UFUNGUZI WA KONGAMANO LA HISTORIA YA UISLAMU AFRIKA MASHARIKI
NA RAMADHANI ALI/HABARI MAELEZO ZANZIBAR
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi Dkt. Ali Muhammed Shein
amesema Historia inaonyesha kuwa Zanzibar imechangia sana katika kukuza
na kueneza ustaarabu wa kiislamu katika maeneo ya Afrika Mashariki.
Amesema
Masheikh na Maulamaa wa Zanzibar walikwenda kueneza Uislamu katika
maeneo ya Ukanda huo na wengine walifika visiwa vya Comoro na nchi
nyengine za Afrika ya Kaskazini na baadhi ya nchi za Asia.
Dkt.
Shein ameeleza hayo alipokuwa akifungua Kongamano la Kimataifa kuhusu
Historia ya Ustaarabu wa Kiislamu katika nch za Afrika Mashariki
linalofanyika katika Hoteli ya Lagema, Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema
anaamini kuwa kutokana na Historia na vigenzo vyengine vingi ndio
viliopelekea Mamlaka ya Kumbukumbu na Nyaraka ya Falme ya Oman
kuichagua Zanzibar kuwa mwenyeji wa kongamano hilo la Kimataifa la
kiislamu kwa nchi za Afrika Mashariki.
“Kwa
hakika Zanzibar ndiyo kitovu cha Historia ya Ustaarabu wa Kiislamu
katika nchi za Afrika Mashariki, hivyo kuichagua Zanzibar kuwa mwenyeji
wa kongamano hili ni pahala pake,”alisisitiza Dkt. Ali Muhammed Shein.
Amongeza
kuwa yapo maelezo ya kihistoria yanayoeleza kwamba msafara wa viongozi
wa dini ya kiislamu ukiongozwa na Sayyid Jaffar bin Abu Talib waliingia
Zanzibar na kufikia kijiji cha Ndagoni Pemba kabla ya viongozi wengine
wa dini kuingia Madina.
Amesema lugha
ya Kiswahili imekuwa chombo muhimu cha kueneza na kuendeleza
ustaarabu na mafundisho mengine ya dini ya kiislamu kupitia mawaidha,
darsana pia tafsiri za vitabu vya dini ya kiislamu katika ukanda wa
Afrika Mashariki.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amesema kuwa ithibati
ya kuingia dini ya kiislamu Afrika Mashariki katika karne ya
tisa ni mabaki ya baadhi ya misikiti iliyojengwa katika karne ya kumi
na kugunduliwa kwenye baadhi ya maeneo ya miji ya kale ya Zanzibar
ikiwemo Unguja Ukuu Kae Pwani kwa Unguja na Mtambwe mkuu kwa upande wa
Pemba.
“Kadhalika msikiti
mkongwe wa Kizimkazi Dimbani ni kumbukumbu isiyo na shaka,
inayobainisha wazi kuwa Zanzibar ilikuwa na idadi kubwa ya waumini wa
dini ya kiislamu katika kipindi cha mwishoni mwa karne ya 11 AD na
kuingia karne ya 12 AD,”alisema Rais Shein.
Amebainisha
Uislamu unafaida kubwa katika kuimarisha na kuendeleza Utamaduni na
maisha ya kila siku na umekuwa ukijitokeza katika masuala mbali mbali
yakiwemo mavazi, malezi, vyakula, elimu, sheria na utawla, shughuli za
mazishi ndoa na hata sanaa katika ujenzi wa nyumba za kale.
Dkt.
Ali Muhammed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inatambua mchango muhimu unaotolewa na Taasisi za kidini na ndiyo sababu
ya kuanzisha Ofisi ya Mufti kusimamia masuala ya kidini ikiwa ni pamoja
na kuziendeleza madrasa na kuyaendeleza malezi ya watoto.
Amesisitiza
haja ya kuimarisha Umoja na kuepuka mifarakano katika jamii na pia
amewataka waumini wa dini ya kiislamu kuishi vizuri na waumini wa dini
nyengine duniani kote.
“Uislamu
ni dini ya amani na kwa hakika mifarakano na vitendo vinavyohatarisha
amani na Ustawi wa Jamii si sehemu ya Ustaarabu wa Kiislamu.”
alisisitiza Rais wa Zanzibar.
Rais
wa Zanzibar amelitaka kongamano hilo liwe chemchem ya tafiti zaidi za
Historia ya Ustaarabu wa Kiislamu Afrika Mashariki na kuzingatia
uwezekano wa kuanzisha kituo cha Historia na Utamaduni wa Kiislamu
Zanzibar.
Akizungumza
katika Kongamano hilo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu
Duniani (OIC) Dkt. Emeleddin Ihsan amesema uislamu ni dini inayosisitiza
amani na maelewano duniani.
Hata
hivyo a mesema hivi sasa imezuka dhana ya kupigwa vita na kuonekana
kama ni dini hatari inayozalisha magaidi jambo ambalo sio la kweli.
“Dini
ya kiislamu inapinga ugaidi na ni dini ya usalama inayosisitiza amani
na maelewano ili kuishi kwa usalama duniani kote hivyo tusikubali
baadhi ya watu wanaoipiga vita dini hii, ”Dkt. Ihsan alisema.
Kongamano
hilo la siku tatu linatarajiwa kumalizika Jumatano ijayo ambapo Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Muhammed Gharib Bilal
atakuwa mgeni rasmi siku ya ufungaji.
No comments:
Post a Comment