Tuesday, June 05, 2012

SUNNA ZA UDHU


SUNNA ZA UDHU
Maana ya sunna katika elimu ya Fiqh ni NJIA iliyopokewa kutoka kwa Mtume kwa maneno au vitendo.

Sunna kifiqh zimegawanyika sehemu mbili

1.Suna Muakkadah (Suna kokotezwa)
2.zisizo Muakkadah (Suna zisizokokotezwa)

Suna Muakkadah
Ni zile alizodumu nazo Bwana Mtume (S.A.W) kuzitenda na hakuziacha ila kwa udhuru
mkubwa sana.

Hukumu yake
Hukumu ya suna muakkadah ni kulipwa thawabu mtendaji na kulaumiwa na sheria mwenye kuacha kuitenda.

Sunna zisizo muakkadah
Ni zile ambazo Bwana Mtume(S.A.W) alizitenda baadhi ya wakati na kuziacha wakati
mwingine.

Hukumu yake.
Hukumu ya suna hii ni kulipwa thawabu mtendaji na wala haadhibiwi mwenye kuacha
kuzitenda.

Sunna zisizo Muakkadah huitwa Majina Mengine MANDUBU au MUSTAHABBU.

SUNNA ZA UDHU.

1.Kupiga Bismillah mwanzoni mwa kutawadha. Imepokelewa kutoka kwa Swahaba Anas Mtume (S.A.W) amesema "Tawadheni kwa BISMILLAH" yaani semeni hivyo mnapoanza kutawadha kama alivyosema Mtume. Nasaai

2.Kukosha vitanga vya mikono kabla ya kuviingiza chomboni ikiwa anatawadha kwa kutumia chombo mfano wa kopo.

3.Kupiga Mswaki :
Hili linatokana na kauli ya Bwana Mtume (S.A.w) Lau si kuwaonea uzito umati wangu,
ningeliwaamrisha kupiga mswaki pamoja na kila udhu" kama alivyosema Mtume Bukhar na Muslim.

4 na 5.
Kusukutua na kupandisha maji puani kwa kutumia mkono wa kulia na kisha kumeka kwa kutumia mkono wa kushoto.

6.Kuasua ndevu nyingi, yaani kuzichokoa ili maji yaweze kupenya ndani ya ngozi.

7.Kupaka maji kichwa chote/kizima.

8.Kusafisha sehemu zilizo baina ya vidole vya mikono na miguu.

9.Kupakaza masikio maji, nje na ndani kwa majimapya sio yale yaliyotumika katika kupakaza kichwa.

10.Kuosha na kupakaza maji viungo mara tatu tatu.

11.Kuanza kuosha mkono/mguu wa kulia kabla ya mkono/mguu wa kushoto.

12.Kusugua, huku ni kupitisha mkono juu ya kiungo wakati wa kukiosha.

13.Kufululiza, yaani kuviosha viungo kwa kufuatanisha kimoja baada ya kingine pasi na
kutia mwanya kati yake, kiasi cha kutokauka kiungo cha mwanzo kabla ya kuoshwa kiungo cha pili. Kufanya hivi ni kumfuata Bwana Mtume, kwani hivi ndivyo alivotawadha.

14.Kurefusha kuosha mipaka/sehemu za uso, mikono na miguu.

15.Kutofanya israfu katika utumiaji wa maji,ikawa mtu anayamwaga majo ovyo ovyo. Ni muhimu tukakumbuka kwamba maji ni miongoni mwa neema kubwa kabisa alizoneemeshwa nazo binadamu, kwani maji ni uhai. Kwa mantiki
hii ni vema tukayatumia kwa uangalifu, ikiwa ni pamoja na kuvihifadhi vyanzo vya
maji.Tujiepushe na matumizi mabaya ya maji katika kila shughuli/kazi za maisha yetu ya kila siku, hasa hasa katika kutawadha na kukoga.

16.Kuelekea Qiblah wakati wa kutawadha kwani huo ndio upande mtukufu kuliko pande zote.

17.Kutokuzungumza wakati wa kutawadha. Haya yote ni kumfuata Bwana Mtume (S.A.W)

18.Kuomba/Kuleta dua hii baada ya kumaliza kutawadha, elekea Qiblah na sema :
DUA BAADA YA UDHU.
(ASH-HADU AN LAA ILAAHA ILLAL-LAAHU WAHDAHU LAA SHARIYKA LAHUU, WA ASH-HADU ANNA MUHAMMADAN ‘ABDUHUU WARASUULUH, ALLAHUMMA JA3LNIY MINAT-TAWWABIYNA, WAJA3LNIY MINAL-MUTATWAHHIRIYN, WAJA3LNIY MIN ‘IBAADIKASWAALIHIYN, SUBHAANAKALLAHUMMA WABIHAMDIKA, ASH-HADU AN-LAA ILAAHA ILLA ANTA ASTAGHFIRUKA WA ATUUBU ILAYKA).

Hapa Inshallah Tutakuwa tumefikia Mwisho wa Mlango wa Sunna Tunamuomba M/Mungu atudumishe katika kufuata Faradhi zake na kushikamana na Sunna Za Mtume (S.A.W) ili kupata Radhi za M/Mungu Ewe Mungu Tusaidie waja wako

No comments:

Post a Comment