JWTZ YAPELEKA KILIO RWANDA
*Yakamata maofisa wake wanne wa Kijeshi
*M-23 wakiri majeshi ya UN ni hatari yatawamaliza
ASKARI wa Umoja wa Mataifa wanaolinda amani nchini Kongo (Monusco),
wakiongozwa na vikosi vya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wamedai
kuwakamata maofisa wanne wa jeshi la Rwanda, katika mapigano ya wiki
iliyopita nchini Kongo.
Akizungumza na MTANZANIA Jumatano kwa
sharti la kutotajwa jina, mmoja wa askari aliyepo ndani ya kikosi cha
JWTZ huko nchini Kongo, alisema maofisa hao wanashikiliwa kwa mahojiano
zaidi.
Taarifa hizi za sasa zinakuja wakati ambapo kumekuwa na
madai ya muda mrefu, ambayo yamekuwa yakitolewa na Umoja wa Mataifa
pamoja na Marekani kwamba, Rwanda imekuwa ikiwasaidia waasi wa kundi la
M-23.
Pamoja na kwamba Rwanda imekuwa ikipinga madai hayo,
kitendo chake cha wiki iliyopita cha kuamua kupeleka bataliani mbili
zenye wanajeshi 1,700 ili kukabiliana na kile kinachodaiwa kuwa ni
kishindo cha vikosi vya Umoja wa Mataifa vyenye jukumu la kulinda amani
katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa kirasilimali, kinatokana na waasi
wa M23 kupata kipigo kikali.
Chanzo chetu hicho kutoka uwanja
wa mapambano nchini Kongo, kililidokeza gazeti hili kuwa maofisa hao wa
Jeshi la Rwanda waliwakamata katika mapigano hayo yaliyodumu kwa zaidi
ya wiki moja, ambayo tayari yamewakimbiza waasi wa M23.
“Askari wa Rwanda tuliowakamata, ni maofisa wa ngazi za juu kabisa
jeshini, tena walikuwa na sare za jeshi hilo… walikuwa wakiwasaidia hao
M23, lakini kwa kuwa sisi tulikuwa makini tulifanikiwa kuwatandika hadi
tukawakamata,” kilisema chanzo chetu hicho.
Habari za uhakika
kutoka vyanzo vya habari vya kuaminika zinaeleza kwamba, hatua hiyo ya
kuwakamata maofisa hao pamoja na kuondoka kwa waasi wa kikundi cha M23,
imefanikisha kushinda vita hiyo kwa zaidi ya asilimia 95.
Mtoa
taarifa wetu huyo kutoka Kongo, ameliambia gazeti hili kuwa, tayari
Monusco wanaoongozwa na JWTZ wameanza kufurahia ushindi huo na kwamba
sasa hivi wanasubiri tamko kutoka kwa wakuu wao, ili kufahamu
kinachofuata baada ya kufanikisha hatua hiyo.
MAPIGANO YALIVYOKUWA
Akielezea namna walivyofanikiwa kutoa kibano kwa M23, askari huyo
kwanza alikiri kuwa mapigano yalikuwa makali, kutokana na kikundi hicho
cha waasi kusheheni vifaa vya kisasa na msaada wanaoupata kutoka
Serikali ya Rwanda.
“Kwa kweli mapigano yalikuwa makali sana,
lakini kwa upande wetu sisi tulikuwa tunajiamini kutokana na vifaa
ambavyo pia ni vya kisasa hususani ikizingatiwa jeshi letu ni la Umoja
wa Mataifa.
“Tulifanikiwa kuteka ngome yao kwa kutumia mbinu mbalimbali za kijeshi na kuwafanya watawanyike kabisa katika eneo hilo.
“Ngome yao ilikuwa ni kubwa sana, ina ukubwa wa zaidi ya viwanja vitatu
vya mpira… na katika eneo hilo kulikuwa kumesheheni vifaa vyao vya
kivita, kama makombora, mafuta, mizinga pamoja na vifaa vingine kama
magari na baadhi ya silaha nyingine kubwa kubwa za kivita,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, sasa hali ni shwari ndani ya nchi hiyo ya Kongo.
“Baada ya kuwasambaratisha sasa wamekimbilia eneo moja lililopo karibu
na mpaka wa Uganda. Kama unavyofahamu hawa jamaa walikuwa wakitumia
mbinu za kujihami kwa kurusha mabomu katika eneo la Rwanda, ili ionekane
kuwa sisi tumerusha,” alisema askari huyo.
