Monday, October 21, 2013

Maalim Seif: Tulinde mila, silka na utamaduni wa Mzanzibari

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Naibu Kadhi Mkuu Sheikh Hassan Othman Ngwali (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Pemba Juma Khamis wakimsalia Mtume katika hafla ya Maulid yaliyofanyika Tumbatu Jongowe. (Picha na Salmin Said, OMKR).
Na Khamis Haji, OMKR 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amewahimiza wananchi wa Zanzibar kuungana katika kulinda na kuhifadhi utamaduni, mila na silka za Wazanzibar, ili kuepusha tabia ya kuipotosha kwa makusudi inayofanywa na baadhi ya watu.  
Maalim Seif ameyasema hay oleo, wakati alipokuwa akihutubia katika hafla ya Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), yaliyoandaliwa na Madrasat Nur Islamiya huko katika kijiji cha Tumbatu Jongowe, Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.
Amesema utamaduni na mila za Wazanzibari ni za kipekee na vuimerithiwa kwa miaka mingi, lakini baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kuvipotosha kwa malengo maalum, jambo ambalo linapaswa kupigwa vita na wananchi kulikataa.
Amesema historia ya Zanzibar ina mafungamano makubwa na Dini ya Kiislamu kwa zaidi ya miaka 1000, hali ambayo inathibitishwa na kuwepo maeneo mengi ya kihistoria, ikiwemo msikiti wa Kizimkazi, magofu ya majengo ya asili huko Makutano katika kisiwa cha Tumbatu, pamoja na athari za iliyopo katika eneo la Kihistoria la Mkuu, kisiwani Pemba.
Aidha, Makamu wa Kwanza wa Rais amesema malengo hayo yataweza kufikiwa iwapo Walimu, Masheikh na Wazee watakuwa na tabia ya kuwafunza watoto wao historian a utamaduni wa nchi yao.
Makamu wa Kwanza wa Rais pia ametumia hafla hiyo kuhimiza umoja na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari wote hasa wakati huu wa kutafuta Katiba mpya ya Tanzania, ili kuweza kulinda maslahi na musatakabala mwema wa Zanzibar.
“Tukishikamana tutakuwa wamoja, tutaweza kutetea na kulinda maslahi ya nchi na watu wake, tukigawana na kuweka mbele maslahi binafsi, badala ya kuweka mbele maslahi ya Taifa tutashindwa kuitumia vyema fursa hii”, alisema Maalim Seif.
Katika risala yao wana Madrasa hao wa Nur Islamiya waliwapongeza wananchi na viongozi mbali mbali, kutokana na michango yao iliyowezesha Madrasa hiyo kujengwa katika kipindi kifupi.
Katika risala hiyo iliyosmwa na Maalim Juma Makame, waliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali, pamoja na wananchi wa kijiji hicho katika kuwajenga watoto katika maadili mema, ili wawe wananchi wema wanaoweza kutegewa na Taifa.   
Nae, Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Hassan Othman Ngwali akihutubia katika hafla hiyo, amewahimiza waumini wa Kiislamu kuzidisha bidii katika kumsifu Mtume Muhammad (S.A.W), na kushikamana na mafundisho yake kivitendo.
Maulid hayo ya Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) hufanyika kila mwaka ifikapo mwezi 12 Mfunguo tatu.   
chanzo cha habari : ZanziNews

No comments:

Post a Comment