Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuzindua rasmi Chuo cha Ushoni cha wajasiri amali wa Kibweni kilichoanzishwa na Jumuiya ya Vijana wa Kibweni { Kibweni Yourth Organization - KYO } katika Mtaa wa Kwa Botoro Kibweni Jimbo la Bububu.
Balozi Seif akiangalia mmoja miongoni mwa wafanuzi wa chuo cha ushoni cha ujasiri amali kiliopo Kwa Botoro Kibweni mara baada ya kukizindua rasmi chuo hicho.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimkabidhi vyarahani Vitano Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa Kibweni Kassim Ali ikiwa mchango wake kusaidia nguvu za nutendji Jumuiya hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi mzima wa Jumuiya
Vijana ya Kibweni pamoja na wadau wao mara baada wa uzinduzi wa chuo cha
Jumuiya hiyo cha Ushoni cha ujasiri amali kiliopo kwa Botoro Kibweni.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema nia ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar ya kuanzisha Wizara inayosimamia sekta ya kazi ni
kuhakikisha kwamba inapambana na tatizo la ajira linaloonekana
kuathiri nguvu kubwa ya Vijana hapa Nchini.
Kauli hiyo aliitoa
wakati akizindua rasmi Chuo cha Ushoni cha ujasiri amali
kilichoanzishwa na Jumuiya ya Vijana ya Kibweni { Kibweni Yourth
Organization } kiliopo katika Mtaa wa Kwa Botoro Kibweni ndani ya Jimbo
la Bububu.
Balozi Seif alisema
hatua hiyo ya Serikali inakwenda samba mba na utekelezaji wa Ilani ya
uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2010 inayoelezea umuhimu wa
kuundwa kwa vikundi vya ujasiri amali ambavyo hutoa fursa kubwa ya
ajira miongoni mwa wananchi.
Alisema kazi za
ujasiri amali zimekuwa zikisaidia kupunguza umaskini na Serikali
itajitahidi kuhakikisha inavijengea nguvu vikundi hivyo vya Jamii ili
viweze kutekeleza majumu iliyojipangia.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar aliipongeza Jumuiya ya Vijana ya Kibweni kwa uamuzi wake wa
kuanzisha Kikundi hicho ambacho ni mkombozi kwa wanajumuiya pamoja na
vijana wa Jimbo hilo.
Hata hivyo Balozi Seif
alihimiza viongozi na wana jumuiya hiyo kuwa wastahamilivu na
kuvumiliana katika harakati zao za kila siku na hatua hiyo aliielezea
kwamba itafanikiwa endapo utaratibu wa kufuata kanuni walizojiwekea
utazingatiwa zaidi.
“ Nimefurahi kuona
Vijana mmejikusanya kuanzisha mfumo wa ajira ambao Serikali kuu kadri ya
hali itakavyoruhusu itazingatia na kutoa msaada unaostahiki ili
kukiendeleza kikundi chenu “. Alisisitiza Balozi Seif.
Alihimiza mpango wa
kuendelea kupanda miti ulionzishwa na vijana hao wa Kibweni ili
kukabiliana na upungufu wa maji uliyoikumba nchi kutokana na tabia za
baadhi ya watu kukata miti ovyo.
Katika kuunga mkono
juhudi za Vijana hao wa Kibweni za kuanzisha Chuo cha Ushoni cha ujasiri
amali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikabidhi
Vyarahani vitano kama mchango wake wa kukipa nguvu Chuo hicho.
Balozi Seif pia
aliahidi kuchangia Kompyuta moja na Mashine ya Kudarzi kwa chuo hicho
hatua ambayo imeungwa Mkono na Mwakilishi wa jimbo la Bububu Hussein
Ibrahim Makungu aliyetoa mchango wa Shilingi Milioni 2,000,000/- taslim
wakati Mbunge wa Jimbo hilo Masoud Sururu ambae ndie mlezi wa Jumuiya
hiyo akaahidi kuchangia Vyarahani Vitano, Pasi na Vifaa vidogo vidogo.
Akisoma Risala ya
wanajumiya hiyo ya Vijana wa Kibweni mmoja wa mwanachama wa Jumuiya
hiyo Farida Juma Haji alisema Vijana wa Kibweni wameamua kuanzisha
jumuiya hiyo wakitambua kwamba Serikali Kuu haina fursa ya kutoa ajira
kwa watu wote.
Alisema elimu ya
ujasiri amali ambayo ni muhimu kwa taifa lolote Duniani ndio itakayowapa
nafasi pekee ya kukabiliana na tatizo hilo la ajira na upande mwengine
jumuiya imelenga kwenda sambamba na mpango wa Taifa wa kupunguza
Umaskini Zanzibar { Mkuza }.
Mapema akikikagua chuo
hicho cha Ushoni cha ujasiri amali cha Kibweni Mwalimu wa chuo hicho
Bibi Subira Haji Yahya alimueleza Balozi Seif kwamba lengo la kuanzishwa
kwa chuo ni kuwajengea mazingira ya ajira vijana wa Shehia hiyo.
Bibi Subira alieleza
kwamba mfumo huo wa mafunzo mbali ya kutengeneza kazi za ajira lakini
pia utasaidia kupunguza wimbi la vitendo viovu wanavyojihusisha zaidi
vijana ndani ya mitaa na kuleta kero na fadhaa kwa jamii.
Chuo cha ushoni cha
ujasiri amali cha Kwa Botoro kilichoanzishwa na jumuiya ya Vijana wa
Kibweni { Kibweni Yourth Organization – KYO } kimeanzishwa karibu miezi
Tisa iliyopita kikiwa na wanafunzi 16 wa rika mbali mbali.
Wanafunzi wa chuo
hicho hupata fursa ya kujifunza ushoni wa nguo tofauti wakianzi na zile
za watoto wadogo kwa hatua ya ukataji na kufuatia ushoni utakaoambatana
na kupatiwa vyeti wakati wanalizapo muda wao wa mafunzo.
Uongozi wa chuo hicho
pia umeweka utaratibu wa kuwarahisishia wanafunzi wake muda wa mafunzo
kulingana na harakati zao za maisha za kila siku ambapo pia hupata wasaa
wa kujifunza lugha ya Kiingereza pamoja na upandaji miti katika maeneo
ya vianzio vya maji vya Mwanyanya.
No comments:
Post a Comment