Thursday, August 01, 2013

Wasifu wa AL-HABIB SAYYID AHMAD BIN HUSSAIN BIN SHAYKH ABI-BAKAR BIN SALIM, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie.

Wasifu wa AL-HABIB SAYYID AHMAD BIN HUSSAIN BIN SHAYKH ABI-BAKAR BIN SALIM, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie.
Syd.Ahmad bin Hussein 1Bwana wetu Abdul-Qadir Bin Abdulrahman Bin Umar Al-Junaid – Radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie – alipokuja kumzungumza Bin Hussain kwenye kitabu chake Al Uqud Al Jaahiza, alimwita Raihana ya Mji wa Unguja. Na Shekhe Mkuu wa Mashekhe zetu, al-Habib Umar Bin Abi-Bakar Bin Sumeit, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie, alimwita Bin Hussain kwenye barua: “Man Qarat Bihi Ain Kulli Zein,” yaani yule ambaye jicho la kila mzuri limefurahi upeo kwaye. Habib Abdulqadir na Habib Umar hawatofautiani kwa jinsi wanavyomuona Bin Hussain. Na maneno wanayotumia kutoka wasifu wake ni matamko ya shangazi na mjomba. Na Bwana wetu Sayyid Umar Abdallah, (Mwinyi Baraka) alisema hivi kumhusu Bin Hussain na ucha Mungu wake, “Alifikishwa daraja ya kumcha Mungu saa ishirini na nne.”  
Ho, tusijiache na fahamu ya kawaida ya tamko hilo, kwani Sharif Junaid, umashuhuri wake, alikuwa akipiga mbali. Tamko Raihana, katika tangamano kama hili alilitumia kwa mara ya mwanzo Shekhe Mkubwa wa Tariqa na Haqiqa, naye ni Al-Junaid wa Baghdad. Alilitumia kwa Bwana Ahmad Bin Abi Hawari – Radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie . Na maana yake ni yule Walii mkubwa ambaye wengine, kwa kusikia uturi wa harufu yake, hupata jazba na hamasa ya kushamiri kuwania Maqamati za juu na juu tena. Na hapa tunazungumza malimwengu ya mbali zaidi kuliko Arshi
Na mwahala pengine al-Habib Umar Bin Sumeit akimtaja Bin Hussain kuwa: “Ni al-Habib ambaye yeye mzima, wote ni nuru.”
Unguja, na sasa tunasikia Daresalaam pia, kunafanywa Hadhara ya Bau-Saudan, yaani Hadhara ya Ajabu ya Zama, Sheikh Abdallah Bin Ahmad Bin Abdallah Bin Muhammad Bin Abdur-Rahman Bin Muhammad Ba-Saudan – Mwenyezi Mungu atunufaishe naye na elimu zake. Katika kitabu chake kinachoitwa Hadaaiqi-l-Arwaa, yaani Bustani ama Vitale vya Roho, anazungumza kile tutachokiita ‘Ngazi za dhikri’. Anataja ngazi moja, na hiyo anaita ‘Sultani wa dhikri’. Yaani dhikri ya mwili, mwili wote, nje na ndani, kiungo kwa kiungo, kia kwa kia, mshipa kwa mshipa, damu na nyama na nywele. Ni dhikri adhimu kweli hii, na ndiyo inayoashiriwa kwenye dua ya Bwana Mtume SallaLLahu ‘Alayhi Wasallam anaposema: “Ewe Allahumma, Jaalia kwenye moyo wangu nuru, na kwenye usikivu wangu nuru, kwenye macho yangu nuru...”, mpaka mwisho wa dua. “Hakika”, anasema Sheikh Abdallah Ba-Saudan: “Mwili wote, nje yake na ndani yake, na pande zake sita, zinataka nuru hii adhimu. Na Mashekhe wengi hawataji dhikri nyingine iliyo juu ya hapo. Ukweli wa mambo, hali haiko hivyo. Ukweli ni kwamba, Sultani ya dhikri ina mwanzo na mwisho.”
Sheikh Ahmed Islamu, mojawapo kati ya watu waliokuwa wakishikamana sana na Bin Hussain, anasema kwamba Bin Hussain alikuwa wote makini tupu alipokuwa akiisoma ile dua ya Al-Murshidul Kamil, al-Habib Ali Bin Muhammad Bin Hussain Al-Habshi inayoanza kwa maneno haya:Allahumma Salli wa Sallim Billisaani-l- Jamia, Fi-l-Hadharati-l-Wasia, ‘Alaa Abdika-l-Jamia, Li-l-Kamaalaati-l-Insaniyyah...na humo, al-
Habib Ali Al-Habshi anaomba nuru hii hii aliyoomba Bwana Mtume SallaLLahu ‘Alayhi Wasallam, ambayo Sheikh Abdallah Ba-Saudan anaiita: Sultani wa dhikri zote.
Syd.Ahmad bin Hussein 2Hebu tutue. Hebu tumakinike makini. Tuangalie tena wasifu wa al-Habib Umar Bin Sumeit juu ya Bin Hussain. Yeye kamwita kuwa “al-Habib ambaye yeye wote mzima ni nuru”. Mwinyi Baraka akipenda kusema, kuwa al-Habib Umar Bin Sumeit alikuwa na kipawa kuwa anapotumia neno, basi hilo ndiyo ndilo. Halina badili. Yeye kamwita “ni nuru wote.” Sheikh Abdallah Ba-Saudan anasema hiyo ni hali ya mtu aliyefika daraja ya Sultani-l-Adhkar. Na ina mwanzo na ina mwisho. Sharif Junaid anamweleza Bin Hussain kwa kuwa ni mtu ambaye ukikutana naye, hali yake ni yule aliyeghibu katika malimwengu ya dhikri. Hiyo si hali ya mtu aliyekuwa mwanzo mwanzo wa Sultani-l-Adhkar. Ni alama ya mtu aliyoko kwenye daraja za juu.
Wasifu huu wa al-Habib, as-Sayyid Ahamd bin Hussain ni kutoka katika sherhe ya Ratib al-Attas, uradi ambao bwana wetu Bin Hussain aliupa umuhimu mkubwa . Sherhe hiyo iitwayo Lulu na Almasi ipo mbioni kuchapwa.

                                          KWA MAKALA NYINGI ZAIDI TEMBELEA