Friday, August 16, 2013

UBORA WA SIKU YA IJUMAA

Siku ya Ijumaa ni siku bora na tukufu miongoni mwa siku za dunia, Mtume (S.A.W)Rehma za M/Mungu zimshukie Juu yake na Amani ameitaja siku ya Ijumaa kama hivi : “Bora ya siku uliyochomozewa na jua ni siku ya Ijumaa, ndani yake Ameumbwa Adamu ndani yake ametiwa peponi. Na ni ndani yake (siku hiyo) alitolewa humo (peponi) na wala hakitasimama kiyama ila ndani ya siku ya Ijumaa”. Kama alivyosema Mtume hadithi imepokewa na Imamu  Muslim.

Zimepokelewa hadithi nyingi kutoka kwa Bwana Mtume (S.A.W)Rehma za M/Mungu zimshukie Juu yake na Amani zikitaja fadhila na ubora wa siku hii ya Ijumaa. Hii ni siku ambayo umo ndani yake wakati (muda fulani) ambao mja hamuombi Mola wake ndani yake chochote cha kheri ila humpa.

 Ni kwa ajili ya fadhila hizi tulizozitaja na nyinginezo, Allah akaichagua siku hii kuwa ni Idi (sikukuu) ya kila juma (wiki) ya waislamu. 

Akawaamrisha waja wake kuipa umuhimu wa pekee siku hii, wajipambe kama walivyoelekezwa na kufundishwa na Mtume wao. 

Waache shughuli zao na waharakie kuiendea ibada ya swala ya Ijumaa. Wakutanike pamoja ndani ya siku hii ili iwe ni nembo, alama na kielelezo cha umoja wao na dalili na ishara ya nguvu yao. Siku hii ni zawadi kwa Umma wa Nabii Muhammad (S.A.W)Rehma za M/Mungu zimshukie Juu yake na Amani kwani ni sababu ya kufutiwa dhambi zao na ni kirudufisho cha ujira na thawabu. 

Lakini kwa masikitiko makubwa, uzoefu unaonyesha kuwa waislamu wamekuwa ni watu wa kuzembea na kupuuza kila kitu. Hata kufikia kiasi cha kudharau matukufu ya dini yao yaliyotukuzwa na Mola Muumba wao, huu ni msiba mkuu na haya ni maangamivu. Leo siku ya Ijumaa machoni na mioyoni mwa waislamu wengi si cho chote na wala si lo lote ila ni siku tu kama zilivyo baki ya siku nyingine za juma. Hili halihitaji ushahidi kwani linashuhudiwa bayana na kila mmoja wetu.

Waislamu tumeipuuza siku yetu tukufu ya Ijumaa, siku iliyokuwa na nafasi,cheo, daraja na iliyopewa umuhimu wa pekee na mababu zetu (wahenga). Wazee wetu hao wema waliutambua umuhimu, utukufu na ubora wa siku ya Ijumaa, hivyo wakawa wakiingojea kwa hamu na shauku kuu.

Waliingojea kama mtu mwenye kiu ayangojeavyo maji baridi au mithili ya mgonjwa aingojeavyo siku ya kupona na kupoa kwake. Wakawa wanakoga, wananadhifisha nguo zao, wakajitia manukato na wakienda mapema msikitini kuhudhuria swala ya Ijumaa. Wakienda msikitini ilhali wamefunikwa na staha, heshima, utulivu na unyenyekevu. Nyoyo zao zikiwa zimesheheni khofu ya Allah Bwana Mlezi wao na ndimi zao zikiwa majimaji kwa utajo (dhikri) wa Mola wao. Macho yao yakiwa yamesitiriwa na maharamisho ya Allah, hata wakiingia msikitini kila mmoja wao akiwania kuchukua nafasi iliyo karibu na khatibu; nafasi ya mbele. Walifanya hivi kutokana na kupupia kwao kuhodhi fadhila za safu ya kwanza na kustafidi na khutba. Khatibu anapopanda juu ya mimbari na kuanza kukhutubu, huwa makini, nyoyo zao zikizingatia, usikivu (masikio) wao huwa wazi. Khatibu hamalizi khutba yake ila huwaliza wote; janibu ya twaa na janibu ya maasi. Janibu ya maasi hulia kutokana na kuichelea adhabu na ghadhabu ya Allah. Wakati ile janibu ya twaa ikilia kutokana na tamaa ya fadhila na thawabu za Allah.

Enyi ndugu waislamu, tuchungeni adabu za siku hii tukufu, tujinadhifisheni, tujipambeni na tujitieni manukato kwa ajili ya siku hii adhimu. Tutokeni majumbani mwetu kwa unyenyekevu kuelekea kwenye nyumba za Allah. Twendeni mapema na tukiingia msikitini kila mmoja wetu akae kwa adabu, heshima, staha na utulivu. Tutahadharini na kufanya kitendo au kusema kauli itakayomuudhi Allah, Mtume wake na waja wake mithili ya kukata/kukengeuka shingo za watu. Tueleweni kwamba kuwaudhi waislamu ni jambo linalopomosha ujira na kubatilisha thawabu adhimu za Ijumaa.

Atakayeingia msikitini miongoni mwetu na ilhali khatibu anakhutubu, basi na asikae chini ila baada ya kuswali rakaa mbili khafifu (nyepesi). Tunapomaliza kuitekeleza fardhi hii ya swala ya Ijumaa, tusiwe na haraka ya kutoka msikitini. Tukae tuswali suna, tulete dua na tumuombe Mola wetu maghfira, radhi na uongofu. Mola wetu Mtukufu tunamuomba airejeshe haiba na utukufu wa siku ya Ijumaa katika nafsi, nyoyo, roho na miili yetu Amiin.

Tunawatakia Ijumaa Njema.

No comments:

Post a Comment