Tuesday, September 03, 2013

MAJAMBAZI YATINGISHA DAR, YAPORA MADUKA 11

Kundi la watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakiwa na bunduki, wamefunga mtaa na kupora fedha na simu za kiganjani katika maduka 11 eneo la Mvumoni Madale, kata ya Wazo na Tegeta Kibaoni, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Mashuhuda wa tukio hilo, wakizungumza jana na NIPASHE, walisema tukio hilo lilitokea juzi Jumapili, majira ya saa 1:30 usiku.
Hata hivyo, kumekuwa na taarifa za kukanganya kati ya wananchi walioathirika kutokana na mkasa huo ambao wanadai wameporwa simu na fedha kwa viwango tofauti katika maduka 11 huku Jeshi la Polisi likisema kuwa maduka matatu pekee ndiyo yamevamiwa na kuporwa kiasi cha Sh. 300,000.

Katika eneo la Mivumoni Madale kwenye maduka yanayofahamika kama maduka 11, majambazi hao walivamia na kupora kwenye maduka sita.

Neema Charles, muuzaji wa Super Market, alisema akiwa anahudumia wateja alishangaa baada ya watu watatu kuingia na kumrudisha mteja aliyekuwa anatoka ndani na kutoa amri ya watu wote kulala chini na kutoa fedha na simu.

“Kati ya watu watatu walioingia ndani mmoja alivaa kininja akaficha sura, alikuwa na bunduki aliyotumia kupiga watu, walipora simu, pochi, fedha za mauzo na fedha zetu binafsi…nilikuwa na Sh. 250,000 kwenye pochi zimekwenda,” alisema.

Alisema walipekua kila mahali na kupora fedha, simu na pochi huku wakiwatolea lugha ya matusi na kuwataka kila mmoja kunyamaza kimya.

Alisema wakati wanaendelea na kupekua, aliwaangalia na ndipo alichomwa na kitu chenye ncha kali karibu na bega la mkono wa kulia na baada ya kupora walikwenda kwenye maduka mengine na tukio hilo lililochukua dakika 20.

Poni Abdalah, mmiliki wa saluni ya kike, alisema alikuwa anahudumia wateja sita na watoto wanne, mara aliingia mtu mmoja na kuwataka kukaa kimya na kutotoka nje.

“Wakati anatoa amri hiyo mmoja wa wateja alikuwa na mwanaye aliyetoka nje akatoka kumfuata, alivutwa na kusukumwa ndani na tulikaa kimya baada ya kujua tumevamiwa,” alisema.

Alisema jirani yake kuna maduka ya M -pesa na Tigo-pesa nayo yaliporwa kiasi cha Sh. milioni 1.5, na kuwafungia ndani na kuondoka na funguo. Alifafanua kuwa baada ya majambazi kuondoka iliwabidi wavunje mlango ili kumtoa muuzaji aliyefungiwa ndani.

“Baada ya kuona bibi aliyekuwa mteja kwenye duka langu kaporwa simu, nilizima taa ya dukani na kukaa kimya ikawa pona yangu, baada ya dakika 20 nikatoka nje nikakutana na dada mmoja ambaye alikuwa mteja kwenye duka la dawa amenyang’anywa funguo wa gari yake na watu hao,” alisema Amos Joseph.

Katika eneo la Tegeta, mtaa wa Tegeta Ndevu, Mariamu William, alisema majambazi hayo yalifika dukani humo kama wateja na kumtaka kaka yake, Emmanuel William, muuzaji kutoa fedha huku wakiwa wamemshikia bunduki.

“Kabla ya kuamuru wenye maduka kuwapa fedha walipiga risasi mbili hewani, alivyokuwa anachelewa kuwapa walichotaka walimpiga na kitako cha bunduki,” alisema.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema kuwa maduka yaliyoporwa ni matatu katika eneo la Madale mawili na moja ni eneo la Tegeta Kibaoni ambayo yaliporwa kiasi cha Sh. 300,000.

Wambura alisema hana taarifa za kuporwa maduka 11 na kuongeza kuwa polisi wanaendelea kuwasaka majambazi hayo.

MWANAMKE ABAMBWA NA SARE ZA JESHI

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemkamata mwanamke aliyefahamika kwa jina la Saida Mohamed (30), mkazi wa Mwasonga Kigamboni akiwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Kamanda wa kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema jana kuwa mwanamke huyo alikamatwa juzi saa 4:00 asubuhi eneo la Mwasonga Kigamboni, wilayani Temeke.

Kova alisema, mwanamke huyo alikuwa na sare za jeshi hilo ambazo ni suruali saba za kombati, mashati saba ya kombati, kofia 10 za kombati, mashati mawili mepesi, fulana mbili, kofia aina ya bereti moja, viatu jozi tatu, ponjoo moja, koti moja, begi moja la kuwekea nguo za kipolisi pamoja na mikanda miwili ya kijeshi.

Aidha, Kamanda Kova alisema mwanamke huyo anaendelea kushikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano.

Katika tukio lingine, watu wawili wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kukutwa na mihuri 27 na nyaraka mbalimbali za serikali pamoja na za taasisi binafsi wakizitumia kufanyia utapeli kwa wananchi.

Kova aliwataja watu hao kuwa ni Sadraki Mwangwi (27), mkazi wa Mbagala Sabasaba na Samuel Mwangwi (38), mkazi wa Kimara Baruti.

Alisema, waliwakamata watu hao wakiwa na nyaraka hizo wakizitumia kuwatapeli wananchi wa sehemu mbalimbali jijini wakiwa wanakata risiti za serikali kama vile bima za magari, risiti za benki, manispaa na halimashauri. Aliongeza kuwa watu hao walikuwa kama mawakala wa kutoa risiti ambazo wananchi walizihitaji kwa bei yoyote ile.

Kova alisema katika msako huo walifanikiwa kuwakamata watu 120 kwa makosa mbalimbali na kusema msako huo ni endelevu.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment