Kamati pia imetoa
mapendekezo ya namna ya kufikia uamuzi kuhusu Shirikisho kwamba wananchi wa
nchi wanachama wataamua kwa kura.
Tukifuata mapendekezo ya Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako na wenzake kama
tufanyavyo sasa Tanzania haina matatizo nayo.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya kazi kubwa na nzuri
iliyofanywa na wana-Afrika Mashariki kuhusu ujenzi wa Jumuiya yao inasikitisha
kuona vinafanyika vitendo vinavyoanzisha mivutano kuhusu mambo yaliyokwisha fanyiwa
kazi na kuamuliwa. Tunapata taabu zaidi
pale watu wanapobagua wenzao na wanapofanya mambo yanayopingana na Mkataba wa
Jumuiya na Itifaki zake. Kwa kweli kama
mwenendo huu hautabadilika sijui mambo yatakuwaje mbele ya safari.
Mheshimiwa Spika;
Nchi
yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyo imara na
iliyo endelevu. Jumuiya ambayo
inaendeshwa vizuri, mambo yake ni mazuri na nchi zote wanachama na watu wake
wananufaika nayo, na hivyo wanaifurahia.
Tanzania haina tatizo na kuharakisha mchakato wa utengamano, lakini
tunapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla hazijakamilika. Tunawaomba wenzetu kuwa makini katika kila
hatua tunayochukua. Bila ya kufanya
hivyo, Jumuiya yetu itakuwa imejengeka
katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa na changamoto
nyingi. Hatupendi ya mwaka 1977 yatokee
tena.
Mheshimiwa Spika;
Napenda
kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli za Jumuiya ya
Afrika Mashariki na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kuzingatia
matakwa ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki zake. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa Jumuiya
haidhoofiki wala kufa. Na iwapo
itadhoofika au kufa kamwe hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo
chake. Ndiyo maana, hatutachoka
kuzungumza na wenzetu kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki
inaendelea kustawi.
Tutaendelea
kukumbushana umuhimu wa kufanya mambo yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza
kubomoa. Tutakumbushana umuhimu wa
kuheshimu matakwa na masharti ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na
maamuzi halali ya vikao rasmi na asasi za Jumuiya. Tukifanya hivyo Jumuiya ya Afrika ya
Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi wanachama na watu wake
kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa kwake.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Idumu Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika na
Waheshimiwa Wabunge;
Asanteni sana kwa
kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment