Al-Habib Ali Bin Muhammad Al-Habshy, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie.
Nimekuwa nikijuiza kwanini linaponijia jina la Shaykh Nurdiin bin Hussain bin Mahmoud Al-Ghassany, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie, huwa ni kope kwa nyusi na jina la al-Habib Ali bin Muhammad bin Hussain al-Habshy, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie? Ewa. Sasa naona.
Shaykh Nurdiin alikuwa ni Shaykh wa tarika ya Shadhilly kama Sayyidina Ibn ‘Atwaai-Llah as-Sakandari, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie, alivyokuwa Shaykh wa Shadhilly. Jina lake jingine Bwana huyo ni al-Imam, al-‘Arif bi-Llah Ahmad bin Muhammad bin Abdulkarim. Kuna mengine yanayowaunganisha hawa watatu. Lakini hayo si ya leo. La leo ni kwamba Sayyidina Ibn ‘Atwaai-Llah ash-Shadhilly ni tarika moja na Shaykh Nurdiin bin Hussain. Aliandika kitabu juu a Shaykh wake al-Imam Abi-l-‘Abbas Ahmad bin Umar al-Mursii, radhi za Mweneyzi Mungu zimwalie.
Wasifu anaoutoa kumfafanua Shaykh wake ni karibu wasifu ule ule anayeutoa al-Imam, Shaykh Abdallah bin Muhammad bin Salim Baakathir, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie, kumfafanua Shaykh wa Shaykh wake, al-Habib Ali bin Muhammad bin Hussain al-Habshy. Yale ambayo Mwenyezi Mungu kamfungulia Ibn ‘Atwaai-Llah kuyaona kwa Shaykh wake Abi-l-‘Abbas al-Mursii ni yale yale ambayo Mwenyezi Mungu kamfungulia Shaykh Abdallah Baakathir kuyaona kwa Shaykh wa Shaykh wake, Habib Ali al-Habshy,
jamali ya kupigiwa mfano, jalali isoweza kuchanganyishiwa macho, ilmu
zenye kuduwaza akili na akhlaqi za juu na rehema na shafaka kubwa juu a
umma wa Mtume, swalla-Llahu aalay wa Ssalaam.
Ni kwa Habib Ali al-Habshy basi ndiyo kwenye ukurasa wa leo tunakwenda kumsikiliza, atufahamishe yale makuu ya Laylatul-Qadr.
بِسْمِ اللهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيم
Himdi
zote zinamhakia Mwenyezi Mungu ambaye liko juu neno Lake na hoja Yake
ndiyo mwisho wa hoja, Mola ambaye ni ya wasaa Rehema Yake, na Neema Yake
ni yenye kukunjuliwa juu ya viumbe wote, Mwenye kulingania waja kwenye
tawhidi Yake. Wakamjibu
wale waja Wake waliopewa tawfiqi. Na akawaita kwenye twaa Yake. Na
wakafanya haraka kuitikia wito huo, wale walio halisi kwenye mapenzi
Yake, na watashi wa kweli wa pendo Lake.
Kazifanya
neema namna namna na kajalia wakati maalum wa kudhihiri athai za neema
hizo kwenye wujudi. Kwa hivyo hakuna zama zezote zile isipokuwa Mwenyezi
Mungu anayo mumo siri kubwa ambayo hushuka kwa mujibu wa takdiri Yake
na wakati alioiwekea.
Na
kautukuza mwezi wa Ramadhani juu ya miezi mingine kwa mambo makhsusi na
akashusha humo Qur’ani, uongofu mkubwa kwa watu na ubainifu mkuu.
Ikadhihiri siri hiyo kwenye mawahibu yenye kushuka kwenye zama hizi
tukufu, kulingana na kushushwa Qur’ani humo kutoka hadhra ya Mola yenye
kubainisha taklifu za ibada na kuzifafanua. Ni Yeye basi Subhannak
– Aliye takata na mawii, Mfalme alioje, Aliye unganisha sababu na
matokeo yake. Tena akazipitisha aqdari kama alivyosajili kwenye Mama wa Vitabu.
