Monday, June 30, 2014

Ramadan kareem

Karibu mwezi mwema
mtukufu Ramadhani kwa niaba ya wana blog wote WA kijana tunawatakia funga njema.

Saturday, May 24, 2014

YAH MUALIKO WA MAULID YA MTUME MUHAMMAD REHMA ZA MWENYEZI MUNGU ZIMSHUKIE JUU YAKE NA AMANI

Bismillahi Rahmani Rahim

Ungozi wa Madrasatul Amini ya Marhum Sheikh Nassor Amran  Iliopo kwa Ali Maua A Chini ya Uongozi na Usimamizi wa Mudiru Alhaj Sheikh Mohammad Nassor Unapenda Kukualika na Kuwakaribisha Wadau wote na Wapenzi Wa Mtume Muhammmad Rehma za Mwenyezi Mungu zimshukie Juu yake Shughuli hii Itafanyika hapa MADRASANI KWETU KWA RATIBA IFUATAYO  SIKU YA IJUMAA TAREHE 30 / 5 / 2014 Kuanzia Saa 4 Asubuhi Maonyesho ya Wanafunzi na Baada ya Swala ya ISHAAI MAULIDI YA JUMUIA  
MASHEIKH NA WAALIKWA KUTOKA SEHEMU MBALIMBALI WATAHUDHURIA NAWE TUNA KUKARIBISHA KUUNGANA NASI KATIKA JAMBO HILI.
Watendaji wa Kuu na Waratibu wa Shughuli hii MAPACHA  NA WAPENZI WA MTUME MUHAMMAD REHMA ZA MWENYEZI MUNGU ZIMSHUKIE JUU YAKE NA AMANI KATIKA Moja ya hafla kama inayo tarajia fanyika Siku ya Ijumaa.


Kwa Mdau yeyote Ambae atahitaji kuchangia Baadhi ya Vifaa kama Maji , Juice N.k Unakaribishwa Ujachelewa.

KWA MAWASILIANO ZAIDI WASILIANA NA 0713526494 / 0712257492 0715800772.

Wednesday, December 25, 2013

RAIS KIKWETE AKUTANA NA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki Moon akimkaribisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwenye ofisi yake iliyopo Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani jana tarehe 24/12/2013.
 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon akimwonyesha sehemu ya kukaa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa ajili ya kufanya mazungumzo naye.
 


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na mwenyeji wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon alipomtembelea ofisi kwake jijini New York, Marekani jana 24/12/2013.
 


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Mwenyeji wake,Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Ban Ki Moon mara baada ya kumaliza mazungumzo yao jijini New York, Marekani 24/12/2013.

Bwana Ban Ki Moon alimwalika Rais Kikwete ambapo viongozi hao wawili walijadili masuala mbalimbali ya kimataifa hususan masuala ya amani na ushiriki wa majeshi ya Tanzania katika kudumisha amani sehemu mbalimbali Afrika na katika nchi nyingine duniani. Tanzania ina majeshi ya kulinda amani katika nchi kadhaa ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Darfur nchini Sudan na Lebanon.
Rais Kikwete yupo jijini New York nchini Marekani ambapo anaendelea vyema na ukaguzi wa kawaida wa afya yake.
(Picha na Freddy Maro / Ikulu)

Wednesday, December 18, 2013

Mama Kikwete aitaka jamii kusaidia kuinua elimu ya wanawake

 
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipokewa na Mwanzilishi na Afisa Mtendaji Mkuu wa CEO Clubs Network, Bwana Tareq Ahmed Nizami, mwandaaji mwenza wa Mkutano wa Wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia, 'The Africa -Middle East-Asia' unaofanyika katika Hoteli ya Atlantis The Palm, huko Dubai katika Jamhuri ya Falme za Kiarabu (UAE), tarehe 16.12.2013. Mwandaaji mwingine wa mkutano huo ni Kituo cha Maendeleo ya Kiuchumi na Uongozi (CELD).
 
 
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na Mama Penehupifo Pohamba, Mke wa Rais wa Namibia wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku tatu wa wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia unaofanyika Dubai kuanzia tarehe 16.12.2013.
 
 
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akizungumza na Balozi wa Tanzania katika nchi za Falme ya Kiarabu (UAE) wakati wa sherehe za ufunguzi wa Mkutano wa wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia unaofanyika katika hoteli ya Atlantis The Palm iliyopo Dubai, Jamhuri ya Falme za Kiarabu tarehe 16.12.2013. Kushoto kwa Mama Salma ni Mke wa Rais wa Namibia Mama Penehupifo Pohamba, na wa kwanza ni Mshauri Maalum wa Mama Pohamba Mchungaji Justina Hilukiluah na wa mwanzo kushoto no Bwana Tariq Nizami, Mwanzilishi na Afisa Mtendaji Mkuu wa CEO Clubs Network.
 
 
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwasilisha mada ya Elimu: Key to the Future of Women in Emerging Economies, kwenye mkutano wa siku tatu wa Wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia unaofanyika huko Dubai tarehe 16.12.2013.
 
Mke wa Rais wa Namibia Mama Penehupifo Pohamba akimpongeza Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete baada ya kutoa mada iliyosisimua wajumbe wa Mkutano wa Wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia unafanyika jijini Dubai, Jamhuri ya Falme aza Kiarabu tarehe 16.12.2013.
 
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipiga picha ya pamoja na Mheshimiwa Margaret Zziwa, Spika wa Bunge la Afrika Mashariki. Viongozi hao ni miongoni mwa viongozi wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia wanaohudhuria mkutano wa siku tatu huko Dubai.
 
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akifanya mazungumzo na Dr. Angela Moore, Balozi wa Heshima kutoka Jimbo la Georgia, nchini Marekani wakati wa mkutano wa wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia huko Dubai tarehe 16.12.2013. PICHA NA JOHN LUKUWI

Na Anna Nkinda – Maelezo, Dubai

Serikali , Asasi za kiraia, Sekta binafsi na watu mbalimbali wametakiwa kusaidia kuinua  elimu ya wanawake kwakuwa faida yake ni pana na endelevu na kwa kufanya hivyo watakuwa wameotesha mbegu ambayo matunda yake yatanufaisha ulimwengu kwa kuufanya uwe na ustawi zaidi, amani na utengamano.

