Shaykh
Abdallah bin Muhammad bin Swaleh Baakathir (radhi za Mwenyezi Mungu
zimwalie), mmoja kati ya wanazuoni wakubwa wa zama zake alirushwa roho
na jambo moja akiogopa sana kwamba watu wasifike hadi ya kutotambua
neema kubwa waliyokuwa nayo. Akiogopa kwamba wakiacha kuitambua neema
hiyo, hapatakuwa tena na shukurani na shukura ni kufuli ya neema.
Ikifanywa shukura, neema hubakia. Zaidi kuliko hayo ni kwamba neema ile
hustawi ikaingia na baraka. Na huvuta neema nyingine ambazo mtu kamwe
hazikumpata kumjia katika mawazo yake. Kwani si anasema Azza-wa-Jaala, "lau matashukuru hakika hakika nitakuzidishieni”.
Aya haifafanui kitakacho zidishwa ni kipi na wala kitazidishwa kwa
kiwango gani. Na madamu hayo yanasemwa na Mola ambaye yeye mwenyewe
kajiita Shaakhir, mwingi wa kushukuru, basi mawazo ni huria. Shaykh
Abdallah Baakathir (radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie) anataja dukuduku
lake mwanzo wa kitabu chake cha al-Ashwaaq anasema hivi, “kupatikana
mtukufu huyu na watu mithali yake katika zama hizi ni neema kubwa
kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Anaitambua mwenye kuitambua na mjinga nayo,
yule ambaye ni mjinga nayo. Tunamwomba Yeye taala atupe sisi tawfiqi ya
kusimama na kushukuru neema zake zote zile za nje na ndani.”
Na anaendelea kusema, “au wanazijua lakini wanazikataa na hawazishukuru.” Hapa Shaykh Abdallah anaashiria kuwa neema huwapo na mtu akaikataa.
Je,
neema hiyo anayoizungumzia Shaykh Abdallah Baakathir ni neema ipi? Hiyo
ni neema ambayo pengine leo watu wa Unguja na Afrika Mashariki nzima
wameisahau, nayo ni kuwepo kwa Al-Habib Ahmad bin Abi-Bakar bin Sumayt
(radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie) miongoni mwao. Neema ambayo al-Habib
Ahmad bin Umar bin Sumeyt (radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie) alikwisha
bashiria kuzaliwa kiasi miaka ishirini kabla ya ujudi wake. Na Leo ni
Miaka thamanini na sita toka kutawafu kwake.
Shaykh
Abdallah Baakathir anamweleze hivi basi, Shekhe wake, al-Habib Ahmad
bin Abi-Bakar bin Sumayt mwanzo mwanzo wa kitabu chake cha al-Ashwaqq,
"Bwana mwenye sharafa kuu na utukufu mkuu, aliyekunywa kifu yake ilmu
zote zile za akili na kupokea, mwenye kukusanya fani za lugha fasaha,
mtatuaji wa mishkeli na mtanzuaji wa mitata. Nadra wa zama na pambo la
miji na Mufti wa pekee aliyekusanya ya fadhila na matukufu.... nilisoma
kwake vitabu kadhaa wa kadhaa na huyu ni Bwana ambaye mazoe yake ni
kutembea kwenye bustani za ilmu na ma’arifi na kuchuma hikma na zile
ilmu zenye kufichika baina wino na ibara. Aliyepweke katika kuhakiki masaaili
na mpweke wa zama zake katika kudiriki undani wake. Kawaswahibu
ma-Qutbu na Mashekhe wakubwa wa zama zake, na mawalii ma-‘Arfina,
wanazuoni wahakiki wa dahari yake. Na kwao kapata enga enga na malezi na
madadi. Na wao wakamshuhudia kwa matukufu walionayo na ukamilifu wake.
Wakamhisabu kuwa yeye ni mmoja wapo ya rijali waliokamilia na
wakamfungulia mapazia kumjulisha siri za tarika na hakika zilizomo humo.
Na wakamnywesha kinywaji safi cha ilmu ladunniya.
Kutokana na baraka zao Mwenyezi Mungu kadhihirisha mangapi kwenye ulimi
wake na kalamu yake, yale ambayo yamefichika kwenye fahamu za wengine,
na akamimina kwenye maji ya matamko yake matamu yale ambayo yanakonga
kiu cha figo cha wanazuoni wa wanazuoni. Ana shuhudiwa kwamba katika
ilmu za hakika na maarifi yeye ni Imamu na mzuri aliyoje kuwa Imam. Na
kwamba yeye ni nguzo marji'i ya watengwa makhsusi na watu wa kawaida
kwenye fani zote za lugha na pia sharia na hukumu.....”
Zaidi
ya Shaykh Abdallah Baakathir, Habib Ahmad bin Sumayt alikuwa pia ni
Shekhe wa Al-Habib Umar bin Ahmad bin Sumayt, Habib Abdulrahman bin
Ubaydillah, Shaykh Sulaiman Alawy, Shaykh Hassan bin Amer na Shaykh
Burhan Mkele, kuwataja kwa uchache. Wanazuoni wa zama, ambao matukufu
yao hayahitaji kupigiwa debe.
KWA MAKALA NYINGI ZAIDI TEMBELEA
KWA MAKALA NYINGI ZAIDI TEMBELEA