Sunday, September 22, 2013

Mufti Mkuu wa Oman Awataka Waislam Kuchangia Mambo ya Kheri.

Na Nassor Mussa ZABECS, Pemba

MUFTI Mkuu wa Oman, Sheikh Ahmed Bin Hamed Alkhalily, amewataka waumini wa dini ya kiislamu nchini kote, kutoa mali na nguvu zao kwa ajili ya mambo ya kheri, ili kupata nusra mble ya Mwenyezi Muungu.

Kauli hiyo ameitoa jana mjini Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba baada ya kufungua msikiti mkuu wa Ijumaa (masijid Mwitani) ambapo alisema sio busara kwa Waislamu kutumia mali zao kwa mambo yasio na tija.

Alisema moja na mambo ambayo Waislamu wanapaswa kuyafanya kwa kasi ni kuimarisha misikiti, ambapo kitendo hicho Mwenyezi Mungu ameahidi katika kitabu chake kitakatifu kukizawadia malipo makubwa.

“Sisi Waislamu tunatakiwa tuwe na mapenzi thabiti miongoni mwetu na kujenga tabia ya uadilifu na kuitumia misikiti kwa kufanya ibada za kweli ili siku ya malipo tupate msamaha,” alisema.

Aidha Sheikh Khalily alieleza kuwa, sio busara kuijenga kwa wingi misikiti bila kuitumia na kuitunza.

Alitumia fursa hiyo kusisitiza umoja miongoni mwa Waislamu na kusema amefurahishwa na msikamano ulioneshwa na waumini katika mji wa Wete kwa kujitokeza kwa wingi katika ufunguzi wa msikiti huo bila ya kujali madhehebu yao.

Wakisoma risala yao waumini wa msikiti huo walimshukuru Mfuti hiyo kwa ukarimu wake wa kusaidia harakati za ujenzi wa msikiti huo na kuja kuufungua.

Msikiti huo wenye uwezo wa kuchukua zaidi ya waumini 1500, hautakuwa kwa ajili ya kusali tu bali utakuwa taasisi inayofanya harakati nyingine kama maktaba kwa kuwapatia elimu vijana na kuendesha mihadhara na semina mbalimbali za kidini.

Jengo hilo la msikiti lenye ghorofa tatu lina vyumba vinane vya madarasa vinavyoweza kuchukua wanafunzi 180 kwa wakati mmoja na kati ya hivyo viwili ni vya mafunzo ya kompyuta ambavyo vinaweza kuchukua takribani wanafunzi 30 kwa mkupuo mmoja.

No comments:

Post a Comment