Wito huo umetolewa leo  na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwenye mkutano wa siku tatu wa wanawake kutoka nchi za Afrika, Asia na  Mashariki ya Kati unaofanyika katika Hoteli ya Atlantis The Palm  iliyopo Dubai , Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema elimu pekee ndiyo mkombozi wa mwanamke kwa kuwa  husaidia kuboresha afya, uchumi, usalama na hupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto. Husaidia watoto kuwa na lishe bora na kuboresha afya ya uzazi na kupunguza kusambaa kwa maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi.

“Umuhimu wa elimu kwa wasichana na wanawake unafahamika kwetu sote  kwa sababu elimu ni mlango kwa ajili ya fursa na inafaida zaidi katika familia, jamii, nchi na bara zima kwani wanawake walio na elimu ya msingi wanafursa kubwa ya kuepuka umaskini, kuwapatia watoto elimu na  kuongeza kipato chao kwa asilimia 10 hadi 20.

Mtoto aliyezaliwa na mama aliye na elimu ana nafasi zaidi ya kuishi ukilinganisha na aliyezaliwa na mama asiye na elimu, watoto walio na mama mwenye elimu ya msingi walau kwa miaka mitano wananafasi ya asilimia 40 ya kuishi zaidi ya miaka mitano salama pia mwanamke aliyeelimika anauwezekano zaidi kwa asilimia 50 ya watoto wake kupata chanjo dhidi ya maradhi ya utotoni”, alisema Mama Kikwete. 

Kwa upande wa Tanzania Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema  idadi ya watu ni asilimia 44.9 kati ya hao wanawake ni asilimia 51.3 Serikali imepiga hatua kubwa za maendeleo za kuwaendeleza wanawake na tayari imeridhia na kusaini maazimio ya kitaifa na kimataifa yanayukusudia kuendeleza haki za wanawake.

Alisema  Serikali imeanzisha sera, mikakati, sheria na kanuni madhubuti zinazoboresha mazingira wezeshi kwa ajili ya usawa wa kijinsia na kuwekeza rasilimali na nguvu kubwa kuimarisha haki za wanawake, kuboresha majukumu na fursa katika siasa, kijamii na kiuchumi.

Mama Kikwete alisema, “Pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kutoa elimu ya msingi kwa watu wote, kufuta ujinga na kupunguza tofauti za kijinsia bado idadi ya wasichana katika vyuo vya elimu ya juu ni ndogo ukilinganisha na wavulana hii inasababishwa na utoro mashuleni ambao unatokana na tatizo la ujauzito, ndoa za utotoni na mila hatarishi”. 

Kwa upande wake  Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha  Maendeleo ya kiuchumi na Uongozi (CELD) chenye makao yake makuu nchini Nigeria ambao ndiyo waandaaji wa mkutano huo Mama Furo Giami alisema huu si muda wa kujadili mambo ya usawa wa kijinsia bali ni wakati wa kuchukua hatua ili kuona kwamba usawa wa kijinsia unatekelezeka katika jamii.

Alisema takwimu zinaonyesha ifikapo mwaka 2028 asilimia 75 ya wanawake watajihusisha katika biashara Dunia nzima ingawa   hivi sasa wanawake wanamiliki robo ya biashara na nusu ya biashara hizo ni katika kuendeleza masoko na kukua kwa kazi za kiuchumi wanazozifanya.

“Ingawa takwimu hizi zinaonyesha uchumi wa mwanamke utakuwa umekuwa lakini hakuna usawa wa kijinsia kwa mfano idadi ya wanawake ambao ni wakurugenzi watendaji katika makampuni 500 ni chache  kwa mwaka 2012 ilikuwa ni asilimia 4, katika viwanda vya uchumi  asilimia 11.1 na katika masoko idadi ilishuka  hadi kufikia asilimia 7.2”, alisema Mama Giami.

Mkurugenzi huyo Mtendaji alisema wanawake wanatakiwa kupewa nafasi ya uongozi ili waweze kupata maendeleo ya kiuchumi kwa  kuwawezesha kiuchumi  siyo tu kuwapatia haki zao katika sekta za afya na elimu.

Mama Giami alisema, “Viongozi wa nchi zetu wanatakiwa kuwapa wanawake teknolojia, mitaji, kuunga mkono miradi ya kijamii na kudhibiti biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu kwa kufanya hivyo maendeleo yatapatikana . Pia wahakikishe  wanawake siyo kwamba  wanapata nafasi pekee ya uongozi bali wanapata nafasi ya kuchangia katika uchumi wao.

Mada kuu katika mkutano huo ni Uongozi ni Elimu: Ufunguo wa mustakabali wa wanawake katika nchi zenye uchumi unaoibuka ambapo washirikiki kutoka nchi za Afrika, Asia na Mashariki ya Kati walipata nafasi za kujadili mafanikio na changamoto za kuwaendeleza wasichana na wanawake kielimu.

Wednesday, December 11, 2013

MWISHO WA KILA KIUMBE NI KIFO , JENEZA LA MANDELA .