Na nakiri kwa moyo na kubaini kwa ulimi kwamba hakuna mwabudiwa wa haki
isipokuwa Mwenyezi Mungu, Mfalme ambaye wamenyenyekea kwa utisho wake
wafalme, na Karimu ambaye enga enga Yake imemvaa anayejiweza na yule
asio kitu. Na nakiri kwa moyo na kubaini kwa ulimi kwamba Bwana wetu
Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake na mpenzi Wake, ambaye iqbali Yake
kwake na kabuli Yake ni jambo lililo hakikishwa, Mwenyezi Mungu amswaliye na amsalimiye, na amzidishie sharafu na ikramu mbele Yake, azihusishe swala hizo tukufu na taslima zilizo latifu kwa Aali zake watukufu, na ma-Swahaba zake wajuzi, na wale waliosimama kwenye njia yao iliyonyooka.
Enyi
waja wa Mwenyezi Mungu nakusieni nyinyi na nafsi yangu kwa taqwa ya
Mwenyezi Mungu. Mwenye sada na sudi njema kweli ni yule mwenye
kutekeleza ahkami Zake na akajikunjulia nje na ndani alama Zake tukufu.
Na hizo, tutanabahi na tujue, ni kutekeleza yale ambayo Mwenyezi Mungu
kaamrisha na kukatazika na yale ambayo kayakataza na kayakataza kwa
ukali.
Basi
kwa umri wangu, hiyo ndiyo njia yenye kumfikisha mtu kwenye radhi za
Mwenyezi Mungu na njia iliyokusanya namna zote za mema na atiyya zake
kocho kocho. Basi yule mwenye kuwajibika nayo itamkusanya yeye chanda
kwa pete kwenye kheri za Dunia na Akhera na ataishi kwenye Baraka Zake, za nje na ndani.
Zaidi
ya hayo hakika nyinyi, Mwenyezi Mungu akuwafikisheni mko katika mwezi,
ambamo Mwenyezi Mungu kakunjua katika mwezi huo, kutoka maandalio ya
u-Karimu Wake, kakunjua busati la maghfira na akafungua humo kwenye
hazina za Wema Wake, milango ya ihsani.
Mawingu
mangapi, na Akajaalia yaangushe mvua za Fadhila Yake kwenye mwezi huo,
(zikaanguka) kwa yule aliyepigwa na ukame, na zidhihiri ndani yake papo
kwa papo alama za uhai.
Na
katika mwezi huo ihsani za u-Karimu Wake zimeokoa wangapi wale
waliozama kwenye maasi, na la si ukarimu huo basi moto wa jahimu ndiyo
ungekuwa maskani yao ya mwisho.
Na
uwe wenye baraka kwenu basi huo mwezi adhimu ambao masiku yake ni mataa
kwa wote, na michana yake ni michana ya furaha, kwa sababu ya twaa ya
Mwenyezi Mungu tangu Dhikri na Tilawa na Swaumu.
Furaha kubwa iliyoje hiyo ambayo matunda yake ni furaha ya daima dawamu kwenye darii ya salama.
Basi
mshukuruni Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu akurehemuni, kwa neema hii
iliyokunjuliwa. Na jitahidini kwa amali njema inayokubalika mbele ya
Mwenyezi Mungu kwa sababu matunda ya jaza njema huumana na amali njema.
Na jikingeni katika wakati huu mtukufu msijitupe kwenye wimbi la maasi.
Kwa sababu kwenye zama tukufu mizigo ya machafu hulipwa marudufu kama
thawabu za mema zinavyotolewa maraudufu. Kuweni basi na hadhari kubwa
msije mkafungulia milango ya ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake
yenye maumivu makali.
Kwa
sababu yule ambaye haachi kauli ya kuongopa na amali yenye kukamatana
nayo, basi Mwenyezi Mungu hana haja kamwe na kuwacha kwa mja huyo
chakula chake kitamu na kinywaji chake.
Na
shaitwani kalipambia kundi lake lilo khasirika, yale mambo ambayo
yatawatia kwenye fedheha siku ya mwisho. Kwa hivyo kuweni na hadhari na
adui huyo na mtindo wake wa kupamba amali mbaya, na ombeni msaada kwa
Mwenyezi Mungu akulindeni na vitimbi vya adui huyo na mpangilio wa hila
zake, na zile njia anazopitia kukuharibieni amali zenu na kauli pamoja
na niya.
Na
juweni kwamba mwezi wa Ramadhani ni mwezi adhimu. Huwapeleka wenye
kuuamirisha, kwa amali njema, kwenye Pepo za Naimu. Mwezi adhimu ambao
Qur’ani umetaja fadhila zake na Sunna pia.
Neema
ngapi Mwenyezi Mungu anazitoa kwa upya, na upya tena kutupa sisi kwenye
mwezi huu. Kati ya mambo ambayo ni yake mwezi huu, ni ule usiku ambao
ni bora kabisa kuliko miezi alfu. Tanabahini mjue hiyo ni Laylatul-Qadr. Na utaijuaje, Laylatul-Qadr ndiyo ipi. Ni amani adhimu, inayoendelea mpaka kuchomoza kwa al-Fajiri.
Sunna imetaja fadhila zake, yale ambayo kwayo imani ya waumini huzidi na nyoyo za wenye kuwafikiwa hukunjuka.
Kati ya yaliyo pokewa makhsusi kwa yule mwenye kusimama kwa ibada kwenye Laylatul-Qadr,
hali ya kuwa ana amini vilivyo na kwa sababu anataka fadhila za usiku
huo, huyo hughifiriwa dhambi zake zilizo tangulia na zile za baadae.
Na Bibi Aisha, Radhy-Allahu ‘Anha kasema kwamba, ‘usiku huo ni usiku wa tarehe kumi na tisa.’ Basi fanyeni ukomo wa uwezo wenu kuipata bidhaa hiyo.
Na imetajwa kuhusu fadhila za mwezi wote kwenye Hadithi iliyopokewa na Abii Masoud al-Ghifaariyyi, Radhy-Allahu ‘Anhu kwamba yeye amemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu, swalla-Llahu aalay wa Ssalaam akisema, siku ulipoandama mwezi wa Ramadhani, “lau waja walijua yaliyomo kwenye mwezi wa Ramadhani, basi waja wangelitamani mwezi wa Ramadhani uwe mwaka mzima.... mpaka mwisho wa hadithi.
Na katika yale yaliyopokewa kutokana na Salman, Radhy-Allahu’Anhu kuwa alisema, “alituhutubia Mtume wa Mwenyezi Mungu swalla-Llahu aalay wa Ssalaam, siku ya mwisho ya Shaaban na akasema, ‘enyi
watu umekufunikeni nyinyi mwezi adhimu, mwezi mkuu wa baraka kuu. Mwezi
ambao ndani yake una usiku ulio bora kuliko miezi alfu. Amejalia
Mwenyezi Mungu kuufunga mwezi huo ni jambo la faradhi na kusimama kwa
ibada jambo la khiyari. Mtu mwenye kutafuta mkuraba kwa Mwenyezi Mungu
humo kwa jambo la kheri au katekeleza faradhi, huwa kana kwamba kafanya
faradhi sabini katika miezi isyokuwa huo. Nao ni mwezi wa subira na
subira thawabu zake ni Pepo.
Na
huo ni mwezi wa kutekelezeana haja, na mwezi ambao mumo rizki ya
muumini huzidishwa. Basi yule mwenye kumfuturisha mwenye kufunga mwezi
huo, hayo huwa ni maghfira kwa dhambi zake na shingo yake kuachiliwa
huru kwa moto. Naye hupata thawabu kama za yule pasina kupunguka
chechote kile katika ujira wake.”
Walisema, “si yeyote yule miongoni mwetu anayepata kile cha kumfuturisha mwenye kufunga.” Akasema, “Mwenyezi Mungu humpa thawabu hizi yule mwenye kumfutarisha mwenye kufunga, kwa Tende au gao la Maji au Maziwa kidogo. Nao ni mwezi mkuu. Mwanzo wake ni Rahma, kati yake ni Maghfira na mwisho wake shingo kuachiwa huru na moto.
