Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi akilifunga Kongamano la Kimataifa la Ustaarab wa
Utamaduni wa Kiislamu afrika mashariki kwenye hoteli ya La Gemma De Est
Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Na Othman Khamis Ame.
Jamii
ya Kiislamu popote pale Duniani inalazima kufanya jitihada za makusudi
katika kuona inaendelea kutumia utamaduni wa Kiislam katika muelekeo
zaidi wa elimu, mawazo ya maendeleo, biashara, uchumi, siasa, sayansi na utawala kwa lengo la kuuongezea nguvu ya ziada.
Hatua
hiyo itawapa muono wa kweli watu wengi wasiokuwa waumini wa Dini hiyo
kuwaondolea shaka kwamba Uislam si kundi la waumini ambao sera zao ni
vurugu, ugaidi na uuwaji mawazo ambayo hata baadhi ya Waislam
wanachangia bila kuelewa.
Makamu
wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Moh’d
Gharib Bilal wakati akilifunga Kongamano la Kimataifa kuhusu Historia ya
Ustaarabu wa Kiislamu katika ukanda wa Afrika Mashariki Hotuba
iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi hapo katika ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya La Gemma Del
Est Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema misikitini mingi siku hizi imekuwa na hotuba za hamasa, jazba , uchochezi na kugeuzwa
kama majukwaa ya kisiasa badala ya kutolewa hotuba za ibada na mafunzo
ya Kiislam yanayohusu kumuabudu Mwenyezi Mungu na mafundisho yake ya
kupenda kufanya mazuri aliyoyaamrisha na kukataa mabaya aliyoyakataza.
Aliwataka
wana jamii wa Utamaduni wa kiislamu kutafakari kwa makini athari hii
iliyojichomoza ambapo isipozingatiwa na kupatiwa dawa maalum inaweza
kumong’onyoa maadili na usaarabu huo wa Kiislamu.
Alieleza
kwamba ipo haja kwa wakati huu kurejeshwa mfumo wa zamani wa kuifanya
Misikiti kuwa ni chimbuko la elimu ambapo ilikuwa mwalimu hukutwa
amezunguukwa na vitabu mbali mbali akiendelea kutoa elimu ambapo nyumba
zao zikijaa baraza kwa kuwa ni sehemu ya Madrassa.
Alifahamisha
kwamba elimu ya dini ilipewa umuhimu wa kipekee ambapo kila mtoto
alijengewa mazingira ya kupata taaluma ya dini kwanza ikifuatiwa na ile ya elimu ya dunia
“
Hakukuwa na mtoto ambaye hakuweza kupata elimu. Vyuo (Madrrassa)
vilienea kila pembe. Vijijini ilikuwa wazazi wakenda kulima mtoto mdogo
anapelekwa chuoni kulelewa na wakubwa zake. Kwa hiyo alianza kupata
hisia za elimu akiwa tangu mdogo “.Alifafanua Makamu wa Raiswa Serikali
ya Jmuhuri ya muungano wa Tanzania.
Dr.
Bilal alisema kwamba Utamaduni wa Kiislam umepata nguvu kubwa kutokana
na msingi wake wa kurithisha vizazi kwa njia ya mashairi, maandiko na
tungo tofauti, hivyo si kosa kueleweka kuwa utamaduni huo umejengwa
chini ya msingi wa elimu kwa vile chimbuko lake linatokana na Qur’aan na Sira za Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad (SAW).
“ Mbali na athari zilizojichomoza lakini bado
utamaduni wa Kiislam unabaki kuwa ni utamaduni wa Kiislam. Una miko
yake, una sifa zake na una matumizi yake. Utamaduni wa Kiislam unaweza
kujisifu kuwa umeweza kusaidia ukuaji wa tamaduni nyingi hasa za Ulaya
“. Alifafanua Dr. Moh’d Gharib Bilal.
Makamu
wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alisisitiza
kwamba Ukuaji wa lugha ya kiarabu kuwa ya Kimataifa ya sayansi na
uendeshaji Serikali umesaidia kuufanya Uislam uwe kiungo cha maendeleo
chini ya msingi wa Quran inayowaagiza waumini kutafuta elimu popote pale
na muda wote wa umri wao.
Amewapongeza
waliowaza kufanya kongamano kama hili hapa Zanzibar na hasa wakati huu
ambao Uislam unapita katika mitihani mikubwa na kuelezea matumaini yake
kutokana na ushiriki mkubwa wa wajumbe utakaotoa maazimio mazuri
yatakayosaidia kupeleka mbele Uislam na ustaarabu wake.
Akisoma
maazimio ya wana kongamano hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya
Kongamano hilo Dr. Juma Halifa Juma alisema wana kongamano hilo
wamependekeza kuendelezwa kwa makongamano hayo kila mara.
Dr
Juma alisema wana kongamano hao walisisitiza umuhimu wa kuandikwa kwa
Historia ya Uislamu wa Afrika ya Mashariki na baadaye kuingizwa katika
mitaala itakayozingatia mfumo wa sasa wa Sayansi na Teknolojia.
Walisema
umuhimu wa kubadilishana utafiti kati ya waislamu wa Afrika na wenzao
wa mabara mengine Duniani unafaa kuzingatiwa vyema ili usaidie
kuimarisha kasi ya utamaduni na Dini ya Kiislamu popote duniani.
Wana
kongamano hao wamemshukuru Mfalme Qaboos Bin Said wa Oman kwa uamuzi wa
Serikali yake kupitia Taasisi zake kuandaa kongamo hilo lililotoa fura
kwa wanafalsafa, wasomi na waumini wa dini ya kiislam kupata
kubadilishana mawazo.
Naye Mwenyekiti wa mamlaka ya
kutunza nyaraka na kumbu kumbu ya Qasri Nchini Oman Dr. Hamad Moh’d Al –
Dhawian Bin Balqas alielezea faraja yake kutokana na michango mikubwa
ya washiriki wa Kongamano hilo hasa wale wenyeji Zanzibar.
Dr.
Hamad alisema utafiti unaonyesha wazi kwamba Afrika Mashariki ni markaz
ya kuleta mabadiliko ya butamaduni wa ustaarabu wa Kiislamu hapa
ulimwenguni.
Akimaribisha
Mgeni rasmi Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Juma
Shamuhuna alisema Zanzibar imepata heshima na bahati kubwa ya kuteuliwa
kuwa mwenyeji wa kongamano hilo jambo ambalo litaijengea historia ndefu
katika masuala ya utamaduni wa ustaarabu wa kiislamu Duniani.
Jumla
ya nyaraka 60 zilijadiliwa katika kongamano hilo lililosheheni
wataalamu, wasomi, watafiti na hata wanavyuoni wa dini ya Kiislamu
kutoka pembe mbali mbali za Dunia.
Kongamano
hilo la pili la Kimataifa la ustaarabu wa Kiislamu likitanguliwa na
lile llililofanyika Uganda mwaka 2012 na limeshirikisha Mataifa kumi na
saba mbali mbali Duniani likiwa na lengo la kujitanga za Zanzibar katika
Nyanja za Utafiti na Taaluma Kimataifa.
Serikali
ya Oman kupitia ushirikiano wa mamlaka ya kumbu kumbu na nyara ya Nchi
hiyo ndio iliyoandaa kongamano hilo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha
Taifa Zanzibar { SUZA }.
No comments:
Post a Comment