Bismillahi twanza kwa jina la Mola Rahman, aliye Rahim. Mwingi wa rehema na mkarimu, mwenye hazina isiyoisha asilani, Ar-Razzaq.
Al-Habib
As-Sayyid Umar Abdallah bin Abi-Bakar bin Salim ama kwa umaarufu wake
Mwinyi Baraka (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie yeye na wazee wake),
shekhe wa mashekhe zetu na ruwaza ya nyoyo zetu, ni kioo cha ilmu na
tarika kwa watu wa Afrika Mashariki.
Al-Habib
Umar Abdallah ndiye aliyemjazi Shaykh wetu kipenzi as-Shaykh Al-Faqeer
Ahmad bin Muhammad bin Shaykh Msiha (radhi za Mwenyezi MUngu zimwalie)
tarika Qadiriyyah na tarika ya mabwana wetu watukufu wa Hadhramut wa
Ba'Alawi.
Katika
kurasa hii tutaandika kwa ufupi juu ya mtukufu wetu huyu aliyezaliwa
huko Zanzibar mwaka 1917 na kufishwa huko Ngazija (Commoros) mwaka 1988,
ambapo ndio ilipo rawdha yake tukufu. Nasabu yake al-Habib Umar inarudi
kwa Bwana wa viumbe na wana wa Adamu, sala za Mwenyezi Mungu na salamu
zake zimshukie na Aali zake na Sahabaze. Kwa upande wa baba yake nasabu
yake inapita kwa Sayyidina Abi-Bakar bin Salim na upande wa mama ni
Jamali-Llayl.
Al-Habib
Sayyid Umar Abdallah, alibobea katika ilmu zote mbili, yaani ilmu ya
dini na ilmu ya skuli. Allianza kusoma ilmu ya dini angali mdogo kutoka
kwa Ami yake Sayyid Abdul-Fattaah bin Ahmad Jamali-Llayl (maarufu
Shariffu Abudu, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie) ambaye ndiye aliyekuwa
mlezi wake baada ya kufiliwa na wazee wake. Sayyid Abdul-Fattaah pia
ndiye aliyekuwa wa kwanza kumwingiza Habib Umar katika tarika Qadiriyyah
kama alivyobainisha kwenye ijaza aliyowajazia muridi wa al-Majalis
el-Ulaa.
Mwaka
1940, Mwinyi Baraka alijiunga na Makerere University kusoma ilmu ya juu
na mwaka 1951 alijiunga na School of Oriental and African Studies
(SOAS), London ambapo alisoma Arabic na Islamic Law. kati ya walimu wake
wakiwemo M.Cowan na J.N.D. Anderson. Mwaka 1961 Habib Umar Abdallah
alijiunga na Oriel College, Oxford na kuchukua BA in Islamic Studies.
Katika thesis yake Al-Habib aliandika juu ya falsafa ya kiisilamu,
angalia kitabu cha Felicity ambacho kimetolewa na Majaalis Qadiriyyah
Mwinyibaraka Uwesiya.
Habib
Umar Abdallah alisoma kwa mashekhe wengi waliobobea katika ilmu mbali
mbali huko Unguja na Shaykh wake mkuu kabisa alikuwa Al-Habib As-Sayyid
Umar bin Ahmad bin Abubakar bin Sumayt (radhi za Mwenyezi Mungu ziwaalie
wote), mwanazuoni wa wanazuoni na shekhe wa mashekhe zetu. Alimlazimu
pia Shaykh Sulayman bin Alawy, mwanazuoni mkubwa kabisa aliyekuwa na
mapenzi makubwa kwa bwana Mtume na Aalil-Bayt, sala na salamu za
Mwenyezi zimshukie Bwana wetu na watu wa nyumba yake. Shaykh Sulayman
al-Alawy (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) ndiye aliyeshika nafasi ya
Al-Habib Umar bin Sumeyt, Al-Habib alipoihama Unguja na kurejea Ngazija,
rawdha yake bwana huyu mtukufu ipo huko Ngazija na kila mwaka hufanywa
hawl kubwa huko na wapenzi wake kukusanyika kwa wingi toka kila pembe ya
dunia, Mwenyezi Mungu atunufaishe nae. Mengi juu ya matukufu ya mabwana
hawa wawili, yaani Al-Habib Umar na Shaykh Sulayman (radhi za Mwenyezi
Mungu ziwaalie) yamo mbioni kuchapwa na mmoja wa mashekhe zetu, na
Mwenye Enzi amjaliye kuyafanikisha hayo.
