Ewe Kijana wa Kiislam Baada ya kumaliza Ukumbusho wa Twahara kwakueleza
Maana yake Ki Lugha na Sharia,Vitu ambavyo kwa vitu hivyo tunajitwaharisha
Aina za Maji ambayo tunaweza Tujitwaharisha,Vigawanyo vya MAJI na Hukumu zake
na Mwisho wetu tulisimama katika Mgawanyo wa Maji kwa kuzingatia uchache wake na WINGI wake
Leo Tunaendelea na Safari yetu ya kukumbushana kwa kuangalia.
NAJISI
1.MAANA YA NAJISI
2.WAJIBU WA KUJITWAHARISHA KUTOKANA NA NAJISI
3. VITU VILIVYO NAJISI
Ushauri kwa Marafiki zangu wageni kurejea Post za Nyuma ili tupate kwenda sawa katika
Safari yetu hii Inshallah tunaanza na Maana ya Najisi.
1.MAANA YA NAJISI
Najisi ni neno la kiarabu lenye maana mbili; maana ya kilugha
na ya kisharia.
Najisi katika lugha ni kila kilicho kibaya
hata kama ni twahara Mf makamasi, makohozi N.k Maana hii ya najisi kilugha
tunaipata katika kauli ya Mola anaposema :
"ENYI MLIOAMINI ! HAKIKA WASHIRIKINA NI NAJISI …." [9:28]
Sote tunakubaliana kwa dalili zote;
dalili nakala na dalili akili kwamba binadamu yeyote ni
kiumbe twahara lakini utaona kwenye aya hii Mola Mtukufu
anawaita washirikina kuwa ni NAJISI kwa sababu ya ubaya na uchafu wa nafsi zao
katika katika kumshirikisha MwenyeziMungu na viumbe alivoviumba mwenyewe.
Neno NAJISI katika Maana ya sharia ni kila kitu kichafu ambacho kinazuia kusihi kwa
ibada kama vile swala, kutufu (twawafu) N.k.
2.WAJIBU WA KUJITWAHARISHA KUTOKANA NA NAJISI
Imempasa na kumuwajibikia mwislamu kuutwahirisha mwili,
nguo, mahala/sehemu alipo na mazingira yake kwa ujumla
kutokana na kila kilicho najisi kwa maana zote mbili kwani
hiyo ni amri ya MwenyeziMungu alipomwambia Mtume wake bali umma mzima :
"NA NGUO ZAKO UZISAFISHE" [74:4]
MwenyeziMungu pia amewasifia waja wake ambao hujitahidi katika suala la
usafi na kujiepusha/kujilinda na najisi aliposema
"HAKIKA ALLAH HUWAPENDA WANAOTUBU NA HUWAPENDA WANAOJITAKASA" [2:22]
Katika kulisisitiza na kulitilia mkazo suala la twahara na kujiepusha na najisi
Bwana Mtume anatuambia :
"Twahara ni nusu ya imani"
Kadhalika Bwana Mtume amewaagiza na kuwaamrisha wanawake
kujitwaharaisha kutokana na damu ya hedhi kama alivyotuamrisha sote
kuondosha kila najisi.
3. VITU VILIVYO NAJISI
1.Mfu/Mzoga ila mwanadamu, samaki na nzige.
2.Kiungo cha mnyama kilichokatwa naye yu hai.
Amesema Bwana Mtume : "Kilichokatwa kwa mnyama na ilhali yu hai hicho (kilichokatwa)
ni mzoga" Abu Dawud.
3.Damu,
4.mkojo,
5.kinyesi (mavi) ya wanadamu, wanyama au ndege.
6.Nguruwe ! MwenyeziMungu anatuambia :
"SEMA SIONI KATIKA YALE NILIYOFUNULIWA MIMI KITU KILICHOHARIMISHWA
KWA MLAJI KUKILA ISIPOKUWA KIWE NI MZOGA AU DAMU INAYOMWAGIKA AU NYAMA YA
NGURUWE KWANI HIYO NI UCHAFU …" [6:145]
7.Mbwa kwa ushahidi wa hadithi isemayo "Mbwa atakaporamba chombo cha mmoja wenu basi
na akimwage (kilichomo ndani) kishe akikoshe (chombo) mara saba"
8.Matapishi,
9.usaha,
10.maji ya madonda
11.Wadii na Madhii.
Wadii ni maji mazito yatokayo baada ya mkojo kutokana na kazi ngumu/nzito.
Madhii ni maji meupe yanayoteleza, haya hutoka wakati wa matamanio khafifu
(kwa mfano kuchezeana baina ya mwanaume na mwanamke).
Matamanio yakiwa ya nguvu ndio hutoka manii.
12.Tembo/Pombe kwa aina zake zote. MwenyeziMungu anasema :
"ENYI MLIOAMINI ! BILA SHAKA ULEVI NA KAMARI NA KUABUDIWA ASIYEKUWA ALLAH NA
KUTAZAMIA KWA MSHARE YA KUPIGIA RAMLI (na kwa vinginevyo, yote haya) NI UCHAFU
UTOKANAO NA KAZI YA SHETANI. BASI JIEPUSHENI NAVYO ILI MPATE KUFAULU" [5:90]
Maziwa ya mnyama asiyeliwa.
Mpaka hapo Ndugu kijana Mwenzangu tutakuwa tumejua nini Maana ya Najisi na wajibu wa Kuziondosha
Hizo na Najisi pamoja na Vitu vilivyo Najisi Inshallah Ukumbusho ujao tuona Aina za Najisi
na Jinsi ya kuziondosha.
katika pombe ni najsi au si najsi kuna khitilafu za wanawavyuoni,,
ReplyDelete