RAIS KIKWETE KATIKA KUMBUKUMBU YA HAYATI NELSON MANDELA

 
Rais Jakaya Kikwete (wa nne kutoka kulia mstari wa pili) akiwa na mkewe mama Salma Kikwete katika ibada ya Kumbukumbu ya Kifo cha aliyekuwa kiongozi mashuhuri wa Afrika Kusini na duniani, Mheshimiwa Nelson R Mandela.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Desemba 10, 2013, ameungana na viongozi wa mataifa mbali mbali duniani na maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini Kuadhimisha Kumbukumbu ya Kifo cha aliyekuwa kiongozi mashuhuri wa Afrika Kusini na duniani, Mheshimiwa Nelson R Mandela.
Maelfu kwa maelfu ya wananchi wamehimili mvua kubwa iliyokuwa inanyesha kwa nguvu kwenye Uwanja wa Michezo wa FNB mjini Johannesburg kumwaga Mzee Mandela ambaye alikuwa ishara kuu ya upinzani wa siasa za ubaguzi wa rangi za makaburu wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mandela ambaye alifariki duniani Ijumaa iliyopita, Desemba 5, 2013, alikuwa Kamanda wa Jeshi la Ukombozi la Chama cha African National Congress la Umkhoto we Sizwe akafungwa jela kwa uhaini kwa miaka 27 na utawala wa Makaburu.
Baada ya kutoka jela mwaka Februari 1990, Mzee Mandela alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini ya mwaka 1994. Lakini Mheshimiwa Mandela alitumikia kipindi kimoja tu cha miaka mitano na kukataa kutumikia kipindi cha pili.
Kiasi cha viongozi 91 kutoka sehemu duniani wamehudhuria Kumbukumbu hiyo iliyokuwa na kila aina ya mchanganyiko wa hisia – wengine wakiwa na majonzi na wengine wakicheza na kuimba kwa muda wote wa shughuli hiyo iliyochukua kiasi cha jumla ya saa tano.
Mbali na Rais Kikwete ambaye amefuatana na Mama Salma Kikwete, marais wengine mashuhuri duniani waliohudhuria Kumbukumbu hiyo ni Mheshimiwa Barack Obama wa Marekani, Mheshimiwa Francois Hollande wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Uingereza, Mheshimiwa David Cameroun na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Ban Ki Moon.
Kumbukumbu hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi wa zamani wa Marekani wakiwemo marais watatu wa zamani wa Marekani – Mheshimiwa Jimmy Carter, Mheshimiwa Bill Clinton na Mheshimiwa George W Bush na mawaziri wakuu wawili wa zamani wa Uingereza, Mheshimiwa Tony Blair na Mheshimiwa Gordon Brown.
Rais Kikwete kesho, Jumatano, Desemba 11, 2013, ataungana na viongozi wenzake katia katika kutoa heshima za mwisho na kuuaga rasmi mwili wa Marehemu Mandela ambao utawekwa kwenye Majengo ya Urais wa Afrika Kusini ya Union Buildings mjini Pretoria.
(Kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais – Pretoria, Afrika Kusini)

Monday, December 09, 2013

RAIS JK AWASILI UWANJA WA UHURU KUONGOZA MAADHIMISHO YA MIAKA 52 YA UHURU WA TANGANYIKA

 
Rais Jakaya Kikwete akiwasili katika Uwanja wa Uhuru kwa maadhimisho ya miaka 52 ya uhuru wa Tanganyika hivi punde.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa sasa amewasili katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kuongoza maadhimisho ya miaka 52 ya uhuru wa Tanganyika uliopatikana Desemba 9, 1961.

Thursday, December 05, 2013

MWENYEKITI WA TANZANIA STUDENT UNION IN EYGPT ( T.S.U)

Mwenyekiti wa Tanzania Student Union in Egypt  ( T.S.U) Ndugu kutura pamoja na wanachama wa Umoja huo Uwanja wa Ndege wa Cairo wakati wa kumsindikiza Ndugu Hussein Mohammad Afif .

Wednesday, December 04, 2013

SAFARI YA NDUGU HUSSEIN MOHAMMAD AFIF KUREJEA TANZANIA.


Al Akhiy Hussein Mohammad Afif katika Picha ya Pamoja akiwa katika Harakati za Mwisho kuliaga Jiji la Cairo Baada ya Kumaliza Masomo yake ya Chuo Al-Azhar , Safari hii ilikuwa 3-12-2013 .

Picha ya Pamoja Wasindikizaji Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Cairo - Misri
Hawa Ni Baadhi ya Ndugu zetu wageni nao walipata Fursa ya Kuja Uwanja wa Ndege kumsindikiza Ndugu yetu Hussein Mohammad Afif akirejea Nyumbani Tanzania.

Monday, December 02, 2013

Dua katika kukumbuka Siku ya Kuzaliwa Bi Salma Rashid Mkwachu Mke wa Rais wa Tanzania Mh Jakaya Mrisho Kikwete.

Mama Salma Rashid Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh , Jakaya Mrisho Kikwete Katika Dua hiyo.
Muongoza Shughuli Sheikh Mohammad Nassor Amran ,akimkaribisha Mama Salma kutoa Neno la kumbukumbu katika Shughuli hiyo.
Mama Salma Akitoa Neno la kumbukumbu katika Shughuli hiyo ya kukumbuka Uzawa wake ambapo anatimiza Miaka 50 , Shughuli hiyo ya Dua ilifanyika Jijini Dar es salaam , Magogoni na kuhudhuliwa na Watu mbalimbali , kwa Niaba ya KKIISLAM BLOG , Tunamtakia Umri mrefu wa Ibada , kheri na FANAKA , AFYA NJEMA na yote yaliyo Mazuri . Amiin

Picha na Mpiga Picha Maalum.

Monday, November 25, 2013

WANAFUNZI WAPYA WA KITANZANIA KUWASILI LEO ASUBUHI NCHINI MISRI




Kundi la Wanafunzi Ishirini wa Kituo cha Kiislamu cha Kimisri kilichopo Chang'ombe Dar es salaam wanaondoka leo usiku kuelekea nchini Misri.

Wanafunzi hao wanakwenda nchini misri kujiunga na chuo Kikuu cha Kiislamu (Azhar Sharif) nchini humo.

"Wanaondoka leo majira ya saa saba usiku kwa ndege ya Egypt Air"alisema Ustaadh Said Zubeir ambaye ni mwalimu mwandamizi wa kituo hicho alipozungumza na Munira blog jioni hii.

Amesema wanatarajiwa kuanza masomo mara baada ya kufika na watasoma kwa miaka saba.

Wanafunzi hao jana walifanyiwa hafla fupi ya kuagwa,hafla ambayo iliongozwa na mudiir wa kituo hicho Dr Osama mahamoud.

Azhar Sharif ni moja katika vyuo vikubwa vinavyoheshimika duniani na vimetoa wanazuoni wengi sana.


 USTAADH MUHAMAD KHAMIS MMOJA YA WANAFUNZI WANAOSAFIRI LEO USIKU AKIFANYA MAHOJIANO NA MWANDISHI WA HABARI NJE YA CHUO CHA KIISLAM CHA KIMISRI,KILICHOPO CHANG'OMBE.
 SHEIKH YAHYA MKALI AKITOA MAELEZO MACHACHE KWA WASAFIRI HAO.

 WANAFUNZI WAKIWA NJE YA CHUO.
Habari na Picha kwa Hisani ya Munira Blog .

