Wasifu wa Habib Ahmad Mash-hur
WASIFU AL-HABIB AS-SAYYID AHMAD MASH-HUR BIN TAHA AL- HADDAD, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie.
Al-Habib
Ahmad Mash-hur.... al-Habib Ahmad Mash-hur. Ni jina lenye kutia ladha
kinywani. Kama bwana wa Jailani, ambaye ana nasabu naye ya tarika na
khirqa, bwana huyu alikuwa ni bwana wa shani. Si sisi wa kumweleza, hata
ikasemwa kwamba kaelezwa. Letu sisi ni kurudi kwa wale ambao
wanatambulika kwamba wanaweza kumzungumza.
Sisi
tumeamua kurudi kwa mwanazuoni wa wanazuoni wa zama zake na Bwana wa
Msikiti Gofu na Ukutani na naibu wa al-Habib Umar bin Ahmad bin
Abi-bakar bin Sumayt. Huyo ni Shaykh Sulayman bin Muhammad bin Said
al-Alawy, radhi za Mwenyezi Mungu zimwaalie yeye na ma-Shekhe zake.
Kwenye ijaza ndefu, kamweleza hivi Habib Ahmad Mash-hur:
“Na
katika wale ambao nimemshika miguu yake, nikanywa utamu wa mashrabu
yake, al-Habib ambaye kakwea makweo ya kuhakiki mambo, akanywa shibe
yake, ..... taa ya uongofu na mwenye kukwatua kutu za moyoni, mwana wa
ma-Qutb na ma-Awtaadi na Ghawth wa miji na mawandani, mwanazuoni wa
wanazuoni, mtukufu Ahmad Mash-hur bin Taha al-Haddad. Nimejumuika naye
na nikaujaza moyo wangu pendo lake na nikapamba masikio yangu kwa johari
za hikma zake, na nikamlazimu huku nachukua nuru za nasari yake na
mashahiri yake na ikasihi kwangu kutokana na Habib huyu mapenzi
yanayotokea kwa ajli ya Mwenyezi Mungu hata nikasiri mimi kuwa natajwa
kwa jina la rafiki yake na mpenzi wake. Nataraji kwa Mwenyezi Mungu kuwa
ataninufaisha naye hapa duniani na Akhera, pamoja na watoto wangu, na
wapenzi wangu, na ndugu zangu, na wale waliotaalaki nami, na zitanirejea
mimi baraka za Sayyid huyu adhimu, baraka za baba zake na wazee wake wa
kale, na ambazo zitanipa mimi sifa za usahihi wa kuwa mimi ni Salman
wao.”