Yule mwenye kumfanyia mtumwa wake mambo wepesi katika mwezi huo, Mwenyezi Mungu humghufiria na akamwacha huru na moto.
Basi fanyeni kwa wingi katika mwezi huo mambo manne. Mambo mawili, kwayo mtamridhisha Rabbu wenu. Na mawili mengine, hayo hamna budi nayo.
Ama yale mawili ambayo kwayo mtamridhisha Rabbu wenu ni ile shahada ya Llaa-Illaha illa-Llaa na kumwomba maghfira Mwenyezi Mungu.
Ama mawili ambayo kwayo nyinyi hamna budi nayo ni, (kwamba) mtamuomba Mwenyezi Mungu Pepo na kwaye mjalinda na Moto.
Na mtu mwenye kumpa mwenye kufunga chakunywa, Mwenyezi Mungu atamnywesha mtu huyo kwenye hodhi Langu, kinywaji ambacho baada ya hapo, mtu huyo kamwe hatoshikwa na kiu.”
Basi
zingatieni hayo Mwenyezi Mungu akurehemuni, ya fadhila ambayo yamo
kwenye mwezi huu na yale yanayozalika ya amali njema yenye kukubalika
mbele ya Mwenyezi Mungu. Na kuweni nyinyi watu walioshikamana na njia ya
wenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na wenye taqwa Yake. Na jitahidini
nyinyi mwezi ukuondokeeni hali kurasa za madaftari yenu zimejaa mema na
nje yenu na ndani yenu zimehifadhika na mambo yanayo kwenda kinyume na
sharia.
Sehemu
kubwa ya mwezi imekwisha pita na umewadia wakati wake wa kuondoka kwenu
na kuendelea na safari yake. Je, mwezi umekufikisheni kwenye hazina
zake, au umekufunulini siri zake, na au umezusha ndani yenu ninyi toba
ya dhati kwa dhambi zilizopita na mabaya yenye kufuata?
Kwani
hakika, hakika dalili za kupata kabuli kudhihiri kwenye udhati wa
iqbali na kumuogopa Mwenyezi Mungu ndiyo dalili yenye nguvu kupita zote
yenye kuthibitisha kwamba hali imo katika istikama.
Na
katika kupita siku za mwezi huu kuna mazingatio kwa upande wenu, ikiwa
mtazingatia. Na makumbusho kwenu vile vile, lau mtakumbuka. Kwa sababu
hakika, hakika siku hizo zitahisabiwa kuwa ni sehemu ya umri wenu na
kwenye kurasa zenu hayo yataandikwa. Basi zingatieni hayo enyi ndugu
zangu. Na simameni kidete kwenye amali njema zenye sifa ya kukubaliwa na
Mwenyezi Mungu na rudini nyuma, msiyaingie maasi katika zama na nyakati
zinazokukabilini. Kwa sababu, hakika, hakika nyinyi mmo kwenye safari
mnaiaga dunia na Akhera ndiko mnako kwenda. Na mtakapofika Akhera, hapo
itakubainikieni waziwazi, ipi biashara yenye faida na ipi ile ya hasara.
Kwa
hivyo jiandaeni kwa nyumba hiyo inayokabili, kwa maandalio yaliyo
kamilia. Na jitahidini kwenye twaa ya Mwenyezi Mungu upeo wa kujitahidi.
Na uchukulieni fursa umri wenu wenye kutoweka, kwa yale ambayo
yatakuleteeni raha ya milele, na kukusanyeni nyinyi na fadhila za
Mwenyezi Mungu hali mna madadi iliyo kamilia kupita zote. Kwa sababu
hakika, hakika, mja aliye wafikiwa ni yule ambaye anatumia nyakati zake
zenye kupita katika yale mambo ambayo yatampatia yeye maisha ya milele
kwenye nyumba ya maziidi. Kwa sababu nyumba ya Akhera imefichwa kwenu na
hamjuwi alama zake. Utakukuteni nyinyi, na hilo lisiwe na shaka,
unyonge wake ama utukufu wake. Yatakukabilini nyinyi, mtaposhuka huko,
yale ambayo huotesha mvii wana wa mkononi, na itakukumbeni nyinyi
kitapo, zama za kushuka huko, ambacho hata majabali hawamudu kukibea.