Monday, November 11, 2013

YAH: MCHANGO WA UNUNUZI WA JENGO LA MADRASA BUGURUNI, DAR

Al-khayr  Madrasa ilipokuwa mwanzo kabla ya kuuzwa.
Al-khayr  Madrasa ilipo sasa panapotakiwa kuendelezwa.
Al-khayr  Madrasa, iliyoanzishwa mwaka 1980, Buguruni Kisiwani jijini Dar es salaam, Tanzania, imelazimika kuhamishwa sehemu iliyokuwepo kwenda sehemu nyingine kutokana na uboreshaji wa miundombinu ya eneo hilo, mnunuzi wa Madrasa hiyo alinunua kwa Tsh. 30,000,000/= (Milioni thelathini) kutokana na udogo wa eneo.
Na nyumba ambayo imepatikana ni yenye namba  ILALA/BUG/KISW/655. Ina thamani ya Shilingi 50,000,000/= (Milioni hamsini) na tayari zimeshalipwa zile Milioni Thelathini kwa makubaliano ya kumalizia deni la Milioni ishirini ifikapo Tar: 30/02/2014. Mkataba ambao umefanyika Tar:04/04 2013 . Shauri hilo limefanyika mahakama ya hakimu mkazi wa wilaya ya Ilala.
MALENGO
Uongozi wa Al-khayr  Madrasa unakusudia kuanzisha kituo cha kulelea watoto yatima, chekechea pamoja na muendelezo wa Madrasa. Hivyo  basi ndugu zetu waislamu na wasiokuwa waislamu tunaomba  kwa kila atakae guswa na jambo hili atusaidie kwa kadri ya uwezo wake ipatikane hiyo shilingi Milioni 20 tunayodaiwa na mwenye nyumba/eneo, kama inavyoonekana pichani: kwa mawasiliano zaidi wasiliana na uongozi wa madrasa:
O713-898686-Mussa Hamadi Ally
0713-574043-Uwessu Hamidu Belege
0716-178823-Lule Ally Ibrahim

Friday, November 08, 2013

HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, ALIYOITOA BUNGENI KUHUSU JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI, 7 NOVEMBA, 2013, DODOMA

Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
 Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni;
Waheshimiwa Wabunge;
Mabibi na Mabwana;
          Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga muda wenu ili niweze kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu masuala muhimu kwa uhai, ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika;
          Nimeambiwa kuwa taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge, kumekuwepo na dhana mbalimbali.  Wapo waliodhani kuwa nakuja kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa matukio ya wiki chache zilizopita.   Wapo waliodhani nakuja kuzungumzia “Operesheni Tokomeza”.  Tena wapo waliokwenda mbali na kufikiria kuwa nakuja kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge waliotoa maoni yao kuelezea kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni hii muhimu. Na wapo pia waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa majeshi yetu ya Tanzania katika Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.
Mheshimiwa Spika;
          Hayo si makusudio yangu.  Kinachonileta mbele ya Bunge lako Tukufu ni kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika Jumuiya hiyo.  Lakini, kwa sababu ya umuhimu wa masuala hayo niliyoyataja na rai niliyopewa kuwa niyasemee japo kidogo.  Nimeona ni vyema nifanye hivyo.
Mheshimiwa Spika;
  Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, napenda kusema kuwa tumefikia hatua nzuri katika utekelezaji wake.  Kama mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekamilisha, kwa mafanikio, hatua ya mwanzo ya kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka.  Pia walishatoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba na kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya Katiba.  Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi wote, ni Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 15 Desemba 2013 au kabla ya hapo.
Mheshimiwa Spika;
          Kwa upande wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka kwenu yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua zinazofuata.  Jambo la kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni na pili kufanyika kwa marekebisho ya nyongeza ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha utekelezaji wake.  Baada ya Bunge kukamilisha kazi yake hiyo itafuatia uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba ifanyike na kutupatia Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na wananchi katika Kura ya Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani, tutakuwa tumepata Katiba Mpya.  Hivi sasa katika Serikali tunaendelea kufanya tafakuri na tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na Kura ya Maoni kufanyika kwa mafanikio.
Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
          Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa sikukasirishwa na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni kuokoa maliasili za misitu na wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao umefikia kiwango kinachotishia kutoweka kwa raslimali hizo.  Kwa kweli hali inatisha.  Miti inakwisha na ndovu na faru wanaangamia. 
Mheshimiwa Spika;
          Wakati, tunapata Uhuru Tanzania ilikuwa na ndovu waliokadiriwa kuwa takribani 350,000.  Lakini, kwa sababu ya ujangili uliokithiri katika miaka ya 1970 na 1980  ilipofika mwaka 1989 kulikuwa na ndovu wapatao 55,000 tu.  Ilipofikia hali hiyo Serikali ikaanzisha Operesheni Uhai iliyohusisha Jeshi la Ulinzi na kuongozwa na Meja Jenerali  John Walden (ambaye sasa ni marehemu) kuendesha mapambano dhidi ya majangili. Kutokana na hatua hiyo na uamuzi wa Shirika linalosimamia biashara ya wanyama walioko kwenye hatari ya kutoweka (CITES) kupiga marufuku biashara ya pembe za ndovu duniani, idadi ya ndovu nchini iliongezeka na kufikia 110,000 mwaka 2009.
Tumewaomba Fankfurt Zoological Society ambao ni wabia wetu katika uhifadhi wa wanyama pori kwa miaka mingi wafanye sensa maalum ya ndovu katika Hifadhi ya Selous na kote nchini ili tujue hali halisi ikoje.  Kazi hiyo inaendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika; 
  Baada ya mwaka 2009 kumezuka wimbi jipya, tena la nguvu kubwa, la kuua ndovu na faru nchini na kwingineko katika Bara la Afrika ambako wanyama hao wapo.  Idadi kubwa ya meno ya ndovu yaliyokamatwa na yanaoendelea kukamatwa nchini na kwingineko duniani inathibitisha ukweli huo.  Kwa mfano, kati ya mwaka 2010 na Septemba, 2013, hapa nchini, kwa jitihada zetu vipande 3,899 vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo 11,212 na vipande 22 vya pembe za ndovu zilizochakatwa zenye uzito wa kilo 3,978 vilikamatwa.  Aidha, katika kipindi hicho vipande 4,692 vya pembe za ndovu vilivyotokea Tanzania vyenye uzito wa kilo 17,797 vilikamatwa nje ya nchi.     
Mheshimiwa Spika;
          Kama nilivyokwisha sema hapo awali matatizo ya kuuawa kwa wingi kwa ndovu na faru lipo pia katika nchi nyingine Afrika zenye wanyama hao.   Nchi za Gabon, Kenya, Afrika ya Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Zimbabwe, Zambia na nyinginezo nazo zinakabiliwa na matatizo kama yetu.  Tatizo limekuwa kubwa kiasi cha kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kushtuka na kuamua kuingilia kati kwa namna mbili.  Kwanza kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa ndovu na faru katika nchi zenye wanyama hao.  Na, pili, kuchukua hatua thabiti kudhibiti biashara ya meno ya ndovu duniani.  Ni ukweli ulio wazi kuwa kama hakutakuwepo na wanunuzi wa meno ya ndovu na faru hakuna ndovu au faru atakayeuawa.
Mheshimiwa Spika;
 Kutokana na ukweli ulivyo uamuzi wetu wa kuendesha Operesheni Tokomeza ni sahihi kabisa.  Manufaa yaliyopatikana baada ya Operesheni Uhai ya mwaka 1989 yanatupa imani kuwa na safari hii pia tutafanikiwa.  Tusipochukua hatua kama hii sasa ni sawa na kuwapa kibali majangili waendelee kumaliza ndovu na faru nchini.  Hakika wanyama hao watakwisha.  Itakuwa ni aibu kubwa kwetu na historia itatuhukumu vibaya.
Mheshimiwa Spika;
          Tumeyasikia maelezo ya Wabunge kuhusu kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.  Nawaahidi kuwa tutayafanyia kazi.  Serikali imeahirisha kwa muda Operesheni hii ili kujipa muda wa kurekebisha kasoro hizo na kujipanga upya.  Watendaji wasiokuwa waadilifu na wale wasiokuwa waaminifu wataondolewa.  Halikadhalika, kasoro za kimfumo nazo zitasahihishwa ili tutakapoanza upya Operesheni itekelezwe kwa mafanikio yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika;
          Miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa kwa uchungu ni ukamataji wa mifugo iliyokutwa kwenye mapori ya hifadhi za wanyama na vitendo vibaya walivyofanyiwa wenye mifugo na mifugo yenyewe.  Narudia kusisitiza kuwa taarifa zote hizo zitafanyiwa kazi na waliohusika watachukuliwa hatua zipasazo.  Pamoja na hayo, napenda kuwakumbusha ninyi watunga sheria wetu kuwa sheria ya hifadhi za wanyamapori hairuhusu mifugo kuchungwa katika maeneo ya hifadhi. 
Naomba tuwakumbushe wananchi tunaowaongoza wajiepushe na kufanya hivyo.  Ni uvunjifu wa Sheria za nchi.  Naomba pia, wananchi waelimishwe ili wajue kuwa wakifanya hivyo na kukutwa katika maeneo hayo na mifugo yao kuna adhabu iliyotamkwa kwenye sheria.   Hivyo tusiwalaumu wala kuwaona maafisa wanyamapori kuwa ni watu wabaya.  Wanatekeleza Sheria iliyotungwa na Bunge hili.  Pale wanapotenda visivyo tuseme, watawajibishwa ipasavyo.
Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo
Mheshimiwa Spika;
          Mapema mwaka huu (2013) Umoja wa Mataifa uliomba nchi yetu ichangie kikosi kimoja cha wanajeshi katika Brigedi Maalum iliyoundwa na Umoja huo kuongeza nguvu ya kudhibiti waasi Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.  Lengo la msingi ni kuiwezesha nchi hiyo kupata amani ya kudumu ambayo imekosekana kwa muda mrefu kutokana na kuibuka kwa uasi mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika;
          Tulikubali, kwani hata kabla ya kuombwa na Umoja wa Mataifa tulishakubali maombi kama hayo yaliyotolewa kwenye Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu.  Ni miezi saba (tangu Aprili) sasa tangu wanajeshi wetu waende Kongo na wamekuwa wanatekeleza majukumu yao vizuri tena kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu.  Sifa hiyo kwa wanajeshi wetu imekuwa inatolewa na viongozi wa juu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa juu wa Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo (MONUSCO) na viongozi wa juu wa Serikali ya Kongo.
Mheshimiwa Spika;
          Majeshi ya Umoja wa Mataifa hupewa majukumu na mamlaka ya namna mbili.  Yapo yanayopewa jukumu la kulinda amani tu.  Wanajeshi wake huwa hawapewi majukumu ya kimapigano na hata pale wanaposhambuliwa wanatakiwa kujihami tu.  Kwa kawaida majeshi yenye jukumu hili hupelekwa mahali ambapo kumekuwepo na makubaliano ya kuacha mapigano.  Wanapelekwa kusaidia kuona Mkataba unatekelezwa ipasavyo. 
