Wasifu wa SHAYKH SULAYMAN BIN MUHAMMAD AL-ALAWIY, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie.
Katika
miaka sitini iliyopita Msikiti Gofu ulipata hadhi kwa Shaykh Sulayman
bin Muhammad al-Alawiy, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie. Hapa,
natufuate basi ule muongozo wa; mwite mwanachuoni mkubwa akupe wasifu wa
mwanachuoni mkubwa mwenzake. Na kwa mintarafu hii wa kusema juu ya
Shaykh Sulayman bin Muhammad al-Alawiy na awe al-Habib Abdulkadir bin
Abdulrahman bin Umar al-Junayd, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie,
maarufu kwa jina la Sharif Junayd mjini Dar-es-salaam na kwengineko
Tanzania. Na yeye kwenye chuo chake cha al-‘Uquudu Al-Jaahizah. Kwa
hakika Sharif Junayd kamtia Shaykh Sulayman bin Muhammad bin Sulayman
bin Said al-Alawiy (pichani kushoto) katika kundi la mashekhe zake. Hiyo
ni fahari juu ya fahari kwani machoni mwa wanachuoni wa wanachuoni
Sharif Junayd ni mwanachuoni. Katika hali kama hii kauli yake Sharif
Junayd hiyo ingalitosha lakini dharura za wakati na uchache wa mizani
ulionea katika zama zaetu unatulazimisha tuenedelea mbele zaidi kuliko
hivyo.
Basi
tunanukulu maneno ya Sharif Junayd (pichani kulia) juu ya Bwana huyo,
“alikuwa mwanazuoni aliyepea katika uwanazuoni na bahari ya ilmu
iliyojaa ilmu tamu tamu na safi, ambaye kafika kwenye kilele cha pekee
kwenye ilimu na hasa ilimu za lugha kama vile nahuu na sarfu na balagha
na mantik... Na licha ya kuwa katabahhar (kazama katika bahari)
ya ilmu mbalimbali alikuwa na istikama. Kaandamanisha ilmu kwa amali
hata akafikia utukufu upeo wa matarajio. Alikuwa na khuluka ya daraja ya
juu na tawadhu’i iliyofika mbali, alikuwa na moyo wenye kubeba mazito
na subira na uvumilivu uliofikia upeo. Alifanyiwa uadui na kwa makusudi
aliudhiwa. Lakini kamwe hakudhihirisha ghadhabu. Aliishi maisha ya
kukinai na zuhdi na taqwa. (Na akapitisha maisha yake yote kulea muridi
kwenye taasisi ya ilmu huko Unguja na huko Msikiti Gofu (karibu na
nyumbani kwake)....
Alipofariki
Shaykh Suleimani, Sharif Junayd alimlilia hivi, “akili yangu amkani
nahisi zimenipotea. Kwa mazito malemevu nimo kwenye ulimwengu mwengine.
Si bida’a ikiwa nimezisahau hisi zangu, nikawa wote nimekufa ganzi.
Kwani masiku yamenielemea kwa mambo mazito, kwa msiba ulionivunjavunja
nisibaki kitu. Kwa kuondoka Ustadh wetu Suleimani, taa ya ilmu na hazina
ya ‘irfaani. Bahari ya ilmu, mwenye kuiendea huchota johari atakazo na
dhahabu pia. Jamali ya zama, mwema wa utajo. Hatajwi kwa baya tangu
ujana wake. Mwingi wa kurejea kwa Mola wake, mcha Mungu mwingi wa
kurukuu mwingi wa kusujudu, mwenye kuhuisha ashari kwa Qurani. Zagao za
amali zake njema ziwazi na zenye kuonekana. Ni shani kubwa ilioje, yiyo
ikiwa ya nuru. Sifa ngapi zenye kuhimidiwa na magapi matukufu ya
kumtenga alikuwa nazo, na ambazo maneno yangu hayafiki. Wara’a fika na
khuluka zenye kuridhisha na uthabiti ambao kamwe wa pili hana, na haiba
na murua na vumilia ya maudhi na khashya ya rahmani. Kalelewa Unguja
kwenye mabustani ya ilmu anachuma matunda yenye wingi wa utamu, kapokea
kwa wakuu ma-Bwana niwasifu vipi wanazuoni hao rabbani. Mtaje shihabu
wetu khasaa mwana wa Sumeyti, mwana kwea wa juu kweye mbingu za ilmu.
Wakammiminia siri zao na kwazo akawazidi kimo wote wa rika yake, ai moyo
wangu na huzuni zangu leo kaniondokea. Hayuko tena kwenye duru wala
kwenye majengo, ai moyo wangu na simanzi zangu. Kwani ye' ni mwezi wa
mwisho kuduru kwenye midani, sasa kumekuwa kiza tangu kuuka kwake na
totoro imetawala. Ewe ni kuu huzuni zangu na mkubwa mno msiba wangu,
furifuri machozi yangu furifuri yanamiminika. Nikiuambia moyo subiri,
huniambia subira si uwezo wangu.... Ewe baba wa Zamil ghafula umeondoka
na kughibu, ewe pweke wa zamani umeghibu hali ya kuwa sisi kubwa haja
yetu kwako, katika kila shani.... Na vikulilie vitivo vya ilmu. Na vilie
vururu visiwe na kizuizi. Ikulilie Unguja kwani buruji ya ilmu nguzoze
zimedamirika. Naapa machozi na kilio changu yatadumu urefu wa zama.
Kaburilo likiwa ardhini ewe mkuu wa matukufu basi lilo liko kwenye pepo
ya Jinani.... furahika basi kwani milele utabaki utajo wako mwema na huo
ni umri wa pili. Lala usingizi macho tele kwenye bustani ya kaburi,
hali umefurahika kwa Raufu na Rayhani.... Ewe Rabbi huyu mja Wako, mgeni
Wako, hela mpokee kwenye dari ya ridhaa na nyumba ya amani. Na
mwonjeshe kwa fadhila Zako maji ya ridhaa na afua Yako, na mkuruba na
maghfira Yako. Na tupe ujira Ewe Rabbi na tupe badili miongoni mwetu, na
tupe kheri na ihnsani. Na juu ya kaburi lake yaanguke mawingu ya radhi,
na yawe ya kudumu urefu wa zamani."
Wasifu
huu wa Shaykh Sulayman al-Alawiy umetoka katika kitabu juu ya maisha ya
al-Habib al-Imam Ahmad bin Hassan al-Attas, radhi za Mwenyezi Mungu
ziwaalie wote wawili, kitabu kilicho njiani kuchapwa.