Bismillahi ndio uwe mwanzo wa kila kitendo na fikira na rahma za Rahman zitutangulie kwa mbeleni na zitulinde migongoni mwetu. Ar-Rahim ndiye Yeye mola Rahim; Mola mmoja apasae kuabudiwa usiku na mchana na viumbe wake wote. Na Hakika Mola hakuumba binadamu na majini ila kwa ajili ya kumwabudia yeye, Allah aliye mpweke pasina mshirika.
Na swala na salamu zimwalie Mtume wetu Hashimu aliyekuwa muadhama mbele ya Mola Karimu kushinda kila Nabiyya. Na ziwaalie Aali zake na Sahabaze kiramu na Mitume mursali pia. Na waja watenda zema Mola awashushie radhi zenye mmiminiko wa mahaba yasiyokwaisha asilani.
Baada ya basmalla na kumtakia mema wetu Habibi, Al-Mustafa Al-Amin Abu-l-Qassim Sayyidina Muhammad ibn Abdillah, Sayyidina-l-Ambiyya waa Imamu-l-Kiblatain, Taha wa Yassin. Basi na tuanze kumwelezea japo kwa uchache Shaykh wetu aliyetufikisha hapa mpaka kufungua website hii ya www.mwinyibaraka.com. Naye si mwingine bali ni Al-Faqiir Shaykh Ahmad bin Muhammad bin Shaykh Msiha, Mwenyezi Mungu atunufaishe naye na radhi zake zimshukie kwa wingi yeye na Aali zake.
Al-Faqiir Shaykh Ahmad, mwandishi wa makala haya lazima aseme kuanzia mwanzo ya kuwa hakujaaliwa kukutana na walii huyu wa Mwenyezi Mungu katika uhai wake ila mahaba yake yamemfikia pale mwandishi alipohitajia mwelekeo katika mambo ya dini na imani. Kwani kwa hakika ya mambo, mahaba ya dhati yanauka malimwengu.
Al-Faqiir Shaykh Ahmad alikuwa ni mwanafunzi na Khalifa wa Al-Habib as-Sayyid Umar Abdallah bin Shaykh Abi-Bakar bin Salim ama kwa umaarufu Mwinyi Baraka, na Mwinyi ndiye aliyemjazi tarika Qadiriyya ya Bwana wetu wa Jailani. La! Si Bwana wa Jailani tu bali Bwana wa ulimwengu kwa hakika. Na vilevile tarika ya mabwana wetu watukufu wa Baa-Alawi. Mahaba yake juu ya Shekhe wake yalimpelekea Al-Faqiir Shaykh Ahmad kabla ya kutawafu kuanzisha taasisi ya Mwinyi Baraka Islamic Foundation ili ije kuwa kioo cha ilmu kama alivyokuwa yeye mwenyewe Sayyid Umar Abdallah, Mwinyi Baraka (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie yeye na wazee wakee na wale wote walioshikamana naye) na amana ya kuendeleza fikra hiyo kuwaachia wanafunzi na muridi wake wa Al-Majaalis El-Ulaa Qadiriyya Mwinyibaraka Uweysia chini ya Ukhalifa wa Shaykh Iddi bin Umar na Shaykh Issa bin Uthman bin Issa. Na Insh-Allah kwa uwezo wake Subuhanna wa Ta’ala amana tumeibeba.
Al-Faqiir Shaykh Ahmad katika matayarisho ya hayo alinunua ardhi yenye ekari 23 maeneo ya Kibaha katika kijiji cha Misugusugu, na katika ardhi hiyo ndipo ilipo rawdha yake tukufu, kwa ajili ya kujengwa kituo cha ilmu, kuanzia shule ya chekechea mpaka Chuo Kikuu na Insh-Allah, Mola na atujalie kufikia malengo hayo kabla ya uhai wetu kwisha na tutimize wasia huu wa Shaykh wetu ili nasi tuwe wamoja katika wale waliomuenzi kwa mahaba ya dhati yeye na Shaykh wake Al-Habib Mwinyi Baraka (radhi za Mwenyezi Mungu ziwaalie wote wawili). Basi na kwa kuanza tumeonelea vyema tuanze na hii tovoti ili iwe ni ukumbusho kwa wale wenye kiu ya kutaka kupata ilmu.
Al-Faqiir Shaykh Ahmad katika uhai wake alikuwa siku zote ni wa kusisitiza watu wawe wa kutafuta ilmu, yeye mwenyewe akiwa mwandishi wa vijitabu kadha wa kadha. Pia alikuwa mwenye kusisitiza juu ya fadhila za kumswalia Bwana wetu na Mtume wetu, Muhammad mtengwa, swala na salamu zimshukie na mashahiri yake mengi ameyatunga juu ya wasifu na fadhila za Bwana wetu Al-Mustafa. Katika moja ya mawaidha yake Al-Faqiir Shaykh Ahmad anayaelezea mapenzi juu ya Bwana Mtume, swala na salamu zimshukie kuwa ni mapenzi yanayotokana na Mwenyezi Mungu, Subuhanna-wa-Ta’ala, moja kwa moja na hayana sababu juu yake, yaani ni mapenzi yanayotokana na nuru yake Allah moja kwa moja. Kwani kila mapenzi mangine yana sababu ya kupenda; mfano mtu akisema anampenda bibi fulani. Anasema, “anaweza akawa anampenda bibi huyo kwa sababu anaona bibi yule anaweza akamkidhia haja zake ama ni kwa sababu ya uzuri wake alionao ama kwa mengine. Lakini inapokuja suala la kumpenda Mtume (swala na salamu za Mwenyezi zimwalie), mja hutokea kumpenda hali ya kuwa hajapata hata kumwona bali ni kwa kusikia tu, kiasi wengine wakawa wanalia na wengine kupiga mayowe kila atajwapo Habibi Mustafa.”
Hapa
tumeainisha kwa ufupi kuhusu Shekhe wetu, Al-Faqiir Shaykh Ahmad (radhi
za Mwenyezi Mungu zimshukie). Urefu wa maneno uyatapata kwenye tovouti
makhsusi juu ya maisha yake al-Habib inayoendeshwa na muridi wa tarika
Qadiriyya, nayo ni http://www.al-faqeer.com/. Na humo kuna mengi yaliyoandikwa kuhusu walii huyu pamoja na vitabu na kaswida zake alizoandika.
KWA MAKALA NYINGI ZAIDI TEMBELEA
KWA MAKALA NYINGI ZAIDI TEMBELEA