Tuesday, July 30, 2013

BADO NATAFARI KAULI HII NITAKUJA NA FIKRA " Onyo la Mufti Simba".

Mufti Simba amesema viongozi wa dini wanaotumiwa na viongozi wa siasa kuzitumia nyumba za ibada kufanya siasa wamefilisika kiimani na wanaendekeza njaa.

Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam katika hafla ya kufuturisha, iliyoandaliwa na familia ya Mwenyekiti wa Taasisi ya Kiislamu ya Imamu Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais mstaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi.

Mufti Simba alisema maimamu wanatakiwa kutambua kuwa misikiti ni tiba ya kiroho, hivyo si vema kuwaruhusu wanasiasa kujitakasa na kujenga makundi kwa waumini wenyewe kwa wenyewe.

Alisema kunahitajika kuwa na amani katika nyumba za ibada hivyo Waislamu wana wajibu wa kulinda dini yao, si kuingia misikitini na kutoa mada zinaloleta shida na migawanyiko kwenye jamii.

“Kama wewe ni mwanasiasa nenda huko bungeni ndiko eneo lako, misikitini si eneo la siasa, msiingie na kuanza kutoa maneno ya kujitakasa. Unaizungumza Bakwata vibaya kwakuwa unataka uiteke, wewe nani? Nenda zako bungeni kafanye hiyo siasa yako,” alisema Mufti Simba.

Mufti alisema kutokana na fujo za mara kwa mara na kuvunjika kwa amani misikitini kutasambazwa waraka maalumu kwa ajili ya kuanzisha kamati za ulinzi misikitini ili kudhibiti fujo hizo zinazotokea kwa mgongo wa dini.

Alisema waraka huo unatokana na kongamano la amani lililofanyika kati ya viongozi wa dini na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema, kwa ajili ya kudhibiti matukio mabaya misikitini yanayoashiria uvunjifu wa amani.

Alisema kwa sasa kila msikiti utakuwa na kamati ya ulinzi na kama kutakuwa na yeyote anayefikiria ama kufanya vurugu atadhibitiwa na kukamatwa kama mhalifu wa makosa ya jinai na atashitakiwa kama watuhumiwa wengine.

Naye Sheikh Khalifa aliwashukuru wananchi mbalimbali na masheikh kwa kujumuika nao lakini alisisitiza kuwa katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu ujao maimamu wanatakiwa kujitambua na kuacha kutumika kwa wanasiasa waliofilisika.

Alisema ni aibu kwa kiongozi wa dini kufikia hatua ya kuwa na mgombea wake msikitini, hivyo kuwagawa waumini wake wasiomtaka mgombea husika.

“Katika chaguzi mbalimbali hali imekuwa mbaya, kwa kuwa chaguzi sasa zimegeuka pesa, mtu anatoa pesa zake na kuwatumia viongozi wa dini, hali hii haitavumiliwa kabisa, utakuta wanasiasa mufilisi wanatoa fedha na viwanja kwa ajili ya kujineemesha wao wenyewe,” alisema Sheikh Khalifa.

Naye Rais mstaafu Mwinyi, aliwashukuru watu wote waliohudhuria futari hiyo huku akisisitiza umoja, amani na utuvuli ambavyo vinawafanya watu waishi na kufanya shughuli zao bila hofu yoyote.

BADO NATAFARI KAULI HII NA NITAKUJA NA FIKRA ...

WAISLAMU WENYEWE KWA WENYEWE TUNAMALIZANA KAULI YAKE NZURI LAKINI PAANGALIWE UPANDE WA PILI JEE WAKITUMIA NYUMBA ZAO SISI TUFANYEJE ?

No comments:

Post a Comment