Wanafunzi
wa kike wa Vyuo vya Mafunzo na Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) wametakiwa
kutoogopa kusoma masomo magumu yanayosomwa na watoto wa kiume kwani
hata wao wanauwezo wa kufanya hivyo na kwa kujifunza kwao fani hizo
wataweza kupata ajira kirahisi.
Wito
huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa uzinduzi
wa awamu ya pili ya mradi wa VETA kwa ajili ya sekta ya gesi na mafuta
ya petroli wenye madhumuni ya kuimarisha ajira kwa vijana kupitia
ufundi stadi uliofanyika katika chuo cha VETA mkoani Lindi
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) akiwa chuoni hapo alitembelea karakana ya chuo hicho na kujionea
wanafunzi wakijifunza kwa vitendo ufundi wa magari, umeme, useremala
na masomo ya kompyuta wanafunzi wote katika madarasa hayo ni wa kiume
kasoro darasa la ufundi umeme ambako alimkuta mwanafunzi wa kike mmoja.
Pia
katika darasa la kompyuta kulikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wa kike
hii inaonyesha kuwa wanafunzi wengi wa kike wanapenda kusoma masomo ya
ukatibu mahsusi (muhtasi) ambayo wanaona kuwa ni rahisi kwao na
kuyakimbia yale ambayo ni magumu kwa kudhani kuwa hawawezi kusoma.
“Chuo
cha VETA Lindi kina jumla ya wanafunzi 224 kati ya hao wasichana ni 63,
kutokana na upatikanaji wa rasilimali zilizopo katika mikoa ya Kusini
Shirika la Madini limefadhili wanachuo 64 kati ya hao wasichana ni 11
mimi kama mzazi na mdau wa maendeleo wa mkoa huu nauliza tuko wapi na je
tutafika?, alihoji Mama Kikwete.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA alisema makusudio ya VETA ni kuona kijana akimaliza
mafunzo yake anaweza kujiajiri lengo likiwa ni kuwaondoa vijana wengi
kutoka kwenye eneo lisilo la ajira na kupata ajira kwani si lazima mtu
aajiriwe ofisini na kuwataka wasome kwa bidii ili waweze kufika mbali.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa huo Ludovick Mwananzila alisema ugunduzi wa
gesi katika mikoa ya Kusini ni kitu kipya nchini hivyo basi wananchi
bila ya kupewa mafunzo fani hiyo inaweza kutoweka.
Alisema
chuo hicho kama kitatumika vizuri kitakuwa ni mkombozi mkubwa kwa
wananchi wa mkoa huo na kuwaomba wazazi kuwa tayari kuwapeleka watoto
wao choni hapo kwani wataweza kuajiriwa au kujiajiri wenyewe pindi
watakapomaliza mafunzo yao na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha.
Mkurugenzi
Mkuu wa VETA nchini Mhandisi Zebadiah Moshi alizishukuru kampuni za
British Gas ya Uingereza ambao wametoa mchango wa kuimarisha mafunzo
kwa wanafunzi katika vyuo vya Lindi na Mtwara na Voluntary Services
Organisation (VSO Tanzania) ambao ndiyo wanaratibu mafunzo hayo.
Mhandisi
huyo alisema chuo hicho ndicho kinachonufaika zaidi na mafunzo hayo
kwani yataboresha mafunzo ya elimu kutokana na ushirikiano uliopo,
walimu watajengewa uwezo katika mafunzo na wanafunzi watakaomaliza
katika vyuo hivyo watakuwa na umahiri mkubwa zaidi.
Alisema,“Vyuo
vyetu vitapata vifaa vya kisasa vya kufundishia na mafunzo haya
yatakuwa ya kiwango kizuri. Tunaahidi kuimarisha uhusiano uliopo na
tutasimamia na kuhakikisha kuwa uhusiano huu unatimiza malengo
yaliyokusudiwa”.
Kwa
upande wao baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho kutoka Mtwara na Lindi
ambao walitoa ushuhuda jinsi walivyoweza kunufaika na mafunzo ya VETA
walisema watu wengi wanaposikia kijana anaenda kusoma hapo wanamdharau
na kuona kuwa ameshindwa kila kitu katika maisha na kukimbilia huko
jambo ambalo si kweli kwani mafunzo wanayopewa ni mazuri na
yanawasaidia katika maisha yao.
“Tunaiomba
Serikali iongeze idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo hivi hii
itawasaidia vijana wenzetu ambao tunakutana nao mitaani kipindi cha
likizo, vijana hawa ni wengi na hawana ajira ili nao waweze kupata elimu
kama hii tunayoipata sisi kwani pindi wakimaliza mafunzo yao wataweza
kujiajiri au kuajiriwa”, walisema wanafunzi hao.
Mradi
huo ambao ni wa miaka miwili kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 umeanzishwa
na kuendelezwa na kampuni ya British Gas ya Uingereza, Voluntary
Services Organisation (VSO Tanzania) , wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi, Serikali ya Uingereza kupitia idara yake ya Maendeleo ya
Kimataifa(DFID) British Council na VETA utatoa mafunzo kwa zaidi ya
wanafunzi 224 kutoka kwa walimu wenye uzoefu wa kimataifa kwa
kushirikiana na walimu wao na kukifanya chuo hicho kufikia viwango vya
kimataifa.
Pia
utaboresha matumizi ya lugha ya kiingereza kwa walimu 15 kwa sababu
vijana watakaowafundisha wanatarajiwa kuajiriwa katika makampuni ya
ndani na ya kimataifa, hivyo lugha ya kiingereza ni nyenzo muhimu ya
mawasiliano na walimu wanne kutoka karakana nne za chuo hicho
watajengwa uwezo kwa kupewa kozi zenye hadhi ya kimataifa ili wapate
tuzo zinazotambulika kitaifa.
Awamu
ya kwanza ya mradi huo ulizinduliwa mwishoni mwa mwaka 2012 katika chuo
cha Ufundi VETA Mtwara na Makamu wa Rais Dk. Gharib Bilal.
No comments:
Post a Comment