Aina ya pili ni ile ya majeshi yanayopelekwa mahali ambapo hakuna amani hivyo wanapewa jukumu la kuchukua hatua za kufanya amani ipatikane.  Majeshi haya hupewa mamlaka ya kutumia nguvu ya kijeshi dhidi ya wanaosababisha amani ikosekane kama ni lazima kufanya hivyo.  Maana yake ni kwamba wanayo ruhusa kuingia katika mapigano dhidi ya watu au vikundi vinavyovuruga amani.  Tofauti na wenzao wa kundi la kwanza, wanajeshi wa kundi la pili wako kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha au kujeruhiwa kuliko wenzao ingawaje wapo wengi nao wameuawa na kujeruhiwa.
Mheshimiwa Spika; 
Wanajeshi wetu wamekwenda Kongo chini ya utaratibu huu wa pili ambao unahusu kuingia kwenye mapigano dhidi ya waasi kama hapana budi kufanya hivyo.   Wametekeleza majukumu yao vyema na kwa ujasiri mkubwa na weledi wa hali ya juu. Bahati mbaya tumepoteza vijana wetu watatu shupavu.  Daima tutawakumbuka na tutawaenzi ipasavyo mashujaa wetu hawa.  Tuzidi kuwaombea kwa Mola awape mapumziko mema.  Ameen.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mafanikio ya kihistoria waliyoyapata hivi majuzi dhidi ya waasi wa M23.  Tunamtakia yeye na wananchi wa Kongo kila la heri katika kazi ngumu iliyo mbele yao ya kujenga upya eneo hilo na kujenga mahusiano mapya miongoni mwa watu wa Kongo.  Pia nawapongeza sana wanajeshi wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri waliyoifanya iliyowezesha mafanikio kupatikana.   Wanajeshi hao ni kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi wanaoongozwa na Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa JWTZ.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika;
          Kama nilivyosema awali, haya mambo matatu siyo hasa makusudio yangu nilipoomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge wetu.  Nimeyachomekea tu kwa sababu ya umuhimu wake katika jamii kwa wakati tulio nao.  Jambo lililonileta hapa leo ni kuzungumzia hali ilivyo sasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na nafasi ya Tanzania katika Jumuiya hiyo.  Nimeona nifanye hivyo kutokana na maswali mengi ambayo Watanzania wanajiuliza kufuatia matukio ya hivi karibuni ya viongozi wa nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Uganda, Rwanda na Kenya kukutana bila ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania na Burundi.  Viongozi wenzangu hao wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe 24-25 Juni, 2013 mjini Entebbe, Uganda; tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa, Kenya; na tarehe 28 Oktoba, 2013 mjini Kigali, Rwanda.
Mheshimiwa Spika;
          Naomba kwanza niweke wazi jambo moja, kwamba nchi mbili wanachama au zaidi hazikatazwi kuwa na makubaliano ya ushirikiano katika kufanya mambo mbalimbali.  Hata sisi Tanzania tunao ushirikiano wa namna hiyo na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Lakini, nchi wanachama zinatakiwa kufanya hivyo kwa yale mambo ambayo hayako kwenye shughuli za Jumuiya kwa maana kwamba hayamo katika Mkataba au Itifaki au hakuna uamuzi wa msingi uliofanywa na vikao au taasisi za Jumuiya kuyashughulikia.  Pia, tunaweza kufanya hivyo kwa mambo ambayo yalishaamuliwa na Jumuiya yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi yo yote iliyokuwa tayari kutekeleza ama peke yake au kwa kushirikiana na nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika;
          Kwa mujibu wa matamko ya pamoja (Communique) yaliyotolewa baada ya mikutano hiyo, kuna mambo yapatayo manane ya msingi yaliyoamuliwa kufanywa na nchi hizo kwa lengo la kuendeleza utengamano wa nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Mambo hayo ni haya yafuatayo: 
(1)              Kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala,  Kigali  na Bujumbura.
(2)             Ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
(3)             Kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4)             Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru  wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote;
(5)             Kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
(6)             Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist Visa);
(7)             Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao; na
(8)             Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika;
          Ni dhahiri kwamba orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na yale yasiyo ya Jumuiya.  Kwa mfano, mambo manne kati ya hayo manane hayamo kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au kupata ridhaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Jambo la kwanza ni uzalishaji na usambazaji wa umeme.  Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa na akiba ya pamoja ya nguvu ya umeme (East African Power Pool).  Hata hivyo, bado jukumu la kuzalisha na kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama zenyewe kuamua.  Lakini, hivi ndugu zetu hawa wanao muhali kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sote ni wanachama?    
Jambo la pili, ni ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.  Hili si suala la Jumuiya bali la nchi ya Uganda kuamua yenyewe peke yake au kwa kushirikiana na wadau wengine.  Rais Yoweri Museveni alituarifu mpango huo na sote tuliupokea kwa furaha kwamba sasa tutapata mafuta karibu na nyumbani.   Alitualika kushiriki katika ujenzi wake sijui sasa amebadili mawazo kwamba Tanzania siyo muhimu.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la tatu ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Sudani ya Kusini na Uganda.  Hili si jambo linalobanwa na masharti ya Jumuiya. Ni juu ya nchi hizi tatu kuamua kufanya ili kuwezesha mafuta yao kufika kwenye masoko.  Hata hivyo, nimeambiwa kuwa Jumuiya imeshazungumzia bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi Uganda, Rwanda na Burundi kuwa nalo lifike Tanzania kupitia upande wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.  Inaelekea mpango huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika ujenzi wa bomba hilo. 
Mheshimiwa Spika;
Jambo la nne ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa – Kampala – Kigali – Bujumbura.  Hili nalo hatuna tatizo nalo.  Si mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni jambo lililo chini ya mamlaka ya nchi wanachama husika.  Hata hivyo, ni vyema kutambua ujenzi wa miundombinu ya reli, barabara na usafiri wa anga na majini kuunganisha nchi za Afrika Mashariki ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha juu yanayoshughulikiwa na Jumuiya yetu.  Jumuiya hutengeneza mikakati ya pamoja na ndiyo maana tuna East African Railway Masterplan, tuna East African Road Network, na tuna Lake Victoria Development Programme kwa ziwa Victoria. 
Kwa ajili hiyo, nilitegemea kuwa reli ya kutoka Mombasa hadi Kigali na Juba ingekuwa na tawi linalounganisha reli hiyo na reli ya Tanzania kama ilivyo reli ya Moshi – Voi – Taveta aliyotuachia mkoloni. Tulitegemea hivyo kwa minajili ya kuunganisha soko la Afrika Mashariki ambapo naamini Tanzania ni mdau muhimu.  Lakini inaelekea kwa maoni ya wenzetu hivyo sivyo. 
Mheshimiwa Spika;
Lazima nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila sababu ya kuuliza kwa nini wenzetu wameamua kufanya hivi.  Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha Aprili 28, 2013 na Juni 24, 2013 walipokutana kuamua kufanya mambo ya kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kubaguana,  Haijawahi kuwa hivi kabla.   
Mheshimiwa Spika;
          Katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa utaratibu wake wa utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hatuna maneno nayo.  Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria na Visa ya Pamoja ya Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa tayari waanze.  Lakini, kwa upande wa kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory) na Shirikisho la Afrika Mashariki tunadhani wenzetu wamekiuka uamuzi wetu wa pamoja.
Mheshimiwa Spika;
          Katika Mkutano Maalum wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 28 Aprili, 2012 Jijini Arusha, tulipokea na kuridhia mapendekezo ya kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory).  Kwa mujibu wa mapendekezo hayo kila nchi mwanachama itasimamia shughuli zake za kiforodha na kukusanya mapato yake kama ilivyo sasa.  Hata hivyo, kwa bidhaa zinazopitia nchi moja kwenda nchi nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji wa mapato utafanyika katika kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia.  Mapato hayo yatawasilishwa kwa nchi husika baada ya kuthibitisha kuwa bidhaa zilivuka mpaka. 
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza la Mawaziri kuunda Kikosi Kazi cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji wa mfumo huo.  Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa kutolewa katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 30 Novemba, 2013.  Iweje leo nchi tatu wanachama ziamue peke yao kuanza kutekeleza?  Wanatekeleza nini na kwa nini wafanye hivyo? 
 