Je, kwa mazito hayo yenye kusakama koo, mnayo maandalio? Na je, kwa
safari ndefu hiyo mmetanguliza zawadi za njiani?
Basi
tanabahini kabla majuto hayajawa mjukuu na mguu haukukutieni kwenye
telezi, na kabla ya kalamu haijakauka juu ya lile ambalo limekwisha
kuandikwa kuhusu hatima yenu.
Basi
toba na tena toba, Mwenyezi Mungu akurehemuni toba dhidi ya machafu
kabla hamjanywa manywaji ya unyonge, na kuingi kwenye shamla baina yenu
na wanafiki, na waouvu kwenye makao mabaya kabisa, na nyumba yenye
kutisha kabisa.
Hasara kubwa ilioje ni ya yule ambaye mizigo ya maovu ndiyo zawadi yake ya njiani na maasi ndiyo sifa yake na ada yake.
Hatima
ya hali yake huyo ni mbaya, tena mbaya na watu wa hali hiyo hawana
thamani kwenye masoko ya saada na sudi njema ya abadi na abadi.
Ni
kweli mwenye akili na uoni wa jicho la ndani ataridhia afike kwenye
mkusanyiko wa kiyama na sura yake ni mbovu kupita sura zote, na aingie
kwenye fedheha katika hadhara hiyo kwa sababu ya yale maovu
aliyoyachuma?
Kwani ni vizuri itambulikane kwamba hizaya yasiku hiyo ni hizaya mbovu kweli na makazi ya wenye dhambi humo ni makazi mabaya kweli.
Hakimu Mwadilifu atadhihiri kwa maangamizo. Na itadhihiri mumo kwa watenda madhambi mwisho mbaya wa pahali hapo. “Siku
itakapobadilishwa ardhi na kuwa ardhi nyigine sio hii, na mbingu pia.
Na wao watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu mmoja asio na mshirika,
mwenye nguvu. Na utawaona waliokwenda kinyume na maamrisho siku hiyo
wamefungwa kwenye minyororo. Nguo zao ni za lami na nyuso zao
zimegubikwa kwa moto. (Na hayo) ili Mwenyezi Mungu ailipe nafsi yeyote
ile iwayo ile iliyoyachuma (Ibrahim, Aya 48-50).” “Siku
hiyo mtahudhurishwa - haitofichika siri yeyote yenu ile iliyofichika.
Basi ama yule atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia atasema;
haya nisomeeni kitabu changu. Hakika nilijuwa ya kuwa nitapokea hisabu
yangu. Basi yeye atakuwa katika maisha ya kuridhisha (al-Haqqa 18-21).” “Na
ama yule atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kushoto huyo
atasema laiti nisingalipewa kitabu changu wala nisingalijua nini hisabu
yangu. Lati mauti ndiyo yangelikuwa yakunimaliza moja kwa moja. Mali
yangu haikunifaa kitu kamwe, Usultani wangu umeniangamilia (al-Haqqa
25-29).”
Je
mmejua enyi ndugu zanguni haki ya siku hiyo na yale malipizo
yatakayodhihiri humo, na kwa hivyo mkawa katika nyumba hii mnaifuata ile
njia ya kumuogopa Mwenyezi Mungu na kuwa na taqwa Yake? Kwa sababu
hatima ya watu wa pote hilo ni hatima ya salama na mwisho wao ni kwenye
nyumba ya milele. Nyumba nzuri iliyoje nyumba hiyo. Mumo kuna Naimu ambayo haiwezi kudirikiwa na akili wala macho, “na
wakatiwa wale wenye kuamini na kutenda amali njema, zenye sifa ya
kukubaliwa na Mwenyezi Mungu, kwenye Pepo kuu ambamo chini yake inapita
mito.”
