Rais
Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwafurahia wasanii chipukizi Gosbert
Bwere(4) anayepiga ngoma na mwenzake Nyambari Mganga(5) walipokuwa
wanamtumbuiza muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa
Nansio,Ukerewe kwa ziara ya kikazi.Rais Kikwete yupo Mkoani Mwanza kwa
ziara ya kikazi(picha na Freddy Maro)
………………
Na Salvator Rweyemamu, Mwanza
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa siyo kazi ya Serikali kuviokoa vyama vya ushirika kutoka
kwenye madeni kwa sababu shughuli za ushirika ni za sekta binafsi na
mali ya wanachama wenyewe.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa makosa ya
ushirika na wezi wa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika hatimaye
yanabebeshwa vyama vya siasa.
Kama
namna ya kuwasaidia wananchi, Rais Kikwete amewataka viongozi mbali
mbali wa mikoa kuwasaidia wananchi ili kupata viongozi waadilifu na
waaminifu na wala siyo wezi kama ilivyo sasa kwa vyama vingi vya
ushirika.
Rais
Kikwete ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo, Jumamosi, Septemba 7, 2013,
wakati alipopokea Ripoti ya Maendeleo ya Mkoa wa Mwanza kwenye Ikulu
Ndogo mjini Mwanza kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano
mkoani humo.
Rais
Kikwete aliwaambia viongozi hao wa Mkoa wa Mwanza: “Tumewahi huko nyuma
kulipa madeni yote ya vyama vya ushirika. Nia ilikuwa kuvisaidia vyama
hivyo na wanachama wake kujipanga upya na kupata uhalali wa kuweza
kukopa fedha za kjuendesha shughuli zao. Lakini sasa, vyama hivyo,
vimerudi kule kule kwenye madeni.”
Alitoa
mfano wa Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Pwani kama moja ya vyama vya
ushirika ambavyo madeni yake yalilipwa na Serikali lakini sasa kina deni
kubwa zaidi kuliko hata lile lililolipwa na Serikali.
“Wale
watu wa Pwani walikwenda kukopa na benki moja ikakubali kuwapa fedha.
Wameshindwa kulipa na ule ushirika nadhani utakufa. Njia bora kwa vyama
vya namna hiyo ni kuviachia vife tu kwa sababu havina faida yoyote kwa
mkulima.”
Aliongeza:
“Vyama vya ushirika siyo mali ya Serikali. Ni mali ya wanaushirika na
hivyo ushirika ni sekta binafsi. Lakini hakuna shaka kuwa baadhi ya
viongozi wa vyama vya ushirika wanatesa wananchi. Wanakopa fedha kwenye
mabenki lakini wanashindwa kuzirudisha fedha hizo na hilo linapotokea
Serikali inalaumiwa kwa hali hiyo.”
Rais
alikuwa anatoa maelekezo yake baada ya kuambiwa kuwa Chama cha Ushirika
cha Nyanza cha Mkoa wa Mwanza kilikuwa kinakamilisha mpango wa kukopa
kiasi cha sh bilioni saba kutoka Benki ya Raslimali Tanzania (TIB) kwa
ajili ya kununulia pamba.
Lakini
aliwaambia viongozi hao: “Uamuzi wa kukopa ama kutokukopa ni wa kwenu.
Nyanza ni mali yenu, wezi waliopata kukibebesha madeni chama hicho
mliwachagua nyie wenyewe. Fedha ni zenu lakini hatimaye athari za makosa
yenu yanaiathiri Serikali na hata vyama vya siasa.”
“Kuna
wakati viongozi wa Chama cha Nyanza walipata kuuza godown ya thamani y
ash milioni 600 kwa sh milioni 50 tu. Hawa ni wezi wa mchana wanaoiba
kweupe. Wanaiba lakini wanataka Serikali iwasaidie. Kwa nini? Nadhani
kazi yetu kama viongozi ni kuwasaidia wananchi kupata viongozi adilifu
na aminifu siyo wezi,” alisema Mheshimiwa Rais Kikwete na kuongeza:
“Tatizo
ni kwamba hata sisi viongozi tunakataa kuwashughulikia wezi kwa sababu
hawa ni watu maarufu na wakati mwingine baadhi ya viongozi wanakula nao
na jambo hilo limekuwa tatizo kubwa sana. Tunavifikisha vyama vya
ushirika mahali ambako sina uhakika kama bado ni mali ya wakulima.
Wakulima wanakutana na ushirika wakati wa kuchagua viongozi tu na baada
ya hapo wakulima hawaonekani tena.”
No comments:
Post a Comment