Habib
Umar Abdallah alikuwa ni mwingi wa safari na kila alipokwenda
ulimwenguni hakuacha kufanya Da'awa na kutafuta wanazuoni wa miji hiyo
na kuchukua ilmu kutoka kwao. Miongoni mwa wanazuoni aliochukua ilmu
kutoka kwao ni Sayyid Abdul-Rahman bin Ubaydillah wa Hadhramut, Sayyid
Alawi al-Maliki wa Makka, Sayyid Alawi al-Haddad wa Malaysia na wengineo
wengi.
Habib
Umar Abdallah amepokea ijaza ya tarika Qadiriyya kutoka kwa mashekhe
tofauti wa nchi mbali mbali. Miongoni mwa mashekhe waliompa ijaza na
u-Khalifa wa Tarika hii tukufu ni mjukuu wa Sayyidina Abdulkadir Jailani
(Qudusu Sirru), Sayyid Tahir Allaudin (radhi za Mwenyezi Mungu
zimshukie) aliyekuwa msamizi wa rawdha ya Al-Gawth Azzam huko Baghdad
kabla ya kuhamia katika nchi ya Pakistan. Zaidi kuhusu Sayyid Tahir
angalia tovoti ya wanafunzi wake, www.yamurshid.com
Hapa
tumedondoa kwa uchache kuhusu Habib Umar Abdallah Mwinyi Baraka, kwa
undani zaidi wa maisha yake na matukufu yake, haya Insh-Allah kwa idhini
yake Subuhanna-wa-Taala yamo mbioni kuandikwa katika kijitabu na mmoja
wa mashekhe zetu. Basi tuwe na subira na Mola amjalie mwandishi uwezo na
nguvu na uhai na afiya kuyaandika hayo ya Habib wetu nasi Insh-Allah
tupate kuelimika kwa hayo. Labda kwa kufungia haya machache tunukulu
maneno ya Imam wa Makka wa wakati wake, Shaykh Bin Baaz. Katika kijtabu
kilicokusanywa na al-Habib al-Faqeer Shaykh Ahmad juu ya safari za
al-Habib ulimwenguni, kiitwacho Mwinyi Baraka katika Ulimwengu wa
Uislamu, al-Faqeer Shaykh Ahmad ananukulu maneno haya:
Akielezea
mwenyewe Al-habib kuwa kila alipokua Makka iliyonawirika, al-Marhumm
Bin Bazz alikuwa akimtanguliza… “Umar swalisha”. Akimwambia: “Bwana
Mtume sala za Mwenyezi Mungu na salamu zimshukie, akisema,
Ahli-shsharafaa laa Ahli-sharaf watu wa Sharaf hupitana kwa Sharaf.
Walaa Yaa arifa Ahli sh-sharaf, wala hawawajui watu wa Sharaf, Illa
Dhawish Sharaf, ila ambao ni watu wa Sharaf”. Kijitabu kilichotajwa hapo
juu kinapatikana katika tovoti ya www.al-faqeer.com
Maneno
hayo ni kweupe kabisa na wala hayahitaji kuyaeleza wa urefu. Huyo ndio
al-Habib Umar Abdallah bin Shaykh Abi-Bakar bin Salim (radhi za Mweneyi
Mungu zimshukie).