Ewe Kijana Mwenzangu baada ya kueleza Maana ya Najisi ki lugha na Mtazamo wa Watu wa Fani ya Sharia leo Inshallah Tunaendelea kwa kuangalia Aina za Najisi na Jinsi ya Kutwaharika (Safika) na hizo Najisi.
AINA ZA NAJISI NA JINSI YA KUZIONDOSHA KWAKE .
Najisi kwa mtazamo wa sharia zimegawanywa katika aina tatu
1. NAJISI NZITO
Hii ni najisi ya mbwa na nguruwe na mnyama aliyezaliwa kutokana nao au mmoja wao (mbwa na nguruwe).
Najisi hii imeitwa najisi nzito kutokana na uzito unaompata mtu katika kuiondosha
NAMNA YA KUONDOSHA NAJISI HII.
Hutwaharishwa(husafishwa) mahala palipoingiwa na najisi ya mbwa na nguruwe kwa kupaosha mahala hapo palipo najisika kwa kupaosha mara saba na mojawapo ya mara saba hizo iwe kwa kusugua na mchanga.
Bwana Mtume Rehma za M/Mungu zimshukie juu yake na amani amesema :
"Twahara ya chombo cha mmoja wenu atakapokiramba mbwa ni kukiosha mara saba, Moja katika Mara saba hizo iwe kwa mchanga" kama alivyosema Mtume
Muslim
2. NAJISI HAFIFU
Hii ni mkojo wa mtoto mchanga wa kiume aliye chini ya miaka miwili na chakula chake mtoto huyu ni maziwa ya mama tu.
Najisi hii imeitwa Najisi hafifu kwa sababu ya wepesi unaopatikana katika uiondosha.
NAMNA YA KUONDOSHA NAJISI HII.
Hutwaharishwa mahala paliponajisika kwa kuingiwa/kupatwa na najisi hafifu kwa kuimwagia maji sehemu hiyo yanatakiwa maji yaenee katika sehemu hiyo iliyopatwa na Najisi.
3. NAJISI YA KATI NA KATI
Hii imekusanya baki ya najisi nyingine ukiondoa najisi ya mbwa na nguruwe na mkojo wa mtoto mchanga wa kiume.
Najisi hii imeitwa Najisi ya kati na kati kwa kuwa haiko kwenye uzito na wala haikufika kwenye uhafifu.
NAMNA YA KUONDOSHA NAJISI HII.
Najisi ya kati na kati, mahala paliponajisika kwa kuingiwa na najisi hii hutwaharishwa kwa kupaosha na maji twahara mpaka iondoke rangi, utamu na harufu ya najisi hiyo. Haidhuru kubakia kimojawapo rangi au harufu ziloshindikana kuondoka.
TANBIHI : ANGALIZO
Usiitumbukize nguo iliyonajisika ndani ya maji machache kama vile ndoo ukadhani kuwa umeitwahirisha bali itakuwa bado imenajisika na kunajisisha maji yote na hivyo kuyafanya yasifae tena kutwahirishia. Unachopaswa kufanya ni kutumia kata au kilicho mfano wa kata, uteke maji na kuitwahirishia nguo hiyo pembeni ambapo maji yanayochuruzika kutoka katika nguo iliyonajisika hayaingii tena chomboni.
Mpaka hapo Ndugu kijana Mwenzangu natumai utakuwa Umepata Muangaza fulani katika Ukumbusho huu na Post zetu nyuma zilizopita Ndugu zangu Tusaidiane katika kheri ikiwa sehemu kuna Makosa Inshallah Tuzinduane Inbox na tutarekebisha Tukumbuke kuwa Mkamilifu Daima ni M/Mungu na Mimi Ni Kijana Mwenzenu na Binaadamu kama sehemu iko Kosa tujulishane M/Mungu ndio Mjuzi zaidi
No comments:
Post a Comment