Nguzo za Udhu
Kusudio la neno Nguzo hapa ni yale mambo ambayo ni lazima kupatikana ili kutimia UDHU wako likikosekana au kupungua moja miongoni mwao, udhu huwa ni batili kisharia.Zifuatazo Ndio Nguzo za Udhu kwa Utaratibu Kama tulivyoelekezwa katika Qur an na kufasiriwa na Mtume Muhammad (S.A.W)
Nguzo za Udhu ziko Sita 6.
1.NIA
Hii ndio nguzo ya kwanza ya udhu.
Neno “nia” Maana yake katika lugha ya kawaida ni MAKUSUDIO.
Ama katika Sharia na watu wa Fiqh ni MAKUSUDIO YA KITU/JAMBO HALI YA KUAMBATANISHA KITU/JAMBO HILO NA KITENDO CHAKE.
na Nia hukaa moyoni mwa mtu. Dalili ya ufaradhi nia Hadith ya Mtume (S.A.W) “Hakika (kusihi kwa) amali kumefungamana na nia na kila mtu (atalipwa) kwa mujibu wa nia (yake).." Kama alivyosema Mtume Hadith imepokewa na Imam Bukhar na Muslim
Malengo ya Nia katika Udhu.
Ni kupambanua baina ya ibada na ada na Udhu ni Ibada .Mfano mwengine wa kumbanua kati ya Ada na Ibada Mfano wa Kukoga kuna kukoga kwa kujisafisha na kukoga kwa Ajili ya kuondosha Josho kubwa Sasa Nia ndio itakayo tofautisha kati ya Mawili hayo Ada au Ibada.Basi kwa mantiki hii ikawa ni lazima udhu uambatane na nia.
Namna ya nia ni mtu kusema moyoni mwake :
“Nawaytu Fardhal-udhui” au
“Nawaytu Raf-al Hadath” au
“Nawaytu istibahat-swalaat”
Muda wa Kuleta Nia katika Udhu.
Nia huletwa wakati wa kuosha fungu/sehemu ya mwanzo ya uso, kwa kuwa hapo ndio mwanzo wa udhu yaani udhu unaanzia hapo na yaletwayo kabla ya hapo huhesabika kama maandalizi ya kuingia ndani ya udhu.
2.Nguzo ya Pili katika Nguzo za Udhu KUOSHA USO MZIMA/WOTE
Dalili kauli ya M/Mungu Mtukufu “BASI OSHENI NYUSO ZENU …”Qur an Suratil Maidah Aya ya 6
Kuosha uso mzima ndio nguzo ya pili ya udhu. Uso huoshwa mara moja tu kwa kuitegemea kauli ya Mtume : “Udhu ni mara moja moja”. Ama kule kuosha mara ya pili na ya tatu ni sunna. Imethibiti riwaya kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu –Rehema na Amani zimshukie – alitawadha mara moja moja na akasema : “Huu ndio udhu ambao Allah haikubali swala ila kwao” Na akatawadha (tena) mara mbili mbili na akasema : “Huu ndio wa wa mtu ambaye Allah atampa ujira mara mbili” Na akatawadha (tena) mara tatu tatu na akasema : “Huu ndio udhu wangu na udhu wa mitume kabla yangu, basi atakayezidisha (zaidi ya) hivi au kupunguza, (huyo atakuwa) amechupa mipaka na kufanya dhuluma”
Mipaka ya Uso
Uso katika Udhu huanzia maoteo/mameleo ya nywele za kichwa mpaka chini ya kidevu, huo ni urefu Upana wake ni tokea ndewe moja ya sikio hadi nyingine. Eneo lote lililo katika mipaka hiyo, ndio huitwa uso katika sharia. Na ni wajibu kuosha kila kilichoota ndani ya mipaka hiyo kama nyusi, kope, sharubu na ndevu.
Ndevu huoshwa nje na ndani zikiwa chache. Ama zikiwa ni nyingi zilizoshindamana kiasi cha kutokuona ngozi basi inatosha kuosha juu yake tu.
3.KUOSHA MIKONO HADI VIFUNDONI
Imelazimu maji yaenee vema katika nywele na ngozi. Ukiwepo uchafu chini ya kucha ukayazuiliya maji kupenya ndani au pete iliyobana isiyoruhusu kupenya maji, udhu hautasihi bali utakuwa ni batili.
4.KUPAKAZA MAJI SEHEMU YA KICHWA
Jinsi Mtume alivyokuwa akipaka za Kichwa imepokelewa na Abdallah ibn Zayd Mtume (S.A.W) Alipakaza (maji) kichwa chake kwa mikono yake, akaipeleka mbele halafu akairudisha nyuma, alianzia sehemu ya mbele ya kichwa chake kisha akaipeleka kichogoni, kisha akairudisha pale mahala alipoanzia”
5.KUOSHA MGUU HADI VIFUNDONI
Inampasa mwenye kutawadha ahakikishe anaosha sehemu yote iliyoainishwa katika sheria. Asiache sehemu yeyote ile iliyo chini ya kucha.
6.MPANGO/TARATIBU.
Kufuatilizisha baina ya viungo hivi vinne vya udhu kwa namna ilivyokuja ndani ya Qur-ani Tukufu.
Na dalili ya Nguzo hii ya Sita inapatikana katika Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema katika Qur an : “ENYI MLIOAMINI! MNAPOTAKA KUSWALI, BASI OSHENI NYUSO ZENU NA MIKONO YENU MPAKA VIFUNDONI, NA MPAKE (maji) VICHWA VYENU, NA (osheni) MIGUU YENU MPAKA VIFUNDONI”Qur an Surat Maidah Aya ya 6.
Ewe Ndugu yangu katika Imani haya Mambo sita NDIO Nguzo za Udhu.
Inshallah tuwe makini sana katika kuchukua kwetu Udhu kwani Tukumbuke kwamba kubatilika kwa Udhu kunapelekea kubatilika Swala kwakuwa Udhu Ndio Msingi kuu wa Swala
No comments:
Post a Comment