Monday, June 04, 2012

MAANA YA TWAHARA



Ewe Kijana Mwenzangu kama Tulivyosema kwamba Inshallah Ukumbusho unaokuja utahusu TWAHARA ( Usafi ) Leo tena tuko na Mwanzo wa safari yetu ya kukumbushana Nini Twahara Ubora wake Falsafa ya Twahara na Makusudio yake na tutasimama katika vitu ambavyo kwa vitu hivyo unaweza ukajitwaharisha (Safisha).
Tuanze safari yetu na Maana ya Twahara Kilugha na Kimtazamo wa Sheria (Istillah )

1. MAANA YA TWAHARA
Twahara katika lugha ya Kiarabu ina maana ya unadhifu na kujilinda na kila kilicho kichafu.

Kwa Mtazamo wa sheria twahara ni kuondosha
1. Hadathi
2. Kuondosha najisi.

1.HADATHI
Hadathi ni hali inayomzuilia mtu kufanya ibada kama vile swala na hali hii huondoka kwa kutawadha ikiwa hadathi ni ndogo, na kwa kuoga ikiwa hadathi ni kubwa kama Vile Janaba N.k.

2.NAJISI
Najisi ni kama vile damu, usaha, matapishi, choo kikubwa na kidogo, mbwa, nguruwe N.k.

UBORA WA TWAHARA

Mwenyezi Mungu Mtukufu amewasifia sana waja wake wanapenda kujitwaharisha na kujitakasa ndani ya Qur-ani aliposema: " Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao tubu na huwapenda wanao jisafisha". (2:222) Suratil Baqarah

Utaona kutokana na aya hii kwamba twahara ni sababu ya kuyavuna mapenzi ya Mola Mwenyezi.
Mwenyezi Mungu anazidi kutuonyesha ubora wa twahara kwa kusema:
"Msikiti ulio jengwa juu ya msingi wa ucha mungu tangu siku ya mwanzo unastahiki zaidi wewe usimame ndani yake. Humo wamo watu wanao penda kujitakasa. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wanao jitakasa.". (9:108) Surat At Tawbah

FALSAFA YA TWAHARA NA MAKUSUDIO YAKE

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameifanya twahara kuwa ni sheria na kuwafaradhishia waja wake kwa sababu Twahara humfanya muislam aishi maisha ya unadhifu (usafi) na utakasifu.
Humfanya awe mtakasifu wa mwili, nadhifu wa mavazi na mahala aishipo. Utakasifu na unadhifu huu humjengea afya njema na mwenendo mzuri kitabia. Usafi huu wa nje/dhahiri ni barabara na chombo cha kumfikisha katika usafi na utakasifu wa ndani/batini ambao humfanya kuwa ni mtakasifu wa moyo, mwenye kauli nzuri laini na nafsi iliyosalimika na husuda, udanganyifu na tabia mbaya zote kwa ujumla.
Muislamu wa kweli ni yule aliyetakasika nje na ndani wakati wote hasa hasa wakati wa kutekeleza ibada, hii ndio sababu Bwana Mtume akatuambia: "Uislamu ni nadhifu(Usafi), basi jisafisheni kwani hatoingia peponi ila aliye nadhifu (Msafi)". Kama alivyosema Mtume Rehma za M/Mungu zimshukie Juu yake na Amani.

VYA KUJITWAHARISHIA (VITU AMBAVYO TUNATUMIA KUWA SAFI )
Vitu vitumikavyo katika Twahara ni hivi vinne
1. Maji
2. Mchanga
3. Dab-gh (ni njia/utaratibu utumikao katika kuitwaharisha ngozi ya mnyama ili iweze kufaa kutumika katika matumizi mbalimbali ya binadamu)
4. Mawe.
Hapo Inshallah tutasimama kwa leo Ewe Ndugu kijana Mwenzangu na Inshallah M/Mungu akipenda tutaendelea katika Uchambuzi hivi vitu vinne ambavyo kupitia hivyo ndio utunaupata huo Usafi au Twahara Ndugu yenu katika Imani

No comments:

Post a Comment