“Lakini
tunamshukuru Mungu, tupo salama ingawa tumempoteza askari mmoja na
askari wengine wenzetu wa Tanzania ambao ni wanne, wamepata majeraha
kidogo lakini wanaendelea vizuri.
“Hivyo nawaomba Watanzania
wenzangu waendelee kutuombea turudi salama, kwa sababu kazi sasa
imeshakamilika,” alisema askari huyo.
Juhudi za gazeti hili kumpata msemaji wa Monusco, Luteni Kanali Prosper Basse kuzungumzia juu ya taarifa hizo, zilishindikana.
Taarifa ambazo tumezinasa kwa siku kadhaa sasa kutoka uwanja wa
mapambano na ambazo zimegusa vichwa kadhaa vya habari zinaeleza kuwa,
brigedia maalumu ya vikosi vya UN yenye dhamana ya kujibu mashambulizi
(FIB), katikati ya wiki iliyopita iliendesha operesheni kubwa
iliyoharibu kabisa ngome muhimu ya waasi wa M23, hali inayotajwa na
wachambuzi wa mambo kuwa ndiyo iliyoishtua Serikali ya Rwanda ambayo
inatuhumiwa kuwasaidia waasi hao.
Taarifa za kijeshi zinaeleza
kuwa, FIB ambayo inaundwa na wanajeshi wapatao 3,000 kutoka Tanzania na
Afrika Kusini chini ya Azimio Namba 2098 la Baraza la Usalama la Umoja
wa Mataifa, limejizatiti kwa zana za kisasa za kivita zikiwamo mizinga
na helikopta za kivita.
Taarifa kutoka mashariki ya Kongo
zinaeleza kwamba, mashambulizi dhidi ya waasi wa M23 ambao hivi karibuni
waliripotiwa kusababisha kifo cha mwanajeshi mmoja wa Tanzania aliye
katika jeshi la UN, yamesababisha waasi hao kukimbilia katika eneo la
milima lililopo umbali wa kilomita tano kutoka mji mdogo wa
Kanyaruchinya Mashariki mwa Goma.
M23 WAZUNGUMZA
MTANZANIA
Jumatano jana lilifanikiwa kuzungumza na Rais wa M23, Bertrand
Bisiimwa, ambapo pamoja na mambo mengine alieleza sababu za vikosi vyao
kuondoka katika ngome yao ya kivita sambamba na taarifa za kuibuka kwa
mapigano mapya ya hivi karibuni.
Katika hilo, Bisiimwa alikiri
kikosi chake kurudi nyuma siku nne zilizopita, huku akiitaja sababu ya
kufanya hivyo kuwa ilitokana na wao kutotaka vita baada ya majeshi ya
Kongo kuanza kuwarushia mabomu kwenye kambi yao.
“Sisi tuliamua
kurudi nyuma tusiendeshe vita, tunajua aliyetupa hayo mabomu ambayo
yalifika mpaka Rwanda, tunaitaka Umoja ya Mataifa ikuje ifanye uchunguzi
wake…wakuje waangalie vifaa yetu waone kama inaweza kurusha mabomu hadi
Rwanda,” alisema.
Hata hivyo, Bisiimwa alisema kuwa sio kweli
kama majeshi ya Umoja wa Mataifa yakiongozwa na JWTZ yaliwasambaratisha
katika ngome yao.
“Sio kweli walikuja Kanyaruchina tukiwa
tumeondoka na tuliondoka si kwa sababu ya kuwakimbia, hapana tulitaka UN
wafanye uchunguzi yake juu ya kurushwa mabomu, kwa sababu wanataka
kutuvalisha mambo ya uongo mchafu,” alisema Bisiimwa.
Bisiimwa
alijigamba kuwa majeshi ya Kongo hayawawezi na kwamba
walikwishawashindwa, lakini akakiri kwamba majeshi ya Umoja wa Mataifa
wanaweza kuwaondoa.
“Ninakiri hiyo kwa sababu Umoja wa Mataifa
inaweza kututoa, unajua inakuwa na nguvu ya hatari,” alisema Bisiimwa
kwa Kiswahili cha tabu.
No comments:
Post a Comment