Mheshimiwa Spika;
          Kuhusu Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki hadithi yake inafanana na hii ya Himaya ya Forodha.  Katika Mkutano wa 14  wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2012, Nairobi, tulipokea taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kutaka kuanzishwa kwa Shirikisho.   Mkutano huo uliagiza nchi wanachama kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi wa kufikia Shirikisho la Kisiasa na mpango wa kutekeleza mapendekezo mengine yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu.  Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri litawasilisha mapendekezo ya majadiliano hayo katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi mwezi Novemba, 2013.  Iweje leo wenzetu hawa waamue kuanzisha mchakato wao wa kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki.   
Mheshimiwa Spika;
     Kwa kweli huwa najiuliza maswali mengi na kukosa majibu kuhusu nini kinachoendelea kufanywa na viongozi wenzangu watatu na kwa nini!  Nakosa majibu ya uhakika.  Je wenzetu wamekosa imani na Jumuiya ya Afrika Mashariki na je wanataka kuunda yao?  Je wanaichukia nchi yetu na hivyo wameamua kutufanyia vitimbi tutoke!  Au sijui wanachuki na mimi!  Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa hatuna mpango wa kutoka (kama vijana wasemavyo hatoki mtu hapa).  Tupo na tutaendelea kuwepo!  
Mheshimiwa Spika;
          Tanzania haijafanya jambo lo lote baya dhidi ya Jumuiya au nchi yo yote mwanachama.  Na ukweli ni kwamba ni mwanachama mvumilivu, mtiifu na mwaminifu kwa Jumuiya.  Tunatimiza ipasavyo wajibu wetu kwa Jumuiya na kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wake na utengamano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Sabahu ya wenzetu watatu kuamua kufanya mambo yahusuyo Jumuiya yetu peke yao kwa kweli haieleweki.   
Mheshimiwa Spika;
Tunasikia eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini wengine hatupo wakasema kuwa wao wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari tutajiunga.  Yaani wana Umoja wa Waliokuwa Tayari (Coalition of the Willing).  Hivi ni nani hayuko tayari (who is not willing?)  Haiwezekani watu waitane wenyewe bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao ndiyo wako tayari na kujenga dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao hatuko tayari.  Madai hayo hayana ukweli.  Ni vyema waseme ukweli.  Kama walitualika tukakataa ndiyo wanaweza kusema hayo.        
Mheshimiwa Spika;
Kumekuwepo na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu, eti kwamba Tanzania haina moyo wala dhamira ya dhati ya kuendeleza  utengamano wa Afrika Mashariki.  Kwa sababu hiyo inasemekana eti nchi yetu imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba Tanzania tunawachelewesha wengine kupiga hatua za haraka.  Wanadai kama siyo hivyo Jumuiya ya Afrika Mashariki ingekuwa mbali kwa maendeleo. Maneno hayo yamekuwa yanarudiwa au kujirudia mara nyingi kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu wa Afrika Mashariki na hata kwingineko duniani waamini hivyo.    
Mheshimiwa Spika;
Napenda kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba madai hayo hayana ukweli wo wote.  Isitoshe hata sababu zinazotolewa kuthibitisha ukweli wake hazina mashiko.  Hazifanani na ukweli kuhusu Tanzania na Watanzania walivyo.  Tanzania ni muumini wa dhati wa umoja na utengamano wa nchi za Afrika Mashariki na Afrika.  Tumethibitisha hivyo kwa vitendo kwa kuunganisha nchi zetu mbili huru yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika na kuwa taifa moja liitwalo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Muungano wa nchi zetu mbili ndio pekee uliodumu kwa muda mrefu kuliko yote Afrika.  
Mheshimiwa Spika; 
 Tanzania ni mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa maana ya kutekeleza Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao na taasisi za Jumuiya.  Kama lipo jambo ambalo hatujalifanya ilivyotakiwa itakuwa ni kwa sababu za msingi na siyo kwa sababu ya kupuuza Jumuiya. Tunaithamini sana Jumuiya na tumeipa kipaumbele cha juu.  Hatuwezi kuhangaika kwa gharama kubwa ya muda wetu, fedha zetu na kutoa mchango wa hali na mali kuianzisha, kujenga na kuifikisha Jumuiya hapa ilipo halafu tuwe ni watu tunaoongoza kutokuipenda na kudhoofisha maendeleo na ustawi wake. Ni maneno ya kushangaza na wala hayaingii akilini.  Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi.
Mheshimiwa Spika;
          Nionavyo mimi msimamo wetu kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira, uhamiaji, pengine ndiyo yanayotuletea hisia zisizokuwa sahihi juu yetu.  Mimi siamini kama kuna mengine.  Hata hivyo, napata taabu kuamini kwamba kutofautiana kwa mawazo katika mambo hayo kutapelekea baadhi ya wenzetu wasipende hata kushirikiana nasi kwa mambo ambayo hayana matatizo na tumekuwa tunashirikiana vizuri. 
Mheshimiwa Spika;
Tanzania imekuwa inawasihi wanachama wenzetu kuwa tujenge Jumuiya yetu hatua moja baada ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Hatuna tatizo la kuongeza kasi ya ujenzi wa Jumuiya lakini tusivuke hatua yo yote.  Tusiende kasi ya kupindukia. Mkataba unaelekeza tunaanza na Umoja wa Forodha, inafuatia Soko la Pamoja kisha Umoja wa Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa. 
Mheshimiwa Spika;
          Ni kweli kabisa hatukuunga mkono kuharakisha Shirikisho la Kisasa kabla ya kukamilisha baadhi ya hatua.  Na, tulifanya hivyo kwa nia njema ya kutaka Shirikisho lijengwe juu ya msingi imara.  Na, msingi huo si mwingine bali utengamano wa kiuchumi kwa maana ya Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa Kifedha zilizojengeka vizuri na kufanya kazi ipasavyo na kunufaisha wanachama wote sawia.
Mheshimiwa Spika;


