Na Anna Nkinda- Maelezo, Wanging’ombe
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka kinamama wa wilaya ya Wanging’ombe
mkoani Njombe kusimamia elimu ya watoto wao wa kike ili waweze kusoma
na kufika ngazi ya chuo kikuu kitendo ambacho kitaongeza idadi ya
wanawake viongozi nchini.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) aliutoa wito huo jana wakati akiongea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kipengere wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe.
Alisema
kutokana na historia wanawake walikuwa wameachwa nyuma kimaendeleo
ikiwa ni pamoja na kukosa fursa ya kupata elimu ukilinganisha na watoto
wa kiume hivyo basi ni jukumu la kina mama kusimamia elimu ya watoto wao
ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakwenda shule kwa wakati kwani mtoto
wa kike akiwa na kipato hawezi kumtupa mzazi wake.
“Bila
ya kuwa na elimu huwezi kupata maendeleo kwani elimu ni msingi wa kila
kitu na ukiwa na elimu utaweza kuepukana na matatizo ya ujinga, maradhi
na umaskini kwani ukienda shule utafundishwa mambo mengi
ambayo yatakusaidia katika maisha yako hivyo basi ni muhimu kwa vijana
wakaenda shule ili wapate elimu”, alisema Mama Kikwete.
Kuhusiana
na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwataka
wananchi wa wilaya hiyo kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kwa wale
wenye ndoa kuwa waaminifu kwa wenzi wao na wale wasio na ndoa kuwa na
subira hadi wakati utakapofika na wasikubali kufunga ndoa kabla ya
kwenda kupima kwani kasi ya maambukizi iko juu kwa asilimia 15.3 ukilinganisha na maambukizi ya mkoa ambayo ni asilimia 14.8.
Mama
Kikwete alisema, “Katika wilaya hii pia kuna tatizo la vifo vya kina
mama wajawazito vinavyotokea wakati wa kujifungua ni jukumu la kila
mmoja wetu kuhakikisha kuwa vifo hivi vinapungua kwani si jambo zuri kwa
mama kupoteza maisha wakati akileta uhai wa mtoto Duniani”,.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Njombe Magharibi ambaye
pia ni Naibu waziri wa Ujenzi Mhandisi Gerson Lwenge alimuomba mama
Kikwete awasaidie kina mama wa wilaya hiyo vitanda vya kisasa vya
kujifungulia vitatu ambavyo vitatumika katika vituo vya Afya vya Mdandu,
Makoga na Wanging’ombe na Mama Kikwete aliahidi kulifanyia kazi ombi
hilo.
Taarifa ya wilaya hiyo inaonyesha kuna jumla ya wanafunzi wa sekondari wa kike 4184 toka Januari mwaka
2013 hadi sasa waliokatiza masomo kwa kupata ujauzito ni 12 kwa upande
wa shule za msingi hakuna mwanafunzi aliyepata ujauzito kwa kipindi cha
mwaka 2012/13.
Kwa
upande wa tatizo la vifo vya kina mama wajawazito vinavyotokea wakati
wa kujifungua idadi imepungua kutoka 112 kwa kila vizazi hai 100000 kwa
mwaka 2010 na kufikia38 kwa kila vizazi hai 100000 kwa mwaka 2012.
Vifo
vya watoto wenye umri wa chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka 12 kwa
kila vizazi hai 1000 kwa mwaka 2010 hadi kufikia 6 kwa kila vizazi hai 1000 kwa mwaka 2012.
Mama Kikwete ameambatana na mmewe Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete katika ziara ya kikazi ya siku saba mkoani Njombe ambapo jana Rais Kikwete aliongea na wananchi wa Kijiji cha Kipengere wilayani Wanging’ombe.
Akiwa wilayani Makete Rais
Dk. Kikwete aliweka jiwe la msingi madarasa ya kidato cha tano katika
shule ya Sekondari Lupalilo, kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Zahanati
ya Ivalalila, kuzindua chuo cha VETA na kuongea na wananchi wa wilaya
hiyo.
No comments:
Post a Comment