Je hamyajui mambo hayo ya siku hiyo? Na ikiwa ni hivyo basi yenu ni hasara iliyofunika hasara zote, “sema; stareheni, kwani hakika hakika mwisho wenu ni motoni. Jahanamu wataiingia na makazi yaliyoje hayo.”
Mwenyezi
Mungu atusalimishe sisi na nyinyi na vitisho vya nyumba hiyo na
atuhifadhi sisi na nyinyi na yale yatoleta unyonge na fedheha, na
Atushike sisi mkono sote kwenye mwezi huu mtukufu na umri uliobaki,
Atushike mkono kwenye jua ya waja wake aliowapa mkuruba Naye, na watenda
zema.
Ewe
Allahumma, Ewe Mola Karimu, Mwenye kutoa pasina kungoja ukaombwa, Ewe
Wahhaabu, Mpaji msikikomo katika upaji Wako, Ewe Rahimu, Mrehemevu, Ewe
Tawwaabu, Mwingi wa kumpa toba mja wako hata akatubia, Nawe ukawa Mwingi
wa kupokea toba, tena na tena.
Sifa
Yako ni Rehema na Ukarimu, na athari za hayo ziwazi kweupe katika
wujudi. Ikiwa nyuso zetu zinapiga weusi kwa dhambi na kufanya mambo
kinyume na maamrisho, basi tegemeo letu za kunawirishwa nyuso hizo
zikapata weupe, tegemeo letu ni juu ya Ukarimu Wako. Ewe Mwenye kukubali
toba ya waja Wake na Mwenye kusamehe maovu, mlangoni Kwako tumesimama,
na Wema Wako tunauomba, na tamaa haiwi njema isipokuwa Kwako tu, na
maombi, haliwi jambo lililo ndilo ila yakifanywa Kwako.
Tunakuomba
kwa ndimi ambazo kwa muda mrefu kwazo tumekuasi. Na tunaelekea Kwako
kwa nyoyo na viungo, ambazo kwa muda mrefu tumefanya maovu mbele Yako.
Na lau si wingi mkuu wa madadi Yako kuu na furifuri ya hilmu Yako
adhimu, ambazo kwazo Ume-tuamili na sisi tumo katika hali hiyo, kamwe
tusingejistirisha kutaka na kuomba. Lakini dhana njema Kwako ndiyo
iliyotasua ndimi zetu kwa maombi. Na kutupa sisi bishara njema kwamba
tutayafikia tunayoyataka na tutayadiriki malengo yetu, hasa hasa kwa
kuwa sisi tuna wasila Kwako, nao ni Mja Sharifu kupita wote uliyemsogeza
Kwako, Bwana wetu al-Habib, alo adhimu, mwenye raafa, mwingi wa rehema,
Habibi Wako ambaye umemteua akawa na cheo cha juu kuliko kila Habibi,
na mtengwa Wako ambaye umemnyanyua na kumweka kwenye cheo kitukufu
kupita vyote kwenye hadhara za mkuruba, muombezi mkuu kupita wote, na
Mtume mtukufu kupita wote, Bwana wa Mitume mursali na Mtume wa mwisho wa
Mitume yote, Bwana wetu Muhammad bin Abdillah, mkweli, muaminifu.
Ni
huyo ndiye tunatanguliza jaha yake Kwako, na kwaye tunaomba uombezi
wake, ili amali zetu zipate kabuli na dhambi zetu zighufiriwe.
Tunakuomba
Ewe Allahumma, kwa cheo ulichompa mbele Yako uumpe shafaa juu yetu na
umsalie Yeye kamilifu kabisa ya swala na timilifu kupita zote, na yenye
sharafa kupita zote, na yenye ku’umu kupita zote. Na swala hiyo
iwafunike Aali zake wote, na Sahaba zake watukufu, na wale wenye kwenda
mwendo wake ulionyooka na wenye kutekeleza haki za Mwenyezi Mungu, na
salamu juu ya Mitume mursali wote. Na himdi zote zile zinamhakia
Mwenyezi Mungu pekee na Rabbi wa viumbe piya.
No comments:
Post a Comment