          Lazima tutambue ukweli kuwa kunufaika kiuchumi ndicho kichocheo kikubwa cha nchi kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa Jumuiya yetu.  Kama mambo ya kiuchumi yakipangika vizuri na kila nchi ikanufaika sawia, unajenga msingi imara kwa Shirikisho la Kisiasa kustawi na kudumu.  Kama ngazi hizi tatu za awali hazitashughulikiwa vizuri na nchi wanachama zikahisi hazinufaiki ipasavyo, Shirikisho litayumba au kuyumbishwa hivyo kudumu kwake kutakuwa kwa mashaka.
Mheshimiwa Spika;
          Tanzania ni kati ya zile nchi zinazotaka ngazi zote za mchakato wa utengamano zitekelezwe moja baada ya nyingine bila kuruka hata moja.  Kwa msimamo na mtazamo wetu,  Shirikisho iwe ndiyo hatua ya mwisho.  Na huo siyo msimamo wangu au wa Serikali peke yake, ndiyo msimamo wa Watanzania walio wengi.
          Bila ya shaka sote tutakumbuka kuwa mwaka 2006 Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya waliunda Kamati Maalum katika kila nchi kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki.  Kwa hapa nchini Kamati hiyo iliongozwa na Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa yake,  Kamati ilieleza kuwa asilimia 74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo waliunga mkono kuharakishwa kwake. 
Mheshimiwa Spika;
          Takwimu hizi zinaelezea ukweli kuhusu hisia za Watanzania, kuhusu kuwepo kwa Shirikisho na kasi ya utekelezaji wake.  Watanzania wengi sana wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki lakini wanataka jambo hilo lisifanywe haraka haraka.  Wanataka lifanywe kwa umakini mkubwa na tuende hatua kwa hatua kama ilivyoainishwa katika Mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
          Sera na msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakwenda sambamba na ile ya wananchi wa Tanzania.  Ndiyo maana tumeafiki mapendekezo ya Kamati ile ya mwaka 2004 iliyoongozwa na Mheshimiwa Amos Wako wakati ule akiwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya.  Kamati hiyo iliundwa kupendekeza namna ya kuharakisha utekelezaji wa mchakato wa utengamano wa Afrika Mashariki.
          Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umetamka muda wa kutekeleza ngazi ya Umoja wa Forodha lakini uko kimya kuhusu ngazi zilizofuata.  Ili kuondoa kasoro hiyo na kwa nia ya kuharakisha Shirikisho Kamati ilipewa jukumu la kutoa maoni na mapendekezo juu ya namna ya kufanya hivyo.  Kamati ilifanya kazi nzuri ya kupata maoni na hisia za watu wa makundi mbalimbali katika nchi wanachama kuhusu ujenzi wa Jumuiya na utengamano.
Mheshimiwa Spika;
          Kwa upande wa Tanzania kwa mfano, Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako ilitambua hisia za Watanzania kuhusu ardhi na ajira na kupendekezwa kuwa masuala hayo yabaki kwenye mamlaka ya nchi wanachama kuamua.  Kuhusu mchakato wa utengamano Kamati ilipendekeza kwanza kwamba mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Forodha uachwe mpaka ufike ukomo wake wa miaka mitano.  Baada ya hapo muda wa kutekelezwa ngazi zinazofuata unaweza kupunguzwa.  Kwa mfano walipendekeza kuwa matayarisho ya kuunda Soko la Pamoja yaanze hata kabla ya mchakato wa Umoja wa Forodha kufika mwisho ili mara wakati huo ukifikiwa Soko la Pamoja linaanze.  Hivyo hivyo mara baada ya ngazi hiyo kuanza matayarisho ya kuanza ngazi ya Umoja wa Kifedha yanaanza.  Ngazi hiyo nayo ikianza matayarisho ya kuunda Shirikisho yanaanza.  Kamati pia imetoa mapendekezo ya namna ya kufikia uamuzi kuhusu Shirikisho kwamba wananchi wa nchi wanachama wataamua kwa kura.  Tukifuata mapendekezo ya Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako na wenzake kama tufanyavyo sasa Tanzania haina matatizo nayo.
Mheshimiwa Spika;
          Baada ya kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na wana-Afrika Mashariki kuhusu ujenzi wa Jumuiya yao inasikitisha kuona vinafanyika vitendo vinavyoanzisha mivutano kuhusu mambo yaliyokwisha fanyiwa kazi na kuamuliwa.  Tunapata taabu zaidi pale watu wanapobagua wenzao na wanapofanya mambo yanayopingana na Mkataba wa Jumuiya na Itifaki zake.  Kwa kweli kama mwenendo huu hautabadilika sijui mambo yatakuwaje mbele ya safari. 
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyo imara na iliyo endelevu.  Jumuiya ambayo inaendeshwa vizuri, mambo yake ni mazuri na nchi zote wanachama na watu wake wananufaika nayo, na hivyo wanaifurahia.  Tanzania haina tatizo na kuharakisha mchakato wa utengamano, lakini tunapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla hazijakamilika.   Tunawaomba wenzetu kuwa makini katika kila hatua tunayochukua.  Bila ya kufanya hivyo,  Jumuiya yetu itakuwa imejengeka katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa na changamoto nyingi.  Hatupendi ya mwaka 1977 yatokee tena.
Mheshimiwa Spika;
          Napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kuzingatia matakwa ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki zake.   Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa Jumuiya haidhoofiki wala kufa.  Na iwapo itadhoofika au kufa kamwe hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo chake.  Ndiyo maana, hatutachoka kuzungumza na wenzetu kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki inaendelea kustawi. 
Tutaendelea kukumbushana umuhimu wa kufanya mambo yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza kubomoa.  Tutakumbushana umuhimu wa kuheshimu matakwa na masharti ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao rasmi na asasi za Jumuiya.  Tukifanya hivyo Jumuiya ya Afrika ya Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi wanachama na watu wake kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa kwake.   
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Idumu Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika na
Waheshimiwa Wabunge;

                   Asanteni sana kwa kunisikiliza.